1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meya wa London ataka iwepo kura ya pili kuhusu Brexit.

Daniel Gakuba
16 Septemba 2018

Meya wa London Sadiq Khan amesisitiza ifanyike kwa mara nyingine tena kura ya maoni juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya. Kiongozi huyo amesema serikali imeshindwa kuendesha majadiliano na Umoja wa Ulaya ipasavyo.

https://p.dw.com/p/34x5v
Pakistan - Sadiq Aman Khan -  britischer Politiker der Labour Party und Bürgermeister von London
Sadiq Khan, Meya wa jiji la LondonPicha: DW/R. Saeed

Meya Sadiq Khan amesema nafasi za ajira, uchumi na kiwango cha maisha ya Waingereza ni muhimu sana kuliko kuchukuliwa  uamuzi wa nchi yake kujiondoa Umoja wa Ulaya katika mchakato wa Brexit kabla ya kuwahoji tena wananchi.

Khan ameyaandika hayo kwenye safu ya wageni katika gazeti la Observer. Amesema jiji la London ambalo ni kitovu cha masuala ya uchumi na fedha litaathirika sana baada ya Brexit.

Uingereza inatarajiwa kuondoka katika Umoja wa Ulaya ifikapo Machi 29, 2019, lakini wakati mkakati wa Waziri Mkuu Theresa May kuhusu Brexit ukipingwa, baadhi ya wabunge na viongozi wa kibiashara wanataka wananchi wawe na kauli kuhusu makubaliano ya mwisho yatakayofikiwa kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Waziri Mkuu May hataki kura nyingine

Mara kadhaa, Bi Theresa May ametupilia mbali miito ya kufanyika kura ya pili ya maoni kuhusu Brexit. Yeye anasisitiza kuwa wabunge watapiga kura ya kukubali au kukataa makubaliano ya mwisho.

Großbritannien Premierministerin Theresa May
Theresa May, Waziri Mkuu wa UingerezaPicha: picture-alliance/Pa Wire/S. Rousseau

Mmoja wa wanachama mashuhuri wa chama cha upinzani - Labour anaunga mkono raia ya Meya Khan, hali inayomwekea shinikizo kiongozi wa chama hicho Jeremy Corbyn kubadilisha msimamo wa chama hicho katika mkutano wake wa mwaka utakaofanyika wiki ijayo.

Chama cha Labour chatakiwa kuchukua msimamo

Kura ya pili ya maoni, inayojulikana kama 'Kura ya wananchi' sio sera rasmi ya chama cha Labour, lakini msemaji wa kitengo cha fedha ndani ya chama hicho John McDonnell alisema mwezi uliopita, kwamba yote yanawezekana.

Akitetea wito wake wa kura nyingine ya maoni kuhusu Brexit, Sadiq Khan amesema serikali imeshindwa kuendesha majadiliano ipasavyo, na kuongeza kwamba kitisho kinachozikabili sekta za ajira na kiwango cha ubora wa maisha ni kikubwa, na kwamba lazima wapiga kura wawe na kauli ya mwisho.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre,dpae

Mhariri: Zainab Aziz