1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 tangu Ghana kuwa huru na athari zake kwa Bara zima la Afrika

6 Machi 2007

Kama nchi ya kwanza katika bara la Afrika chini ya Jangwa la Sahara, miaka 50 iliopita Ghana ilipata uhuru kutoka ukoloni wa Uengereza. Lakini, kama zilivo nchi kadhaa za Afrika, uhuru mpya wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi umesababisha hali tegemezi mpya pamoja na matatizo mepya ambayo yanabidi yakabiliwe kwa ukakamavu zaidi kuliko ilivyokuwa kabla.

https://p.dw.com/p/CHIp
Wananchi wa Ghana wakishehrekea miaka 50 ya uhuru wa nchi yao.
Wananchi wa Ghana wakishehrekea miaka 50 ya uhuru wa nchi yao.Picha: AP

Mfano mzuri ni Ghana, vipi zinavoweza kufikia nchi ambazo zinaendesha marekebisho, kama vile kuwa na chaguzi huru kwa njia ya demokrasia, uchumi wa kiliberali, magazeti yalio huru pamoja na jumuiya za kiraia zilizo macho kutetea haki na maslahi ya raia. Ghana ni mfano mzuri wa nchi za Kiafrika ambazo, kwa mafanikio, zimejitahidi kujivuwa na makosa ya zamani yaliofanywa na mifumo ya kijamaa, kupambana na rushwa na kuhama kwa wasomi pamoja na kuwapa mustakbali vijana wake.

Hata hivyo, mfano wa Ghana unaonesha pia kwamba kukuwa uchumi kuna mipaka yake katika nchi za Kiafrika zisizokuwa na rasil mali na ambazo zinalazimika kujikwamua. Hali tegemezi mpya, tena inayofuata maagizo ya wafadhili wa misaada ya maendeleo, taasisi za fedha za kimataifa, biashara ya dunia, hivi sasa imechukuwa nafasi ya hali tegemezi ya zamani katika wakati wa ukoloni.

Bado rasil mali ndio sharti muhimu la mafanikio katika nchi za Kiafrika; na mali ghafi za Afrika zitakuwa muhimu zaidi kwa uchumi wa dunia katika miaka ijayo. Madini ya Coltan na dhahabu kutoka Kongo, mafuta kutoka Angola, madini ya Manganese kutoka Gabon, yote hayo yamefanya uchumi wa nchi za Kiafrika zilizo na utajiri wa mali asili ukuwe. Lakini kujikomboa nchi hizo kutokana na umaskini na maendeleo duni kutafikiwa tu ikiwa rasil mali hizo zinaambatana na siasa nzuri. Angola, uchumi wake unapanda kwa asilimia 26 kwa mwaka- kasi kubwa kabisa kushuhudiwa hivi sasa duniani- lakini maskini wa nchi hiyo hawafaidiki kabisa na neema hiyo. Huko utajiri wa nchi hiyo unaifaidia tabaka ya wanasiasa mafisadi.

Pia mikakati yenye nia njema ya misaada ya maendeleo haijaweza kuzikomboa nchi nyingi za Kiafrika. Zaidi ya nusu ya fedha zinazotiririka barani Afrika ni zile za misaada ya maendeleo. Uwekezaji wa kweli wa kiuchumi ungekuwa muhimu zaidi na ungezifanya nchi hizo zijitegemee zaidi. Huenda wafadhili hao huwategemea watekelezaji wasiofaa, tawala zilizo fisadi sana na maimla.

Wale waliolemaa na misaada ya maendeleo mara nyingi hawajajifunza kuchukuwa dhamana mikononi mwao. Kwanini huko Senegal nusu ya watoto hawaendi shule, licha ya kwamba wafadhili wamewekeza katika sekta ya elimu? Kwa nini katika Kenya kila mwaka bado hakuzuliwi watu kufa kutokana na njaa, kwa vile kunakosekana miundo mbinu na mifumo ya usambazaji? Kwa nini utawala fisadi wa Ethiopia unawapiga marungu waandamanaji katika mji mkuu wa Addisababa, unawaweka watu hao vizuizini kwenye kambi za mateso, na bado utawala huo huo utegemee kwamba miradi yake itazidi kuendelezwa kwa msaada wa wafadhili.

Hali katika nchi za Kiafrika, chini ya jangwa la Sahara, imeboreka sana katika miaka 15 iliopita. Mabadiliko kutoka tawala za kiimla na kuja mifumo ya kidimokrasia imeshuhudiwa Benin, Mali, Msumbiji, Namibia na Afrika Kusini. Vita virefu vya kienyeji katika Liberia na Sierra Leone vimekoma. Afrika inataka kujiamulia yenyewe namna ya kuitanzua mizozo ilioko- ile ya usalama na kukanyagwa vibaya haki za binadamu- labda kwa ujiingizaji wa kijeshi.

Baada ya kumalizika vita baridi, Afrika ilipotea katika ajenda ya siasa za kimataifa. Lakini tangu kuanza karne mpya mambo yamebadilika. Mataifa ya zamani yaliokuwa na ushawishi, kama vile Marekani au Uengereza, yamezidisha ushawishi huo, na wadau wengine, kama vile China, zinajiingiza kwa nguvu katika bara la Afrika. Maslahi yao yanafanana: kwanza kupata rasil mali kwa bei nafuu na baadae kuituliza mizozo na michafuko.

Na kuna sababu nyingine kwanini sasa Afrika iko katika macho ya siasa za kimataifa. Imetambuliwa kwamba masuala muhimu ya mustakbali wa mwanadamu- hasa hali ya hewa na pia magonjwa ya kuambukiza, uhamiaji wa watu- hayawezi kupatiwa majibu bila ya Afrika. Masuala ya mustakbali wa dunia yanaweza tu kutanzuliwa kwa pamoja, haiwezi nchi yeyote kuibadilisha hali hiyo bila ya kuitegemea nchi nyingine.