1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa madakitari Kenya na viwavi jeshi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
17 Februari 2017

Mgomo wa madaktari Kenya, suala la wapi zimeishia fedha za wahanga wa mashambulio ya Boko Haram Nigeria, na janga la viwavi hatari kabisa kusini mwa Afrika ni miongoni mwa mada katika Afrika katika magazeti ya Ujerumani

https://p.dw.com/p/2Xkpm
Kenia Demo der Ärzte in Nairobi - Vertretter der KMPDU festgenommen
Picha: Reuters/T. Mukoya

Tunaufungua ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii kwa ripoti ya gazeti la "die Tageszeitung " la mjini Berlin kuhusu mgomo wa madaktari nchini Kenya."Wenye kuongoza mgomo wa madaktari wapelekwa korokoroni" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo la mji mkuu Berlin linalozungumzia mgomo wa miezi miwili wa madaktari na wauguzi . Kwa kukamatwa viongozi saba wa shirika la madakitari wa Kenya, mzozo huo unatishia kuzidi makali limeandika die Tageszeitung lililomnukuu Miriam Muindi, mmojawapo wa wauguzi akielezea shida wanazokabiliana nazo kazini; uhaba wa madawa, vifaa vya matibabu ama havifanyi kazi au hakuna kabisa pamoja na mishahara duni.

Die Tageszeitung linasema madaktari wanalipwa Euro 1300 kwa mwezi na wanadai nyongeza ya asili mia 300. Wanataka yatekelezwe makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 . Mishahara duni ndio chanzo cha madaktari kuhamia ng'ambo. Kwa mujibu wa shirika la afya la Umoja wa mataifa WHO, daktari mmoja nchini Kenya analazimika kuwahudumia wagonjwa elfu tano. Die Tageszeitung linalinganisha na hali nchini Ujerumani ambako daktari mmoja anawahudumia wagonjwa 260.  Itafaa kusema hapa kwamba ripoti ya die Tageszeitung imeandikwa kabla ya mahakama ya Rufaa kuamuru waachiwe huru  viongozi wote 7 wa chama cha madaktari waliohukumiwa  kifungo cha mwezi mmoja gerezani siku ya Jumatatu kwa kukiuka maagizo ya mahakama ya kusitisha mgomo wa madaktari ulioanza mapema mwezi  wa Desemba mwaka jana.

 Misaada ya kiutu haijulikani imekwenda wapi Nigeria

Lilikuwa gazeti hilo hilo la mjini Berlin,die Tageszeitung lililozungumzia kuhusu misaada ya fedha waliyokusudiwa wahanga wa mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram isiyojulikana imechukuliwa na nani. Katika  maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Nigeria yanayogubikwa na mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram, mamilioni ya watu wanategemea misaada ya kiutu. Gavana wa jimbo linaloathirika zaidi la Borno, Kashim Shettima anasema mashirika sita tu kati ya 126 ya misaada ya kiutu ndiyo yanayowajibika. Mashirika hayo ni pamoja na Madaktari wasiokuwa na Mipaka, shirika la kimataifa la msalaba mwekundu, na mengineyo. Mashirika mengine hayajulikani yanafanya nini. Mengi yalipiga kambi katika mji mkuu wa jimbo la Borno Maiduguri tangu mwishoni mwa mwezi wa Agosti mwaka jana.

Na hakuna dalili za mabadiliko-hakuna hata njia moja kuelekea vijijini na usalama ndio kabisa hakuna-watu hawawezi kusafiri hata kilomita 70 kutoka maiduguri kuelekea mji wa Bama bila ya kukabiliana na hatari ya kushambuliwa-linasema die Tageszeitung linalomaliza ripoti yake kwa kukumbusha Nigeria imepokea misaada kadhaa kugharimia miradi ya elimu, afya na maji safi ya kunywa. Hakuna kinachoonekana na ndio maana Hamza B-Lawal wa shirika lisilomilikiwa na serikali Connected develepment amemhakikishia Katrin Gänsler wa die Tageszetung,watafanya kila la kufanya kufahamu fedha za misaada ya kiutu zimemalizikia wapi.

Viwavi jeshi wateketeza mashamba Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazetini ya Ujerumani wiki hii inamulika kitisho kinachosababishwa na janga la viwavi hatari walioingia kusini mwa Afrika kutoka nchi za Latin Amerika."Ni janga kubwa hili,viwavi wanateketeza  mashamba tangu madogo mpaka makubwa" Frankfurter Allgemeine limemnukuuu Gerhard Verdoorn wa kituo cha Griffon Poison Information Center cha Afrika Kusini  akisema. Mbali na mahindi viwavi hao wanateketeza pia nafaka nyengine kadhaa, mboga mboga na majani ambayo ni chakula kikubwa cha mifugo.

Viwavi hao ambao kutokana na kujikusanya kwao makundi makundi, wanajulikana kama "viwavi jeshi" wanaweza kuteremka hadi kundi la viwavi elfu moja  na kuhujumu mita moja ya mraba kwa wakati mmoja. Haijulikani bado viwavi hao hatari wamevuka vipi bahari na kuingia Afrika. Pengine kupitia mazao ya chakula hadi Nigeria. Frankfurter Allgemeine linamalizia ripoti yake kwa kuzungumzia juhudi za serikali za kusini mwa Afrika za kukabiliana na kitisho cha janga la Viwavi jeshi."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri: Gakuba Daniel