1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Albert wa pili wa Ubeligiji ziarani katika jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo

Oumilkher Hamidou29 Juni 2010

Wakongomani wajkiandaa kuadhimisha miaka 50 tangu walipojipatia uhuru wao kutoka Ubeligiji

https://p.dw.com/p/O5e1
Rais Joseph Kabila wa jamhuri ya kidemokrasi ya KongoPicha: AP Photo

Mfalme Albert II wa Ubeligiji na viongozi wengine wa kimataifa wataadhimisha hapo kesho miaka 50 tangu Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ilipojikomboa toka enzi za ukoloni, ingawa nchi hiyo tajiri kwa maadini ya kila aina imekabwa tangu wakati huo na miongo ya vita, rushwa na umaskini.

Wimbo wa taifa la Kongo ulioimbwa kwa mara ya kwanza June 30 mwaka 1960 unawahimiza wananchi "wanyanyuke na kuijenga nchi kwa amani ili izidi kupendeza kuliko zamani." Matumaini hayo lakini, yametoweka vibaya sana.

Utawala wa miaka 32 wa Mobutu Sese Seko, aliyeingia madarakani mwaka 1965, uliikamua sana Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Ingawa ina akiba kubwa ya madini ya dhahabu, shaba, kobalt na alamasi, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo ni moja wapo ya nchi maskini kabisa za dunia, nchi iliyoathirika na vita vya miaka minane vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2003 na kugharimu maisha ya watu wasiopungua milioni tatu.

Miaka minne baada ya Joseph Kabila kuchaguliwa kuwa rais, imesaidia kuleta utulivu kidogo. Hata hivyo, thuluthi mbili ya wakongomani milioni 60 bado wanalazimika kuishi kwa dala moja na senti 25 kwa siku.

Maaskofu wa Kongo wameandika katika risala yao ya pamoja kuadhimisha miaka 50 ya uhuru kwamba "Ndoto ya Congo inayopendeza imevurugwa".

"Kwa maoni yetu, Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo imerejea nyuma badala ya kusonga mbele," wamesema wachamungu hao.

Ziara ya mfalme Albert wa Pili ni ya kwanza kuwahi kufanywa na mfalme wa Ubeligiji katika koloni lake hilo la zamani tangu miaka 25 iliyopita. Atajiunga na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon, na rais Jacob Zuma wa Afrika kusini katika maadhimisho ya uhuru hapo kesho mjini Kinshasa.

Afrika kusini imezitaja sherehe hizo kuwa ni "tukio muhimu kwa bara lote la Afrika. Hata hivyo, viongozi wa Afrika kusini wameelezea wasi wasi wao kwa kushindwa rais Kabila kurejesha utulivu katika eneo la mashariki la nchi hiyo.

Flüchtlingsfrauen im Kibati Camp im Kongo
Wakinamama walioyapa kisogo maskani yao wamewekwa katika kambi ya KibatiPicha: picture-alliance/ dpa

Ziara ya mfalme Albert II na waziri mkuu aliyejiuzulu, Yves Leterme, inabainisha uhusiano ulioanza upya kuwa mzuri kati Ubeligiji na koloni lake hilo la zamani. Uhusiano huo ulipooza kufuatia lawama za rushwa zilizotolewa na waziri mmoja wa Ubeligiji dhidi ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mfalme Albert wa pili na Vyes Leterne hawapangi kusema chochote hadharani wakati wa ziara hiyo ya siku nne iliyoanza jana usiku mjini Kinshasa. Hata katika karamu ya chakula cha usiku hii leo, mfalme Albert II hajapangiwa kuwahutubia viongozi wa mataifa ya kigeni watakaohudhuria sherehe za miaka 50 ya uhuru wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Na hata katika gwaride la kijeshji la kesho, mfalme Albert II anatazamiwa kuvaa suti tuu badala ya sare ya kijeshi, ingawa yeye binafsi ana cheo cha luteni jenerali na naibu amiri jeshi nchini mwake.

Mfalme Albert wa pili atatumia ziara yake hiyo ya siku nne, miongoni mwa mengineyo, kuitembelea hospitali ya mfalme Baudoin pamoja na shule mjini Kinshasa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Afp,Reuters

Imepitiwa na: Miraji Othman