1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michel Barnier:Uingereza hatarini kutoka EU bila makubaliano

Angela Mdungu
2 Aprili 2019

Kiongozi mkuu wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya katika suala la Brexit Michel Barnier ameonya kwamba kadri siku zinavyozidi kusogea Uingereza inazidi kujiweka katika hatari ya kuondoka umoja wa Ulaya bila makubaliano

https://p.dw.com/p/3G4XF
EU-Gipfel Brexit in Brüssel | Michel Barnier
Picha: Reuters/T. Melville

Barnier ameyasema hayo mjini Brussels, siku moja baada ya wabunge wa Uingereza kushindwa kuungana ili kupitisha mpango wa kujitoa uliofikiwa na Waziri mkuu Theresa May mwaka uliopita.

Mjumbe huyo wa majadiliano wa Umoja wa Ulaya amesema, umoja huo hauna nia ya kutengana na Uingereza bila makubaliano maalumu lakini wako tayari kufanya hivyo kutokana na hali ilivyo hivi sasa. Barnier ameongeza kuwa ingawa mchakato wa Brexit umekuwa mgumu kutekelezeka, Umoja wa Ulaya uko imara.

Akizungumzia mchakato huo Barnier amesema, Bunge la Uingereza limekuwa likikataa kujitoa kwenye umoja wa ulaya bila makubaliano. Hata hivyo amesema njia pekee ya kuepukana na kujitoa bila makubaliano ni kupitia fikra chanya za walio wengi. Barnier ameeleza kuwa mjadala wa mpango wa kujitoa unapaswa kuendelea kufanywa kuwa mjadala wa wazi kwa watu. Kwa mujibu wa Barnier kwakuwa hapakuwa na  mtizamo chanya wa walio wengi juu Uingereza kujiondoa kabla ya machi 29, Kifungu cha 50 kimeongezwa muda hadi tarehe 12 ya mwezi Aprili.

Atoa ushauri iwapo May atakwama tena

Barnier ameonya kwamba kama Waziri mkuu May atashindwa kupitisha mpango wake kwa Bunge, basi Uingereza itasalia na njia mbili pekee, kuondoka bila makubaliano ama ama kuomba upya kuongezewa muda kupitia kifungu cha 50 na kwamba hatua hiyo itapaswa kufanyika kabla ya Uingereza kujiondoa Umoja wa ulaya kabla ya ama ifikapo Aprili 12.

Großbritannien London - Debatte zum Brexit
Bunge la Uingereza katika moja ya mijadala ya BrexitPicha: picture-alliance/dpa/PA Wire/House of Commons

Bunge la Uingereza limekuwa likikataa mara kadhaa mipango mbadala ya ule wa Waziri Mkuu Theresa May wa kujiondoa kwenye umoja wa ulaya likiwa limekwisha piga kura mara tatu bila matokeo yenye mafanikio. Matokeo ya mpango huo kugonga mwamba kwenye baraza la wawakilishi yameiweka serikali May katika wakati mgumu.

 Hata hivyo Bi May, ambaye anajulikana kwa nia yake thabiti huenda akajaribu kurudisha tena mpango wake wa makubaliano ya kujitoa Umoja wa ulaya kwa mara nyingine baadaye wiki hii. Kujitoa kwa Uingereza katika Umoja wa ulaya bila makubaliano, kutaathiri biashara na safari katika  vituo vya ukaguzi na maeneo ya mipaka pamoja na kanuni mpya kati ya Uingereza na nchi 27 za Umoja wa ulaya.

Mwandishi: Angela Mdungu/RTRE/APE

Mhariri:Sekione Kitojo