1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo waipoozesha Ugiriki

17 Julai 2013

Mgomo wa saa 24 wa wafanyakazi wa sekta ya umma nchini Ugiriki umeipoozesha kabisa nchi hiyo, huku bunge likitarajiwa hivi leo kupitisha mpango unaopingwa na wafanyakazi hao wa kukata nafasi za ajira kwenye serikalini.

https://p.dw.com/p/199U9
Anti-austerity protesters and parliamentarians of the anti-bailout radical leftist SYRIZA party participate in a rally in Athens, July, 16, 2013, during a 24-hour general strike. Trains ground to a halt and hospitals worked with emergency staff as Greek workers went on strike on Tuesday in protest at government plans to fire thousands of public sector employees. REUTERS/John Kolesidis (GREECE - Tags: POLITICS BUSINESS CIVIL UNREST)
Griechenland Generalstreik 16.07.2013Picha: Reuters

Maelfu ya wafanyakazi wenye hasira waliacha ofisi zao na kuandamana mbele ya bunge la Ugiriki hapo jana, dhidi ya mpango wa serikali kuwapunguza wafanyakazi wa sekta ya umma, ili kukidhi matakwa ya wakopeshaji wa kigeni.

Mgomo huo dhidi ya mpango mpya wa kuwahamisha au kuwafukuza kazi wafanyakazi wa serikali ulifanyika siku moja tu kabla ya bunge kuupigia kura mkururo wa mageuzi ambao lazima upitishwe kabla ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa hawaidhinisha msaada zaidi wa kifedha.

Maandamano makubwa kabisa kuwahi kutokea

Zaidi ya waandamanaji 30,000, wakiwemo polisi wa baraza la manispaa na walimu ambao wamelengwa kwenye mpango huo wa kuwafuta au kuwahamisha kikazi, walikusanyika kwenye uwanja wa bunge wakipiga ngoma na kuweka zogo, katika kile kinachotajwa kuwa moja ya maandamano makubwa ya kupinga hatua za kubana matumizi kuwahi kufanyika nchini Ugiriki mwaka huu.

Mgomo mkubwa nchini Ugiriki wa tarehe 16 Julai 2013.
Mgomo mkubwa nchini Ugiriki wa tarehe 16 Julai 2013.Picha: Reuters

Mmoja wa waandamanaji hao, Eleni Fotopoulou, mwenye umri wa miaka 58, aliliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA, kwamba inaonekana kama Ugiriki imeshakuwa maiti na sasa tai wanapigania mzoga wake. Mwanamke huyo ambaye ni mwalimu mstaafu na mama wa watoto wawili, aliongeza "Sina tena hasira, nina fadhaa. Lazima tupambane."

Ugiriki imegawanyika juu ya ikiwa wafanyakazi wa sekta ya umma, ambao kawaida kazi zao zinalindwa na katiba, wanapaswa pia kuyapata maumivu ya kufukuzwa au kuhamishwa kazi, ambayo tayari yamewanamia wale wa sekta binafsi.

Schäuble kupokewa kwa maandamano

Hata hivyo, kimsingi, wote wanakubaliana kwamba jamii ya Ugiriki haiwezi tena kubeba mzigo wa makato zaidi ya matumizi na kupandishiwa kodi. Huo ndio ujumbe ambao serikali ya Ugiriki inasema itampa Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, anayewasili mjini Athens hapo kesho.

Mgomo mkubwa nchini Ugiriki wa tarehe 16 Julai 2013.
Mgomo mkubwa nchini Ugiriki wa tarehe 16 Julai 2013.Picha: Reuters

Kuna uwezekano mkubwa, waandamanaji wakajitokeza tena hapo kesho, kumuonesha Schäuble upinzani wao dhidi ya mpango unaopigiwa chapuo na Ujerumani. Wagiriki wengi wanailaumu Ujerumani kwa mgogoro wao wa kiuchumi na picha zinazomuonesha Kansela Angela Merkel kwenye taswira ya mtawala wa Kinazi zimejaa mjini Athens.

Wakopeshaji wa Ugiriki, ambao tayari mara mbili wameshaipa nchi hiyo fedha zifikiazo euro bilioni 240, wamekasirishwa na kiwango kidogo cha maendeleo kilichopigwa, hasa kwenye suala la kuweka sawa sekta yake ya umma yenye wafanyakazi 600,000, ambayo inaonekana kujaa ufisadi na isiyo ufanisi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman