1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michael Bloomberg kupiganaia kiti cha rais wa Marekani

Oumilkheir Hamidou
25 Novemba 2019

Matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake, kinyang'anyiro cha kiti cha rais wa Marekani, bilioneya Michael Bloomberg apania kushindana na Donald Trump na mkutano mkuu wa chama cha CDU ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3Tf6Q
USA | New Yorker Ex-Bürgermeister Michael Bloomberg
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. M. Ebenhack

Tunaanza na siku ya kimataifa dhidi ya kutumiliwa nguvu wanawake. Gazeti la Badische Zeitung linaandika:"Tatizo kubwa wanalokabiliana nalo wale wanaotaka wasaidiwe linatokana na uhaba wa mapendekezo ya misaada ambayo tokea hapo haitoshi. Kuna upungufu wa vituo karibu 15000 vya kuwapokea wanawake kote nchini Ujerumani. Picha gani anaipata mwanamke anaejikuta katika hali ya vitisho vya kupigwa na kuteswa , anapotambuwa kwamba  ingawa vituo vya kuwapokea wanawake walioko katika balaa la kupigwa viko, lakini nafasi ya kumpokea hakuna? Ni vizuri kwamba waziri wa familia Franziska Giffey anajaribu kuanzisha mradi wa uwekezaji kwa lengo la kukabiliana na hali hiyo."

Tajiri Bloomberg kuania tikiti ya chama cha Democrat kwaajili ya uchaguzi wa rais Marekani

Kinyang'anyiro cha kuania kiti cha rais wa Marekani kimepamba moto. Katika wakati ambapo mchakato uliolengwa kumvuwa wadhifa wake rais wa Marekani Donald Trump unaendelea katika baraza la wawakilishi, tajiri mkubwa, aliyewahi kuwa meya wa jiji la New-York, Michael Bloomberg ajimwaga katika mashindano ya kuania tikiti ya chama cha Democrat kwa uchaguzi wa rais. Gazeti la "Reutlinger General Anzeiger"  linaandika:"Akiwa muasisi wa milki mojawapo kubwa kabisa inayochanganya pia kituo cha televisheni cha Bloomberg TV, meya huyo wa zamani wa jiji la New-York ameshajijenga katika ufundi wa vyombo vya habari. Ingawa amekawia kujibwaga katika kampeni za mwanzo za chama cha Democrat, hata hivyo ni mashuhuri kote nchini. Hatokawia kukamata nafasi ya mbele kati ya wagombea 20 wa chama cha Democrat. Shida yake kubwa ni umri wake tu. Kinachostaajabisha kusema kweli ni kwamba hakuna  mgombea kijana wa chama cha Democrat aliyejitokeza hadi wakati huu-kama ilivyokuwa wakati wa Barack Obama au Bill Clinton. Kabla ya Bloomberg kujibwaga ringini, Trump alianza kumdhihakii-ushahidi timamu kwamba anamuogopa."

 

Markus Söder anyemelea wadhifa wa kansela

Tunamaliza kwa mkutano mkuu wa chama cha kihafidhina cha CDU mjini Leipzig ambapo gazeti la "Der neue Tag linamulika zaidi jinsi mwenyekiti wa chama ndugu cha CSU, Markus Söder alivyojitokeza katika mkutano huo. Gazeti linaandika:"Katika mkutano mkuu wa CDU mjini Leipzig picha moja tu ndio iliyosalia vichwani mwa watu; picha ya chama kinachotanga tanga kumtafuta muokozi. Hivyo ndivyo inavyotafsirika shauku kubwa waliyokuwa nayo wajumbe walipomkaribisha  waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Söder jumamosi iliyopita. Ikiwa Söder amejiwekea matumaini ya kichini chini ya kugombea kiti cha kansela kwa tikiti ya vyama ndugu vya CDU/CSU uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwaka 2021, basi atafanya vizuri akiendelea kuyaweka siri angalao kwa sasa."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/INlandspresse

Mhariri: Grace Patricia Kabogo