1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo: Haile Gebreselassie astaafu

8 Novemba 2010

Ligi Kuu za Ulaya, ziliendelea mwishoni mwa wiki, huku mfalme wa mbio za mita 10,000 na 5,000 Muethiopia Haile Gebresallesie akistaafu.

https://p.dw.com/p/Q1ld
Haile Gebreselassie astaafuPicha: Alexander Göbel

Borussia Dortmund wanaendelea kutamba katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, huku chipukizi Mainz wakianza kusuasua baada ya kuanza msimu kwa kishindo. Huku Uingereza Liverpool wamefufua matumaini yao ya kusalia katika Ligi ya Premia na nchini Spain, Real Madrid wasalia kileleni baada ya kushinda " Madrid derby".

Tukianza na ligi ya Ujerumani Bundesliga, Ushindi dhidi ya Hanover ndio waliouhitaji kusalia kileleni mwa ligi kwa wiki nyingine ya pili na timu changa ya Borussia Dortmund haikuvunja moyo hawakuwa na huruma na Hanover walipowachapa mabao 4 bila ya jibu.

Fußball Bundesliga Hannover 96 gegen Borussia Dortmund Flash-Galerie
Borussia Dortmund wako kileleni mwa Bundesliga.Picha: dapd

Na kwa kuwa chipukizi Mainz ambao walikuwa wanawahemea Dortmund mgongoni walishindwa Jumamosi na Freiburg- Dortmund sasa wanatamba kileleni mwa ligi wakiwaacha Mainz kwa pointi nne, na wako mbele kwa pointi saba dhidi ya timu inayoshikilia nafasi ya tatu Bayer Leverkusen.

" tulistahili kushinda."  ndio ilikuwa jibu la Jurgen Klop kocha wa Dortmund.

Wachambuzi wa Bundesliga wanasema Dortmund inazidi kudhihirisha kuwa wako tayari kunyakua ubingwa msimu huu.

Stuttgart walijinyanyua kutoka meno ya kushushwa daraja walipowakomea Werder Bremen mabo 6-0. Bayer Leverkusen nao walizinduka walipokuwa nyuma kwa bao moja dhidi ya Kaiserslautern na kuwashinda 3-1.

Jumamosi mlinzi wa  Bayern Munich Philip Lahm aliokoa jahazi la mabingwa hao wa Ujerumani aliposawazisha bao lao la tatu na kugawana pointi na Borussia Moenchengladbach.

Real Madrid vs. Inter Mailand FLASH-Galerie
Real Madrid wanaongoza Spain.Picha: AP

Mainz ambao walikuwa wamefanya mapinduzi msimu huu katika Bundesliga- wameanza kuteleza na Freiburg haikuwa na huruma nao Jumamosi ilipowafunga bao 1 bila ya jibu. Eintracht Frankfurt wamejinyanua hadi nafasi ya nne katika ligi baada ya ushindi wao wa 3-1 dhidi ya mabingwa wa zamani Wolfsburg. Hoffeinheim wako katika nafasi ya tatu, Hamburg ni ya sita pamoja na Nuremberg waliowashinda Cologne 3-1

Barani Afrika Mfalme wa mbio za masafa marefu  Haile Gebrassellasie kutoka Ethiopia  aweka mabuti chini na kuamua kustaafu baada ya kutawala mbio za masafa marefu za mita elfu 10 kwa muda mrefu.

Gabresellasie ambaye anafahamika kama Emperor nchini Ethiopia aliingia katika uwanja wa riadha kwa kishindo aliposhinda mataji manne mfulilizo katika mbio za mita 10,000 mwaka wa 93 mjini Stuttgart hapa Ujerumani. Katika michezo ya Olimpiki huko Atlanta 1996 na Sydney 2000 Gebreselassie alishinda medali za dhahabu. Alikuwa ndio bingwa wa dunia katika  10,000 na 5,000 na kuachana na mbio hizo kirasmi mwaka wa 2003 alipojinyakulia medali ya shaba. Alianza kushiriki katika nbio za marathon 2002 na kunyakua taji la dunia 2007 mjini Berlin.

Ingawa alikata utepe kwa kishindo kwa zaiid ya miongo miwili- Mfalme wa mbio za mita elfu 10 aliondoka uwanjani jana mjini New York katika mbio za marathon huku akiwa amevunjika moyo. alijiondoka katika mbio baada ya kupata matatizo, na ndipo alipotangaza wakati umewadia kusema tosha.

Edison Pena Chile Grubenunglück Marathon New York Flash-Galerie
Mbio za marathon mjini New York jana.Picha: AP

Nchini Uingereza Fernando Torres ndie alikuwa mwiba wa Chelsea pale Liverpool ilipowashangaza mabingwa hao kwa mabao 2-1. Uhsindi huu wa vijana wa Roy Hodgson ukawanyanyua kutoka katika hatari ya kushushwa daraja. Hii ndio mara ya pili Chelsea walio kileleni mwa premia ligi wameshindwa msimu huu.

Hamu ya Arsenal kutetea taji la Premi ilipata pigo jana waliposhindwa kwa bao 1 bila jibu na Newcastle. Ilhali Manchester United sasa wanawahemea Chelsea mgongoni baada ya kushinda mechi yao dhidi ya Wolverhampton. Chelsea wana pointi 25, mbili mbele ya Manchester United, huku Arsenal na Manchester City wakishika nafasi ya tatu kwa pointi 20.

Nchini Spain Real Madrid wamesalia kuiongoza La liga- baada ya kuwashinda majirani zao Atletico Madrid 2-0 hapo jana. Awali mahasimu wao Barcelona waliongoza ligi kwa muda mfupi walipowanyamazisha Getafe ugenini 3-1.

Villareal ambao waliwashinda Atletico Bilbao licha ya kuwa Bilbao ndio walikuwa wa kwanza kuona lango, wanashika nafasi ya tatu, Ilhali Espanyol wako katika nafasi ya nne baada ya kuwashinda Malaga 1-0.

Mwandishi: Munirra Muhammad/RTRE: AFP

Mhariri: Josephat Charo.