1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meya wa Caracas mbaroni

20 Februari 2015

Polisi Ijumaa(20.02.2015) imeingia kwa nguvu kwenye ofisi ya Meya wa Caracas Antonio Ledezma na kumkamata mkosoaji huyo wa muda mrefu wa serikali jambo ambalo limeongeza hali ya mvutano nchini humo.

https://p.dw.com/p/1EfEM
Meya wa mji mkuu wa Venezuela Caracas Antonio Ledezma.
Meya wa mji mkuu wa Venezuela Caracas Antonio Ledezma.Picha: picture-alliance/dpa

Kukamatwa kwa meya huyo kumekuja katika siku ya maadhimisho ya mwaka mmoja tangu kuzuka kwa maandamano dhidi ya serikali ambayo yalisitisha takribani shughuli zote nchini humo.

Wananchi kadhaa walikusanyika wakati wa usiku nje ya makao makuu ya shirika la ujasusi la polisi mjini Caracas ambako inaaminika meya huyo anashikiliwa.

Mara baada ya habari za kukamatwa kwa meya huyo zilipoanza kuvuja katika mji mkuu huo wanancchi walianza kwa pamoja kugongesha vyombo vyao madirishani kupinga kukamatwa kwake wakati madereva wa magari wakiliza honi zao.

Kukamatwa kwa meya huyo Antonio Ledezma kumenaswa kwenye video ya uchunguzi ambapo sehemu za video hiyo zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kundi la wanaume waliokuwa wamevalia mavazi meusi na rangi ya kijivu na fulana za kujikinga na risasi walionekana wakimchukuwa kwa nguvu meye huyo mpinzani mwenye umri wa miaka 59 kutoka kwenye jengo lake.

Meya anyakuliwa

Mfanyakazi wa timu ya usalama ya meya huyo ambaye haruhusiwi kutaja jina lake amesema maafisa waliokuwa na silaha baadhi yao wakiwa wamefunika nyuso zao walitumia silaha zao kuvunja mlango wa ofisi ya meya huyo na kumbwakuwa.

Maandamano ya upinzani Caracas. (18.02.2015)
Maandamano ya upinzani Caracas. (18.02.2015)Picha: picture-alliance/dpa/M. Quintero

Mbunge wa upinzani Ismael Garcia ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter kwamba ameshuhudia Ledezma akichukuliwa kutoka ofisini mwake kama vile mbwa.

Mke wa meya huyo Mitizi Capriles amemwitika dhamana Rais Maduro binafsi kwa usalama wa mume wake.

Rais amshutumu kwa njama ya mapinduzi

Wiki iliopita Rais Nicolas Maduro wa Venezuela alimtaja Ledezma kuwa miongoni mwa wapinzani wa serikali na kumshutumu pamoja na mataifa ya magharibi kula njama ya kufanya mapinduzi ya kuiangusha serikali ya nchi hiyo hiyo ikiwa ni mojawapo ya kauli kadhaa anazozitowa kiongozi huyo tokea ashike madaraka hapo mwaka 2013.Ledezma alizidhihaki tuhuma hizo katika mahojiano mbali mbali kwa kusema kwamba kitu hasa kinachoiyumbisha Venezuela ni rushwa ilioko serikalini.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.Picha: picture-alliance/dpa/S. Donaire

Mara baada ya kukamatwa kwa meya huyo Rais Maduro alisikika kwenye televisheni na radio akimsakama Ledezma kwa kusema kwamba atawajibishwa kwa kujaribu kuchochea machafuko nchini Venezuela nchi ambayo inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeziita tuhuma za serikali ya Venezuela za kuwepo njama ya mapinduzi kuwa hazina msingi na ni uzushi na kusema kwamba zimekusudia kundowa nadhari kutoka kwenye matatizo ya kiuchumi yanayozidi kuongezeka kama vile uhaba mkubwa wa bidhaa kila mahala na kupanda kwa gharama za maisha kulikofia asilimia 68 mwaka jana.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AP
Mhariri: Mohammed Khelef