1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 25 ya Mkataba wa Maastricht

7 Februari 2017

Imetimia miaka 25 tangu uliposainiwa Mkataba wa Maastricht katika mji wenye jina hilo ulioko Uholanzi, karibu na mpaka wa Ujerumani. Mkataba huo ndio uliounda Jumuiya ya Umoja wa Ulaya mwaka 1992.

https://p.dw.com/p/2X5sn
Viongozi wa Ulaya wakisaini Mkataba wa Maastricht
Picha: picture-alliance/dpa

Februari saba mwaka 1992 mji mzima wa Maastricht ulisombwa na hisia ya furaha na matumaini makubwa anasema gavana wa mkoa wa Limborg Theo Bovens. Akizungumza na shirika la habari la AFP amesema mtu angeweza kuihisi ile hali ya kuunga mkono mshikamano wa Umoja wa Ulaya.Kila mtaa ulikuwa ukijinasibisha  na nchi nyingine ya Umoja wa Ulaya, anasema maduka yalikuwa yakipambwa kwa bendera za nchi zote kuanzia Ubelgiji Ujerumani hadi Uingereza. Ni siku kama ya leo katika jengo jipya la mkoa kwenye mji huo wa Maastricht  nchi 12  wakati huo ndizo zilizotia saini makubaliano ya kuwa na Umoja wa Ulaya, makubaliano ambayo yalifungua njia ya kuundwa kwa kile kinachotambulika leo hii kama Umoja wa Ulaya na Umoja wa sarafu ya pamoja ya Euro.

Ikiwa ni miaka 25 imekwisha pita  baada ya misururu ya migogoro, ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa sarafu hiyo ya Euro mgogoro wa kisiasa nchini Ugiriki na mivutano ya kiuchumi wimbi la wahamiaji ambalo halijawahi kutokea tangu vita vya pili vya dunia pamoja na Brexit,mji huo wa Maastricht na wakaazi wake 120,000 wanahisi kwamba mji huo bado una umuhimu mkubwa na hata pengine jukumu la kuufanya Umoja huo uendelee kusimama.

Mustakabali wa Umoja wa Ulaya

Mkataba wa Maastricht unahifadhiwa katika benki moja nchini Uholanzi
Picha: picture-alliance/dpa/EPA/M. van Hoorn

Meya wa Mastricht Annemarie Penn-te Strake anasema kwamba anahisi wanawajibu wa kujaribu kuuwasha tena mshumaa kwa mara nyingine na kuitia nuru ile ndoto inayoendelea kuwepo ya kuhakikisha kwamba Ulaya iliyokuwepo miaka 25 iliyopita ya kuwa na Ulaya moja inaendelea kushamiri tena na sio kuwa jinamizi linalowatia khofu kama ilivyokuwa sasa.Meya huyo anasema kwamba kwakuwa makubaliano ya kuunda Umoja wa Ulaya chumbiko lake ni Maastricht  basi watu wa mji huo wanahisi wana kila sababu ya kulitilia maanani ule ukweli kwamba  wanaishi katika enzi ambazo Ulaya inakabiliwa na matatizo mengi na wasiwasi na mashaka makubwa pamoja na khofu juu yake.

Mamlaka husika zinatowa mwito kwa watu wa Ulaya kurejea  katika mitizamo na maadili yaliyounda mkataba huo ambayo wanakhofia kwamba nyingi ya nchi wanachama wa Umoja huo wa Ulaya wamejitenga nayo. Miongoni mwa mambo yanayoyosisitizwa ni pamoja na kuzingatiwa kwa ile fikra ya watu wa Jumuiya hiyo kujiona kuwa wote ni raia wa Ulaya ili kujenga mwelekeo bora katika kuimarisha mazingira ya kazi na hali ya maisha sambamba na kuibadili mifumo ambayo imegeuka kuwa ya kitaasisi zaidi. Hata hivyo mtaalamu wa masuala ya Ulaya kutoka chuo kikuu cha Maastricht Sophie Vanhoonacker anasema kuelekea katika njia ya kuwa na Umoja wa Ulaya imara na thabiti ni kibarua kigumu katika ulaya hii ambayo imekuwa kubwa lakini pia iliyogawika. Juu ya yote lakini mtaalamu huyo anahisi pia cha muhimu kinachotakiwa kufaniyka ni viongozi wa kisiasa kuchukua hatua na kuwajibika.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba