1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo mwishoni mwa wiki

13 Novemba 2009

Kinyanganyiro cha mwisho cha tiketi za Kombe la dunia 2010.

https://p.dw.com/p/KW8X
Nembo ya Kombe la dunia 2010

KOMBE LA DUNIA KANDA YA AFRIKA

Wakati timu ya Taifa ya Ujerumani, imevunja mpambano wake wa leo na Chile,mjini Cologne, wa kujiandaa kwa Kombe la dunia, 2010 nchini Afrika Kusini, kwa msiba wa kifo cha kipa wake Robert Enke, timu kadhaa za taifa kutoka kanda mbali mbali,zinaingia uwanjani leo kuania tiketi za mwisho za Kombe la dunia.Mpambano wa kufa-kupona kanda ya Afrika, ni ule kati ya mabingwa Misri na majirani zao Algeria.

Changamoto hii, imetanguliwa tayari na fujo nje ya chaki ya uwanja pale jana basi walilopanda wacheazji wa Algeria kutoka uwanja wa ndege wa Cairo, lilipohujumiwa kwa mawe na chipukizi wa Misri na wachezaji 4 kujeruhiwa. Ingawa Misri imeomba radhi,Algeria imekataa samahani hiyo.

Mabingwa wa Afrika Misri , wanajua "leo ni leo, asemae kesho muongo": Hatima ya mafiraouni kucheza Kombe la dunia mwakani nchini Afrika kusini, itategemea ushindi nyumbani Cairo dhidi ya Algeria.Algeria, yatosha tu kutoka sare na kuondoka Cairo na tiketi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu 1986 ilipocheza mara ya mwisho Kombe la dunia,huko Mexico.Algeria, inaongoza kundi hili ikiwa na pointi 13 -pointi 3 zaidi kuliko mabingwa wa Afrika,Misri.Misri, haikucheza Kombe la dunia tangu 1990 nchini Itali.

Ushindi wa mabao 2-0 wa Misri,leo utaziweka timu hizo mbili sare daraja moja,tangu kwa pointi hata kwa magoli.Ni mshindi tu wa kundi hili atakaetoroka na tiketi ya kombe la dunia .Kwahivyo, jazba kubwa tayari zipo kati ya mashabiki wa timu hizi 2.Uhasama wao ulianzia miaka 20 iliopita mjini Cairo, pale Misri, ilipoishinda Algeria bao 1:0 na kuipiga kumbo nje ya Kombe la dunia la Itali, 1990.

Algeria, leo inataka kulipiza kisasi tangu cha pigo hilo hata cha alhamisi usiku pale basi walilopanda wachezaji wa Algeria, kutoka uwanja wa ndege wa Cairo, lilipohujumiwa kwa mawe na mashabiki wa Misri .Wachezaji wao 4 walijeruhiwa na Algeria,ikatoa lalamiko rasmi kwa serikali ya Misri.Misri, iliomba msamaha,lakini Algeria iliukataa msamaha huo.Ni chini ya hali hii, mpambano wa leo wa kukata na shoka unachezwa kati ya mahasimu hao 2 wa dimba.

Morocco,iliozimwa 0:0 tena nyumbani na Togo Juni,mwaka huu, imeshindwa katika malalamiko yake iliotoa kutaka matokeo ya mechi yake na Togo yanafutwa.Mahkama ya dimba imesema imelikataa dai la Morocco la kupewa ushindi wa mabao 3:0 kutokana na kuwa Togo eti, ilimchezesha mchezaji asiestahiki kucheza.Morocco tangu mwanzo haikuwa na nafasi ya kucheza Kombe la dunia mwakani.Majirani zao Tunisia,lakini ,wana miadi leo na Msumbiji, mjini Maputo .

Tunisia, inahitaji ushindi Msumbiji ili kuizima Nigeria, yenye miadi na Harambee Stars, mjini Nairobi.Kama changamoto ya Cairo kati ya Algeria na Misri, macho ya mashabiki wa Tunisia na Nigeria, yanakodolewa Maputo na Nairobi. Tunisia inaania kucheza kwa mara ya 4 katika Kombe la dunia tangu 1978 ilipocheza Rosario,Argentina wakati NIgeria, inataka kufuta madhambi ya kupigwa kumbo na Angola, nje ya Kombe lililopita la dunia , Ujerumani, 2006.

Mapambano mengine leo ni kati ya Morocco -simba wa Atlas na simba wa nyika-Kameroun ambamo Kamerun yatumai kunguruma na kutoroka na tiketi ya kombe la dunia.Togo ina miadi na Gabon.Mjini Kigali, Rwanda inacheza na Zambia wakati Sudan, inaikaribisha nyumbani Khartoum,Benin.

Tembo wa Ivory Coast,ambao wameshakata tiketi yao ya Afrika Kusini, wanamalizana na Guinea. Burkina Faso inaikaribisha nyumbani Malawi.Kesho Jumapili,kinyan'ganyiro hiki kitakamilishwa na changamoto 1 kati ya Ghana (Black Stars) iliokuwa timu ya kwanza kanda ya Afrika kufuzu kwa Kombe la dunia na Mali,mjini Accra.

Endapo mpambano wa leo Ijumamosi, kati ya Misri na Algeria ukimalizika kwa ushindi wa Misri wa mabao 2:0 , changamoto ya kuamua nani kati yao atacheza Kombe la dunia,itachezwa Sudan.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE

Mhariri: Aboubakary Liongo