1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfumo wa kuonya mapema Tsunami

23 Desemba 2009

Miezi michache tu baada ya Tsunami kuteketeza zaidi ya maisha ya watu 200,000, kituo cha utafiti wa jiologia GFZ cha Ujerumani kilianza kushughulikia mfumo wa kusaidia kuonya mapema panapozuka hatari ya Tsunami.

https://p.dw.com/p/LCWX
FA technician works on board of German R.V. Sonne as a buoy which will be part of a tsunami warning system developed by GITEWS (German-Indonesian Contribution for the Installation of a Tsunami Warning System) is seen on the background during a installation simulation on Sunda straits off Java island, Indonesia, Tuesday, Nov. 15, 2005. The system developed by German and Indonesian researches, involves sensor on the ocean floor and buoys on the surface of the sea that transmit earthquake and tsunami activity to observation stations. The system is scheduled to be fully installed over the next two weeks. (AP Photo/Fadlan Arman Syam)
Mfanyakazi katika manowari ya Kijerumani R.V.Sonne akitayarisha chombo kimojawapo katika mfumo wa kusaidia kutoa mapema onyo la Tsunami.Picha: AP

Katika kituo hicho kikuu chenye vyombo vya kuonya mapema mabadiliko yanayotokea baharini na kuweza kusababisha Tsunami, kundi la kama watu saba huelekeza macho yao kwenye skrini kubwa iliyo ukutani kutazama tetemeko la ardhi la mwisho lilikotokea nchini Indonesia na lini. Kiongozi wa wafanyakazi hao Bayu Pranata anasema kuwa kwa wastani, kama mitetemeko 40 hutokea kila siku katika kanda hiyo na kuongezea:

"Tunachotaka kujua ni ile mitetemeko inayopindukia 7 katika Kipimo cha Richter na inayotokea si zaidi ya kilomita 70 kwenda chini ya usawa wa bahari. Hali hiyo ikitokea basi ni lazima kukusanya habari zaidi ili kuweza kuamua iwapo wakaazi waonywe juu ya hatari ya kutokea mawimbi ya Tsunami."

Baada ya kukusanya data hizo muhimu, Pranata na wafanyakazi wenzake wana muda wa kama dakika tano tu kuamua iwapo watoe tangazo la kwanza la kuwatahadharisha wakaazi. Uamuzi wa haraka ni muhimu sana.

Zaidi ya asilimia 90 ya mawimbi ya Tsunami husababishwa na mitetemeko ya ardhi inayotokea chini ya bahari. Kwa hivyo, data zinazokusanywa na vyombo maalum vilivyowekwa sehemu mbali mbali nchini Indonesia, ni kiini cha mfumo wa kusaidia kuonya mapema hatari ya kutokea mawimbi ya Tsunami.

Mfumo wa kutoa onyo la Tsunami unahitaji vyombo mbali mbali vinavyoweza kupima kwa haraka mabadiliko yote yanayotokea na kupeleka data hizo upesi iwezekanavyo katika kituo kikuu cha vipimo.Kwa njia hiyo ndio maisha ya binadamu wengi yataweza kunusurika.

Ujenzi wa kituo kikuu cha Ujerumani na Indonesia unatazamiwa kukamilika mwakani katika mwezi wa Machi. Lakini hiyo haimaniishi kuwa wataalamu wa Kijerumani wataondoka moja kwa moja,kwani kuna mipango na mikakati inayohitaji kujadiliwa ili kuhakikisha kuwa mradi huo wa kuwaonya wakaazi mapema vya kutosha utaendelezwa.

Mwandishi: Z.Robina/ZPR/P.Martin

Mhariri: Miraji, Othman