1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Cote d'Ivoire uko pale pale

10 Januari 2011

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ashindwa kumshawishi Gbagbo aachie ngazi, lakini asema inawezekana kuutatua mgogoro huo wa kisiasa. Je ziara yake inafungua njia ya jeshi kuingilia kati?

https://p.dw.com/p/zvtb
Olusegun ObasanjoPicha: AP

"Mgogoro huo unaweza kutatuliwa", ndivyo alivyosema Obasanjo lakini pia hajaondoa uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi, msimamo ambao umekuwa ukitajwa na jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika magharibi, Ecowas, tokea mgogoro huo ulivyoanza baada ya uchaguzi wa Novemba 28 mwaka jana.

Ouattara achoshwa na Diplomasia

Obasanjo alifanya ziara ya ghafla Jumamosi usiku kwenda Cote d'Ivoire na hapo jana alikuwa na mazungumzo na viongozi wote wawili Gbagbo na Ouattara ambaye bado amekwama katika hoteli ya Golf akiwa chini ya ulinzi mkali wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huku pia wanajeshi wanaomtii Gbagbo wakiizingira hoteli hiyo. Ouattara anaonekana ameshakatishwa tamaa na hatua za kidiplomasia katika kuutatua mgogoro huo kutokana na kauli yake hii:

Kombibild Gbagbo und Alassane Ouattara
Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara waendelea kuvutanaPicha: AP/DW

''Nafikiri ni wazi kwamba Laurent Gbagbo hataki kuondoka madarakani. Viongozi watatu wa serikali pamoja na waziri mkuu wa Kenya walikuwa hapa siku kadhaa zilizopita Januari mosi alisema atatoa jibu lake katika siku kadhaa zijazo. Ikiwa ataamua kuondoka madarakani sawa ikiwa hataki nafikiri jumuiya ya Ecowas itachukua hatua mwafaka za kumuondoa madarakani ama kupitia njia maalum ambayo inashughulikiwa na jeshi au nguvu za kijeshi zitatumika. Na sidhani kama jeshi kuingilia kati itakuwa ni tatizo kubwa kwa sababu hii ni njia ambayo imetumika katika nchi zingine barani Afrika na Amerika ya Kusini.''

Jumuiya ya Ecowas ikiongozwa na rais Jonathan Goodluck wa Nigeria imetishia kumuondoa kwa nguvu bwana Gbagbo ikiwa hatoondoka mwenyewe kwa hiari.

Gbagbo adai kuna njama dhidi yake

Hatua ya kutaka kumuondoa madarakani kupitia nguvu za kijeshi imetajwa na Laurent Gbagbo kama kitendo kinachoingilia uhuru wa masuala ya ndani ya Cote d'Ivoire. Obasanjo alipoulizwa ikiwa anaunga mkono hatua ya kijeshi katika mgogoro huo amejibu kwamba ikiwa mahala pana tatizo inabidi kufikiria kutumia njia zote zinazowezekana kutatua tatizo hilo. Kwa maneno mengine ni hatua ambayo inaweza kufikiriwa ikiwa njia zote za kidiplomasia zitashindwa.

Elfenbeinküste Unruhen Dezember 2010
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa walinda Hoteli Golf anakokaa OuattaraPicha: AP

Hadi kufikia sasa Gbagbo amekataa katakata kuachia madaraka ingawa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi na kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa yanaonyesha alishindwa katika uchaguzi wa rais kwa tofauti ya pointi 9 na mpinzani wake Alassane Ouattara anayetambuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa kiongozi mpya wa taifa hilo.

Ziara ya Obasanjo nchini Cote d'Ivoire imetajwa kama ni hatua ya mwisho ya kidiplomasia kabla ya kufikiriwa kutumika nguvu za kijeshi kumuondoa Gbagbo madarakani. Hata hivyo wapo wanaopinga kuutatua mzozo huo kwa njia za kijeshi kama vile rais wa Ghana, John Atta Mills, aliyetangaza hapo Ijumaa kwamba hawezi kupendelea upande mmoja katika mgogoro huo na haamini kama ni mzozo unaohitaji jeshi kuingilia kati. Mpaka sasa ni viongozi wanne wa nchi za Kiafrika waliofika Cote d'voire katika kipindi cha wiki iliyopita kujaribu kuutatua mgogoro huo lakini hakuna aliyefanikiwa.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/RTRE
Mhariri: Josephat Charo