1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

7 Machi 2008

Mashindano ya ukumbini-Indoor ya riadha huko sevilla yaanza .Münich yaizaba Anderlecht 5:0 katika kombe la UEFA.

https://p.dw.com/p/DKcz
Anderlecht's Jelle Van ashindwa kuziba lango lao.Picha: AP

Mashindano ya riadha ya ukumbini ya ubingwa wa dunia –World Indoor athletics championship yanayofungua pazia kwa michezo ijayo ya Olimpik ya Beijing,China hapo August 8 mwaka huu yalifunguliwa rasmi jana mjini Sevilla,Spian.

Janeth Jepkosgei,bingwa wa dunia wa mita 800 huko Osaka,mwaka uliopita ataka kuwa msichana wa kwanza wa Kenya kutwaa medali ya dhahabu ya Olimpik mwaka huu.

Katika medani ya dimba, Pele anajiunga na kamati ya maandalio ya Brazil kwa kombe la dunia 2014.

Na Bafana Bafana-timu ya Taifa ya Afrika kusini ina miadi kwa mpambano wa kirafiki na Paraguay hapo Machi 26 mjini Pretoria.

RIADHA:

Huu ni msimu unaotangulia michezo ya olimpik ya majira ya kiangazi mjini Beijing hapo August 8 na masbhindano yote ya riadha wakati huu yanalenga kuwanoa majogoo wake kwa waume kwa mashindano hayo.Mwenzangu Alex Mwekideu anasimulia:

Kuanzia jana (ijumaa) wanariadha 600 kutoka nchi 157 walianza mtihani wao huko sevilla,Spain kupimana nguvu.Kati yao ni wale wa Kenya na Ethiopia.

Jumla ya mabingwa 20 wa dunia tangu wa mashindano ya ukumbini-indoor hata ya nje -outdoor wanapimana nguvu-wale waliotamba katika mashindano kama haya ukumbini mjini Moscow, 2006 na wale waliotoroka na medali za dhahabu mjini Osaka,Japan mwaka jana.

Bingwa wa dunia na wa Olimpik wa masafa marefu wakike wa Ethiopia Meseret Defar anatetea taji lake la mita 3000.

Macho lakini yatakodolewa Maria Mutola wa Msumbiji ,anaeania katika mashindano haya medali yake ya 8 ya dhahabu katika masafa ya mita 800.Mutola lakini ana umri wa miaka 35 na anaelewa kibarua ni kigumu.Alikwisha onjeshwa shubiri na mkenya Janeth Jepkoskei mwaka jana katika ubingwa wa dunia huko Osaka, japan.Na Janeth amepania kuwa mwanariadha wa kwanza wa kike wa Kenya kutawazwa bingwa wa olimpik.

Kwani, tangu Janeth kuwa mwanamke wa kwanza wa Kenya kushinda taji la ubingwa wa dunia,alipompiga kumbo Maria Mutola mwaka jana, mashabiki nchini Kenya, wamekuwa wakitazamia kuwa huu utakua mwaka wa wasichana wa Kenya huko Beijing.

Janeth alinukuliwa kusema, “Nilipokwenda Osaka, sijajikuta katika shinikizo kubwa la kubidi kushinda kama mara hii na kwahivyo, mambo yalikuwa rahisi zaidi.sasa kila mmoja ananitazamia kushinda taji la Olimpik.”

Kujiandaa kwa mazowezi hakujakuwa rahisi hivi karibuni nchini Kenya kutokana na hali ya machafuko ya kisiasa yaliofuatia uchaguzi wa kutatanisha wa mwaka jana.

Nyumbani kwa Jeneth huko Rift Valley ,kulikua shina la ghasia hizo na baadhi ya kambi za mazowezi za wanariadha zilibidi kufungwa wakati nyengine zilizingatia kuhamia sehemu nyengine ya Kenya.Wanariadha 2 wa Kenya waliuwawa katika machafuko hayo-nao ni Lucas Sang huko Eldoret na mwenda-mbio za marathon Wesley Ngetich huko Trans mara.

Eldoret, imetoa mabingwa wakubwa wa riadha duniani wa masafa ya kati na marefu.Nyumbani mwa Janeth ni kati ya nyumba walikotoka mabingwa wengine wakubwa wa Kenya wa masafa ya mita 800 kama Wilson kipketer,aliebadili uraia na kukimbia chini ya bendera ya Denmark na bingwa wa sasa Wlfred Bungei.Janeth anawahusudu sana mabingwa hao na ndio iliomtia ari kukimbia pia masafa hayo na kuwa bingwa.Lakini ikiwa kuna mwanariadha yeyote aliemlea na kumnoa makali basi ni yule bingwa wa olimpik wa mita 800 huko Seoul, 1988 Paul Ereng.Na Ereng ni mmoja kati ya wanariadha wa zamani anaeamini kwamba Janeth Jepkosgei atawika huko Beijing,August hii na kurudi Eldoret na medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpik kwa msichana wa Kenya.

Wasichana wa Kenya wamenyakua medali 3 za fedha za olimpik na I ya shaba .Medali zote hizo zimetoka katika masafa ya mita 5000 na marathon.

Kwa mara ya kwanza, Kenya iliteremsha wanariadha wake wa kike katika medani ya Olimpik huko Mexico City, 1968-miaka 40 iliopita na wakati ule hakuna hata mmoja alievuka duru ya kwanza.Kinyume na sura ilivyo hii leo.Wasichana wa Kenya kama wenzao wa Ethiopia wamepiga hatua kubwa na ikiwa kila kitu kitakwenda sawa sawa ,bingwa wa dunia wa Osaka,japan, Janeth Jepkosgei, atazamiwa kuiletea Kenya,medali yake ya kwanza ya dhahabu ya wasichana kutoka Beijing,August mwaka huu.

DIMBA:

Wenyeji wa kombe la dunia 2010-Afrika kusini wakijiandaa kwa kombe hilo wana miadi na Paraguay-timu ya taifa kutoka Amerika kusini hapo Machi 26.Mpambano huo utachezwa katika Super Stadium huko Atteridgeville.Huo utakua mpambano wa kwanza wa bafana bafana tangu ilipopigwa kumbo nje ya Kombe la afrika la mataifa nchini Ghana hapo Januari.Timu hizi mbili-Afrika Kusini na Paraguay,zilitoka sare mabao 2-2 katika kombe la dunia 2002 huko Korea ya Kusini na huo ulikua mpambano wao wa kwanza kabisa.

Baada ya kuchezwa Afrika Kusini, likiwa kombe la kwanza kabisa kuaniwa barani Afrika, itakua zamu ya Amerika kusini kuandaa kombe la 2014.Kura imeiangukia Brazil.Pale Brazil ilipotunikiwa nafasi hiyo,Pele hakuwapo katika sherehe hiyo mwaka jana .Sasa lakini asema mfalme Pele anajiunga na Kamati ya maandalio ya kombe la dunia huko kwao Brazil kutoa mchango wake kimaandalio baada ya kuutoa uwanjani akiwa mchezaji. Pele aliichezea Brazil katika kombe la dunia kwa mara ya kwanza 1958 akiwa chipukizi wa miaka 17 huko Sweden.Halafu akacheza tena kom,be la dunia la 1962 huko Chile ,lakini aliumia na mapema kabla ya finali.

Pele,akateremka kwa mara ya tatu katika kombe la dunia la 1966 huko Uingereza.Lakini, lilikuwa kombe la mwanamsumbiji Eusdebio kutamba na sio la Pele.Miaka 4 baadae,nyota ya Pele ilinawiri kwa mara ya mwisho katika mawingu ya kombe la dunia huko Mexico pale yeye na Revelino walipoiongoza Brazil kutwaa Kombe la dunia kwa mara ya 3 mjini Mexico.

Sasa Pele anasema na ninamnukulu,

„nataka kuwa sehemu ya Kombe la dunia litakaloitukuza Brazil.“

Pele akasema kwamba anaamini anaweza kuchangia sana kufanikisha kombe la dunia nchini Brazil.

Kwanini Pele hakuhudhuria sherehe ya kuchaguliwa Brazil kuandaa kombe la dunia nyumbani 2014 hapo Oktoba mwaka jana .Rais wa shirikisho la dimba la Brazil ( CBF ) Teixeira ameshika wadhifa huo tangu 1989 na mara ya kwanza kuibuka hadharani kuwa ana tofauti na Pele, ilikua 1993.Hii na pale FIFA ilipomuweka kando Pele asishiriki katika kura ya kombe la dunia la 1994 nchini Marekani iliofanyika huko Las Vegas.

Hii ilifuatia hujuma kali ya Pele kwa Teixeira ambae bamkwe wake ni rais wa wakati ule wa FIFA Joao Havelange pia kutoka Brazil.Miaka 6 iliopita,Pele alitangaza kwamba amani kati yake na Teixera imerudi.Hatahivyo, watu 2 hao hawakuwahi kukaribiana.Pele atakaekuwa na umri wa miaka 73 hapo 2014 kombe litakapoaniwa Brazil,yamkini akapewa wadhifa wa balozi katika kamati hiyo ya maandalio na pengine akazitembelea nchi zote 31 zitakazokwenda Brazil kwa dimba hilo.

Kesho,Arsenal london ina kila uwezekano wa kupanua mwanya wake katika premier League hadi pointi 4 mradi tu itandike Wigan Athletics na kuondoka na pointi 3.Manchester united ilioziba mwanya na Arsenal hadi pointi 1 mwishoni mwa wiki iliopita ilikua na miadi jana kucheza kombe la FA.

Arsenal ilitamba kweli kati ya wiki hii pale ilipokuwa klabu ya kwanza ya Uingereza kuwalaza mabingwa wa Ulaya AC Milan tena uwanjani mwao San Siro.Ni chini ya ari ya ushindi huo ndipo kesho jumapili Arsenal inapambana na Wigan Athletics.

Kati ya wiki hii, viongozi wa ligi wa Ujerumani Bayern Munich walitamba nao katika kinyan’ganyiro cha kombe la ulaya la UEFA.Munich imeshatia mguu mmoja katika robo-finali ya kombe hilo baada ya kuirarua Anderlecht ya Ubelgiji kwa mabao 5-0.Munich ilifungua mlango wa Anderlecht tayari katika dakika ya 9 ya mchezo pale Hamit Altintop alipoutikisa wavu kwa mkwaju wake maridadi ajabu kutoka masafa ya mita 60. Bao la mwisho la Munich lilipachikwa na mfaransa Franck Ribbery kwa mkwaju wake wa freekick kutoka masafa ya mita 20.