1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo kuathiri Kombe la dunia 2010 ?

Ramadhan Ali15 Novemba 2007

kuna kitisho cha mgomo mkuu unaoweza ukachelewesha maandalio ya komb la dunia la kwanza barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHaq

Wakati Ubelgiji na Holland zimetoa rasmi juzi maombi yao kuandaa kwa ubia kombe la dunia kwa 2018 baada ya Brazil, 2014, maandalio ya kombe la kwanza barani Afrika nchini Afrika Kusini, 2010 yameingia mashakani.

Mgomo mkuu unatishia kusimamisha kazi za ujenzi wa viwanja na zana nyengine kwa kombe hilo la dunia.Shirikisho la wafanyikazi wa migodi “National union of Mineworkers” limetangaza mgomo utaanza wiki ijayo na limekwishatoa ilani ya mgomo kama inavyotakiwa na sheria.

Mgomo unaohatarisha kuchelewesha maandalio ya kombe pekee la dunia barani Afrika,unazusha shaka shaka mpya juu ya uwezo wa Afrika wa kuandaa kombe la dunia.Afrika ilipewa jukumu hilo chini ya utaratibu wa zamu kwa kila bara-mfumo ambao sasa rais wa FIFA Sepp Blatter, ametangaza kuuzika kabisa baada ya Brazil kuchomoza nchi pekee iliojitokeza kugombea kuandaa kombe hilo 2014.

Ubelgiji na jirani yake Holland,zimetoa juzi rasmi maombi yao ya kutaka kuandaa kombe hilo la dunia la dimba kwa mwaka 2018 baada ya lile la Brazil huko Amerika Kusini.

Kombe la dunia liliandaliwa na nchi mbili kwa ubia mwaka 2002 –Japan na Korea ya kusini na Uswisi na Austria zitaanda mwakani kwa ubia kombe la Ulaya la mataifa- la pili kwa ukali baada ya kombe la dunia la FIFA ulimwenguni.

Holland na Ubelgiji bila ya shaka zitakumbana na upinzani mkali kutoka Uingereza,ilioandaa mara ya mwisho kombe hilo 1966.China,Australia,Mexico na Marekani,lakini pia Russia na Spain pia zimeonesha hamu ya kuania kuliandaa kombe la dunia 2018.

Kwa sura hii,kwanini Afrika inahatarisha nafasi pekee iliopewa tangu kombe hili kuanzishwa Montevideo,Uruguay, 1930 ?

Ujenzi umeshasimama katika uwanja wa Moses Mabhida Stadium,mojawapo ya viwanja 5 vilivcyojengwa kutoka msingi huko Durban.KJumezuka mzozo huko juu ya malipo-mzozo ambao unawaingiza pia wafanyikazi wanaotumikia miradi mengine ya kombe la dunia 2010.

Miradi hiyo inajumuisha viwanja vyote 10 vinavyojengwa wakati huu ama upya au kufanyiwa ukarabati .Ni pamoja pia na njia ya reli ya Gasuttrain itayounganisha johannesberg na uwanja wa ndege wa King Shaka nje ya Durban.

Muandazi wa mgomo katika mkoa wa Kwazulu-Natal amesema mamia ya wafanyikazi walioandamana na kutoa taarifa ya malalamiko kwa Baraza la jiji la Durban juzi jumatano waweza pia kuchafua kura ya kuamua jinsi timu zitakavyopambana itakayopigwa mwezi huu-Nov. 25.

Wafanyikazi wanadai sehemu ya keki ya Kombe la dunia na hawataki nao kutoka mikono mitupu.

Wakati mwenyekiti wa kamati ya maandalio ya kombe la dunia Afrika Kusini, Danny Jordaan ameomba juzi mabishano yoyote juu ya malipo yasuluhishwe haraka kama iwezekanavyo,viongozi wa vyama vya wafanyikazi wanadai kuwa –waliohusika wanakwepa dhamana zao.wanasema eti “matatizo yetu si matatizo yao.”Kwahivyo, wanauliza na wao kwanini matatizo yao ya kumaliza maandalio ya kombe la dunia kwa wakati yawe matatizo ya wafanyikazi ?

Afrika Kusini imejionea mlolongo wa migomo mikubwa mwaka huu-usoni kabisa ni mgomo wa mwezi mzima wa watumishi serikalini.

Tayari kulikwisha enea uvumi kwamba Afrika Kusini haitakamilisha maandalio ya kombe la dunia 2010 na hii ikapelekea baadhi ya nchi nje ya Afrika kujitolea kuziba pengo na kuandaa.

Tayari ijumaa hii na kesho jumamosi, firimbi Italia kwa duru ya kwanza ya kuania tiketi za kombe la dunia 2010 kanda ya Afrika:Huko Djibouti, wenyeji wanaumana na majirani zao Somalia wakati kesho mjini Moroni,visiwa vya Comoro vina miadi na jirani zao Madagascar.Huko Bissau, Guinea Bissau inacheza na Sierra Leone.