1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Reginald Mengi afariki dunia

Sudi Mnette
2 Mei 2019

Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania na Reginald Mengi ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa makampuni ya habari ya vyombo vya habari ya IPP amefariki dunia.

https://p.dw.com/p/3HoJF
Tanzania Reginald Mengi
Picha: ITV/Radio

 

Mengi  aliekuwa na umri wa miaka 75, ambae amefahamika sana kutokana na umiliki wa vyombo vya habari vikiwemo radio, magazeti na televisheni amefariki dunia mjini Dubai ambako alikuwa akipatiwa matibabu, kwa mujibu wa moja kati ya makampuni anayoyamiliki.

Kampuni ya uchapishaji wa magazeti ya the Guardian imeandika katika tovuti yake kuwa "tunasikitika kutangaza kifo cha mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi, kilichotokea Dubai Jumatano Jioni."

Rais Magufuli atoa salamu za rambirambi

Tansania Daressalam Präsident John Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John MagufuliPicha: DW/E. Boniphace

Kupitia ukurasa wake wa Twitter rais wa Tanzania John Magufuli ameandika "Nimehuzunishwa na habari  za kifo cha mengi,  siku zote nitamkumbuka kwa mchango wake wa maendeleo ya nchi yetu na mtazamo wake alioundika katika kitabu chake, 'I can, I will, I must,"

Mengi alizaliwa mwaka 1944 katika familia duni mkoani Kilimajaro nchini Tanzania, ambapo baadae alianzisha kampuni ya habari ya IPP ambayo imekuwa ikihudumu nchini Tanzania na baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa jarida la Forbes hadi kifo chake alikuwa anamiliki magazeti 11, radio na vituo vya televisheni.

Aidha ana makampuni yanayotengeneza sabuni, kampuni kubwa zaidi ya maji ya kunywa nchini humo, na alikuwa akijihusisha na biashara ya uchimbani madini kama ya urani, shaba na makaa. Mwaka 2014 aliwekwa nafasi ya 50 miongoni mwa watu matajiri kabisa barani Afrika, akikadariwa kumiliki utajiri wa takribani dola milioni 560.

Kwa mujibu taarifa za vyombo vya habari vya nchini Tanzania Mengi alifariki Dubai Jumatano asubuhi ambako alikuwa anapatiwa matibabu. Marehemu alikuwa na umri wa miaka 75. Kabla ya kuingia katika shughuli za kibiashara marehemu alifanya kazi kwenye kampuni maarufu ya ukaguzi wa mahesabu ya Cooper Brothers. Mengi alisomea taaluma ya uhasibu nchini Uingereza.

Reginald Mengi atakumbukwa sana nchini Tanzania kwa wema wake wa kusaidia makundi mbalimbali ya jamii, na hasa kwa kuwapeleka watoto wenye matatizo ya moyo kwenda kupatiwa matibabu nchini India.