1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa wiki

29 Mei 2009

Finali ya Kombe la DFB Berlin na FA London leo:

https://p.dw.com/p/HzyK
Majogoo wa B.LeverkusenPicha: AP

Baada ya msimu wa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani kumalizika mwishoni mwa wiki iliopita na kutawazwa Wolfsburg, mabingwa wapya na FC Barcelona kuichezesha Manchester United kindumbwe-ndumbwe na kutwaa taji la Champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya, leo jioni kuna finali 2 za kusisimua:

Wakati katika Uwanja wa Olimpik wa Berlin ni finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani kati ya Werder Bremen na Bayer Leverkuesen, mjini London ni finali ya Kombe la FA kati ya Chelsea na Everton. Imetangazwa pia kura ya mapambano ya Kombe la Afrika la mataifa ,Januari 10-31 mwakani nchini Angola, itapigwa mwishoni mwa mwaka huu.

Tukianza na finali ya Kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani jioni hii katika uwanja wa Olimpik wa Berlin, Werder Bremen ina nafasi ya mwisho ya kufuta machozi na kuondoka angalao na taji moja baada ya kutofanya vyema katika Bundesliga na kupokonywa Kombe la UEFA na Shakhtar Donetsk ya Ukraine wiki mbili zilizopita.

Katika mpambano wa mwisho wa msimu wa Bundesliga kati yake na mabingwa Wolfsburg Jumamosi iliopita, Bremen ilikandikwa mabao 5-1. Mpambano wa leo utakuwa pia wa mwisho kwa jogoo lao la Brazil, Diego ambae msimu ujao anahamia Juventus nchini Itali. Ushindi leo dhidi ya Leverkusen utawafuta machozi Wabremen kwa misukosuko mingi waliopata msimu huu.

Leverkusen imekuwa pia na misukosuko yake na kabla ya finali ya leo (Jumamosi) kulizagaa uvumi kwamba, wachezaji wakipanga kuasi dhidi ya kocha wao Bruno Labadia. Meneja wa Bayer Leverkusen, Rudi Voller-mshambulizi hatari wa zamani wa timu ya Taifa na hata Bremen yenyewe, anakanusha hakuna njama ya uasi. Ikiwa kuna uasi wowote itakuwa basi dhidi ya Bremen, kwani Leverkusen pia inalihitaji Kombe hili kufuta madhambi ya msimu uliokwenda kombo.

Ama katika finali ya leo (Jumamosi)ya Kombe la FA huko Uingereza kati ya Chelsea na Everton. Kama katika finali ya Berlin kati ya Bremen na Leverkusen, Chelsea na Everton kila moja ina sababu ya kiu kikubwa cha ushindi leo.

Chelsea inataka kumuaga kwa ufanisi kocha wao wa muda mdachi Guus Hiddink na pia kufuta machozi kwa kupigwa kumbo dakika ya mwisho nje ya finali ya Champions League na FC Barcelona ya Spain, mabingwa wapya wa Ulaya waliowavua taji juzi Manchester United.Chelsea walisahau pigo walilopewa na Barcelona na kutamba kwa mabao 4-1 mbele ya Arsenal, lakini Everton ni timu nyengine kabisa. Everton yataka leo kutumia nafasi hii kunawirisha msimu wa ufanisi kwao kwa kutwaa kombe.

Mkondo uliopita Everton kuingia finali ya leo unaonesha wanaweza kuzima vishindo vyoyote. Kwani, waliiangusha Liverpool, Aston Villa, Middlesbrough na hata mabingwa Manchester United ingawa katika changamoto ya mikwaju ya penalti.

Mjini Cairo,imetangazwa kwamba kura ya kuamua vipi timu zilizofuzu kwa Kombe lijalo la Afrika la Mataifa nchini Angola, litakalotangulia Kombe la dunia Afrika Kusini, itapigwa Novemba 30 mjini Luanda-hii ni kwa muujibu wa CAF-shirikisho la dimba la Afrika. Kura hiyo itapigwa wiki chache tu kabla dimba lenyewe kufunguliwa hapo Januari 10 hadi 31 atakapotawazwa bingwa mpya au wa zamani Misri.

Misri, pamoja na wenyeji wa Kombe lijalo la dunia-Bafana Bafana-Afrika Kusini, zinajinoa wakati huu kwa Kombe la Mashirikisho linaloanza Afrika Kusini wiki 2 hivi kutoka sasa-Juni 14-28. Miongoni mwa mabingwa wengine watakaoania Kombe hilo ni Brazil, mabingwa wa Ulaya Spain na mabingwa wa Asia, Iraq.

Muandishi: Ramadhan Ali /RTRE

Mhariri: Josephat Charo