1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro mpya wa kisiasa Zimbabwe.

27 Oktoba 2009

Mugabe na Tsvangirai washindwa kuelewana.

https://p.dw.com/p/KGCL
Mahasimu wawili Tsvangirai(kushoto) na Mugabe.Picha: AP

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na Waziri mkuu Morgan Tsvangirai wameshindwa kufikia maelewano kuutatua mgogoro mpya uliozuka kati yao kuhusu utekelezaji wa masuala muhimu yanayoikabili serikali ya umoja wa taifa ilioundwa mwezi Februari mwaka huu. Hali hiyo ya mkawamo imejitokeza tangu siku 10 zilizopita baada ya Bw Tsvangirai kusema chama chake Movement For Democratic Change-MDC kitasusia vikao vya baraza la mawaziri pamoja na chama cha ZANU-PF cha Rais Mugabe .

Misimamo yao:

Msemaji wa chama cha MDC Nelson Chamisa alinukuliwa na Shirika la Ufaransa AFP akisema kwamba Viongozi hao wakuu wamekutana lakini kwa bahati mbaya hali hiyo ya mkwamo bado inaendelea. Mkutano wao wa muda wa masaa matatu ulikua wa kwanza kati ya mahasimu hao mawili wa muda mrefu, tokea pale Bw Tsvangirai ambaye ni waziri mkuu katika serikali hiyo ya Umoja wa taifa alimauamua kusitisha ushirikiano wote na Rais Mugabe akisema "Si mwaminifu na wala haaminiki." Uamuzi huo alioutangaza tarehe 16 ya mwezi huu umezusha mgogoro mwengine baada ya pande hizo mbili kushirikiana kwa muda wa miezi minane tu.Msemaji wa Rais Mugabe na kambi ya ZANU-PF George Charamba iliuuelezea mkutano huo kuwa kikao cha kawaida cha kila Jumatatu amabacho huzungumzia masuala ya makubaliano yaliofikiwa, lakini msemaji wa Tsvangirai , James Maridadi akasema huo haukua mkutano wa kawaida bali wa kujadili masuala ambayo hadi sasa bado hayajatekelezwa kulingana na makubaliano yaliofikiwa.

SADC Kujaribu kuondoa tafauti:

Kwa upande mwengine kamati ya siasa, ulinzi na usalama ya Jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika-SADC inatarajiwa kukutana mjini Harare Alhamisi ya wiki hi kujaribu kuutatua mgogoro huo mpya, na msemaji wa MDC amesema , ikiwa jumuiya hiyo itashindwa basi hakutokuwa na jengine isipokua kuitishwe uchaguzi mku mpya utakaokua huru na wa haki, chini ya usimamizi wa Jumuiya ya SADC na Umoja wa Afrika , akiongeza kwani " Wao wanaelekea mashariki na sisi magharibi."Kiongozi wa MDC Tsvangirai anasema atashirikiana tena na Mugabe tu ikiwa masuala yaliosalia yatatekelezwa, ambayo ni pamoja na mvutano juu ya kugawana nyadhifa nyengine muhimu pamoja na serikali kusitisha vitendo vya kuwaandama wafuasi wa upinzani. Nyadhifa zinazobishaniwa ni pamoja uteuzi wa magavana wa mikoa na uamuzi wa Mugabe wa kuwateuwa tena Gavana wa Benki kuu Gideon Gono na Mwanasheria mkuu Johannes Tomana bila ya kushauriana na Waziri mkuu Tsvangirai.

Nini itakua hatima ya mgogoro huu:

Bado haijafahamika mgogoro huo utatoa sura gani hatimae kuhusu mustakbali wa serikali hiyo ya Umoja wa kitaifa , lakini Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 85 amenukuliwa na gazeti la serikali Herald akila kiapo kwamba hatoridhia madai ya chama cha MDC. Ama uamuzi wa kusitisha ushirikiano na ZANU-PF na kususia vikao vya baraza la mawaziri, ulitokana na kumakatwa kwa afisa wa MDC Roy Benett ambaye sasa ameachiwa huru kwa dhamana. Bennett ambaye ni mzungu alipendekezwa na MDC kuwa Waziri mdogo wa kilimo, lakini hadi sasa Rais Mugabe amekataa kumuapisha.Chama cha MDC kililalamika mwishoni mwa juma kwamba wabunge wake wanaandamwa na kunyanyaswa na askari wa usalama na kwamba wafuasi wa ZANU-PF na askari wa usalama wenye kupinga kuwepo kwa serikali hiyo ya umoja wa taifa wanahusika na kuvamiwa ofisi ya chama hicho. Polisi walisema waliivamia ofisi hiyo ya MDC, kutafuta silaha.

Mwandishi:Mohamed Abdul-Rahman/afp

Mhariri:Oummilkheir Hamidou