1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa Mali,Afghanistan ya barani Afrika?

Abdu Said Mtullya24 Oktoba 2012

Hali ya kaskazini mwa Mali ni ya hatari, kiasi kwamba, bila ya msaada wa jumuiya ya kimataifa haiwezi kudhibitika tena.Na uwezekano wa nchi za Afrika magharibi kujiingiza kijeshi katika nchi hiyo unazidi kuwa mkubwa

https://p.dw.com/p/16VT6
Waziri wa mambo yanje wa Ujerumani Guido Westerwelle na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Sahel Romano Prodi
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Sahel Romano ProdiPicha: AFP/Getty Images

Kansela wa Ujerumani pia amesema Ujerumani ipo tayari kutoa mafunzo ya kijeshi ili kusaidia nchini Mali. Hali ya kaskazini mwa Mali imeshaenda mrama. Makundi ya waislamu wenye itikadi kali , yenye uhusiano na al-Qaeda yanawanyanyasa watu. Sehemu hiyo haina polisi tena.Na kwa mujibu wa taarifa wapiganaji wa jihad kutoka nje wanamiminika katika sehemu hiyo.

Watu sasa wanaanza kuiita Mali kuwa ni Afrighanistan-yaani Afghanistan ya barani Afrika kwani uwezekano wa jumuiya ya kimataifa kujiingiza Mali kijeshi unazidi kuwa mkubwa. Ujerumani pia imesema ipo tayari kutoa mafunzo ya kijeshi ili kuisaidia serikali ya Mali katika harakati zake za kupambana na makundi ya watu wenye siasa kali kaskazini mwa nchi hiyo.

Watu katika sehemu hiyo wanaishi katika hali mbaya . Mama mmoja amesema watu wanabakwa, wanapigwa na wanauliwa.Amesema wanaishi katika madhila makubwa. Iwe ni katika mji wa Timbuktu, Gao au Kidal inapepea bendera nyeusi ya waislamu wenye itikadi kali. Watu walioshamiri kwa silaha, wenye vilemba na ndevu ndefu, wanavinjari barabarani katika magari yao. Polisi wao ndiyo wanaotoa mwongozo wa maisha, kwa mujibu wa sheria ya kiislamu.

Sehemu ya kaskazini mwa Mali inadhibitiwa na watawala wapya -yaani Waislamu wenye itikadi kali, kama vile Ansar dine au Wanajihadi wa Mujao,Shule nyingi zimefungwa,watoto wanaandikishwa jeshini kwa nguvu, na wanawake wasiofunika nyuso zao wanakuwa katika hatari ya kutiwa ndani au mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi kwao.

Maafa makubwa yanatokea kaskazini mwa Mali .Watu wanatandikwa viboko kila siku,wanapigwa mawe na wanakatwa sehemu za miili yao.Pamoja na hayo yote Waislamu wenye itikadi kali wanaziteketeza turathi za utamaduni wa dunia.

Lakini jumuiya ya kimataifa sasa haitaki kuendelea kusubiri. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa ridhaa ya kuchukua hatua za kijeshi kaskazini mwa Mali. Umoja wa Afrika na Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi pia zinatayarisha mpango wa kuikomboa Mali ya kaskazini kwa kutumia nguvu za kijeshi. Kamishna wa masuala ya amani na usalama kwenye Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra ameeleza kwamba sasa pana mabadiliko katika msimamo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu mgogoro wa nchini Mali.Amesema kwa kusimama pamoja mgogoro huo utatatuliwa kwa mafanikio.

Lakini jambo moja ni wazi kabisa, kwamba serikali ya Mali haitaweza kuutatua mgogoro wa kaskazini mwa nchi hiyo peke yake.

Mwandishi:Göbel Alexander

Tafsiri:Mtullya abdu.

Mhariri: Gakuba Daniel