1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Korea waleta wasiwasi wa Kimataifa

Saumu Ramadhani Yusuf25 Novemba 2010

Korea Kaskazini yatoa onyo kwamba itaishambulia tena Korea Kusini

https://p.dw.com/p/QHlY
Kisiwa cha Korea Kusini cha Yeonpyeong karibu na mpaka wa Korea KaskaziniPicha: AP

Korea Kaskazini imeilaumu Korea Kusini pamoja na Marekani kwamba ndizo zilizosababisha hatua yake ya kurusha  mabomu dhidi ya Kusini na kuonya kwamba iko tayari kushambulia tena wakati ambapo  manuari za  Marekani zinaelekea katika rasi ya Korea ambako hali ni tete. Viongozi wa nchi zenye nguvu duniani wanasumbuka vichwa jinsi ya kuushughulikia mgogoro huo pamoja na kuudhibiti utawala wa kikomunisti wa Korea Kaskazini kuhusiana na shambulio lake katika eneo la bahari ya Yellow Sea.

Korea Kaskazini iliyotengwa na jumuiya ya Kimataifa imetoa taarifa ikiinyoshea kidole cha lawama Marekani kwamba haiwezi kuepuka dhamana ya kuhusika na mashambulio ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo vya watu wanne wakati jeshi la Pyongyang lilipovurumisha mabomu katika eneo ambako kuna bahari hiyo inayozozaniwa.

Utawala huo wa Kaskazini pia hakuacha kuitupia maneno jirani yake Korea Kusini.Imeionya nchi hiyo inayoiita kibaraka wa Marekani itafakari  tabia yake la sivyo itajikuta ikishambuliwa tena na tena bila ya uoga.

Südkorea Insel Yeonpyeong Beschuss durch Nordkorea
Picha: AP

Onyo hilo la Korea Kaskazini limekuja wakati ambapo hivi sasa manuari za kijeshi za  Marekani na Korea Kusini zinaelekea katika eneo hilo kwa ajili ya kuanza siku nne za luteka  ya kijeshi kuanzia hapo jumapili,ambayo yatahusisha pia  mashambulio ya angani ya ndege zisizokuwa na rubani.

Ingawa mazoezi hayo ya kijeshi yalikuwa yameshapangwa kufanyika kabla hata ya uchokozi huo wa Korea Kaszini lakini sasa Marekani inataka kuweka wazi kwamba iko tayari kuleta usalama katika eneo hilo kwa kuchukua hatua mwafaka. Ujerumani pia imeitaka nchi hiyo kuzingatia makubaliano ya awali ya kuacha vita.

Aidha taarifa iliyotolewa leo na Korea Kusini  inaeleza kwamba nchi hiyo inapanga kuongeza kwa kiasi kikubwa wanajeshi wake ikiwa ni pamoja na jeshi al nchi kavu katika visiwa vyake vitano vilivyoko kwenye eneo la bahari hiyo ya Yellow Sea.Juu ya hayo Kusini pia imesema imeshaongeza kiwango cha bajeti yake kuelekea mpango wa kuvishughulikia vitisho vya mara kwa mara vya Korea Kaskazini.

Symbolbild Flaggen Europafahne und US-Flagge
Jumuiya ya Kimataifa yaitaka China kuishawishi Korea Kaskazini kuacha uchokoziPicha: picture-alliance/dpa

Tayari Korea Kusini imeshaimarisha idadi ya wanajeshi wake katika bahari hiyo.China inayoonekana kuwa mshirika mkubwa wa Korea Kaskazini imesema kwamba inapinga uchokozi wa kijeshi  katika rasi ya Korea na kuzitolea mwito pande zote mbili kuvumiliana.

Rais Wen Jiabao ambaye yuko Moscow,Urusi amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba katika hali iliyojitokeza sasa katika eneo hilo,ni vyema kwa pande zote husika kujizuia kufanya vitendo vya uchokozi na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kutuliza mvutano huo.

Matamshi hayo ya Wen Jiabao ndio taarifa ya kwanza kutoka China tangu Korea Kaskazini iliposhambulia kisiwa cha Korea Kusini na kuua wanajeshi wawili na raia wawili huku watu wengine 18 wakiwa wamejeruhiwa na wengi kuyakimbia makaazi yao hapo jumanne.

Korea Kaskazini imekataa katakata kuridhia pendekezo la kikosi maalum cha Umoja wa Mataifa kinacholinda amani katika eneo baina ya Korea Kaskazini na Kusini tangu kumalizika vita vya mwaka 1950-1953 vya Korea hizo mbili.

China imetolewa mwito na Marekani pamoja na washirika wake katika eneo hilo Korea Kusini na Japan kusaidia kuikanya Korea Kaskazini na pia kuishawishi irudi haraka katika mazungumzo ya Nuklia ya Pande sita yaliyokwama.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri.Aboubakary Liongo