1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michezo wiki hii

4 Septemba 2009

Ujerumani na Afrika kusini leo

https://p.dw.com/p/JSOv
Logo WM 2010 Süd Afrika

-Kinyanganyiro cha kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini kinaendelea jioni hii katika kanda mbali mbali-ulaya,Amerika kusini,Asia na Afrika:

Wenyeji wa kombe hilo Bafana-Bafana-au Afrika kusini, wanapimana nguvu jioni hii na Ujerumani mjini Leverkusen -Je, vuvuzela ni ruhsa uwanjani ?

Katika kanda ya Afrika-Simba wa nyika Kamerun wana miadi leo na Gabon,mabingwa wa Afrika Misri waimeitembelea Rwanda.

-Kundi B: Harambee Stars-Kenya wako kwa machinga-Msumbiji-macho lakini yakikodolewa mpambano wa kundi hili baina ya Nigeria na Tunisia-nani atatoroka hapo na tiketi ya kombe la dunia ?

-DFB-shirikisho la dimba la Ujerumani lapanga kuichukulia FIFA hatua ya kisheria ikiwa litashikilia wachezaji waruhusiwe na klabu zao kushiriki Kombe lijalo la Dunia chini ya umri wa miaka 20 mwezi huu nchini Misri.

Bafana Bafana au Afrika Kusini, ikijianda nayo kwa Kombe la dunia inateremka uwanjani jioni hii mjini Leverkusen,katika kitongoji cha Cologne kwa changamoto na makamo bingwa wa Ulaya-Ujerumani.Ujerumani ina miadi ya kukata tiketi yake ya kombe hilo la dunia na Azerbaijan jumatano hii ijayo kabla mpambano wake wa kukata na shoka na Urusi hapo Oktoba.

Kikosi cha Ujerumani kinaregarega na mwaka kabla Kombe hilo la dunia, kocha Joachim Loew yumo bado kupanga na kupangua.Hana wachezaji wengi wenye maarifa kama vile nahodha Michael Ballack.

Jioni hii Ballack anavaa jazi ya Ujerumani kwa mara ya 94 na ndio nyota pekee wa dunia katika kikosi cha Ujerumani. Mwengine mwenye maarifa kiasi, ni mlinzi wa Bayern Munich ,Philipp Lahm na mshambulizi Bastian Schweinsteiger. Iwapo stadi wa FC Cologne alieihama Bayern Munich-Lukas Podolski ni fit kucheza leo, haijulikani. Matumaini yanawekwa kwa mshambulizi wa Stuttgart wa asili ya Brazil ,Cacau lakini pia Miroslav Klose na Mario Gomes wote wa Bayern Munich.Hata langoni,kocha Loew, amekuwa akifanya majaribio mengi tangu kustaafu Oliver Kahn. Nani alinde lango -Robert Enke -kipa wa hannover 96 au Rene Adler wa Bayer-Leverkusen ?

Kwavile, mpambano wa jioni hii unachezwa Leverkusen,uamuzi haukuwa taabu kwa kocha Loew: Rene Adler atalinda lango lake nyumbani.Waafrika Kusini nao pia wamekuwa wakipepesuka na wameshindwa hata kukata tiketi ya Kombe lijalo la Afrika la mataifa mapema mwakani nchi jirani ya Angola. Katika Kombe la dunia wameingia bila kupingwa kama wenyeji.

Hii si mara ya kwanza kwa Ujerumani kukutana na Bafana Bafana.Walikwishcheza pamoja huko Afrika Kusini .Mara hii Bafana bafana inatembelea Ujerumani.Mpambano wa leo utatoa ishara kwa Ujerumani iwapo ni tayari kwa zahama ya jumatano na Azerbaijan ambayo Ujerumani haidiriki kushindwa.kwani, inahitaji pointi zote 3 kabla mpambano wake wa Oktoba wa kufa-kupona na Urusi.

Katika kanda ya Afrika, macho yanakodolewa mpambano wa kundi B kati ya Super Eagles -Nigeria mjini Abuja na Tunisia. Tunisia ilicheza katika Kombe lililopita la dunia 2006 hapa Ujerumani na inataka pia kwenda Afrika Kusini.Nigeria, ilitolewa na Angola na haikuja Ujerumani katika Kombe la dunia. Mara hii, Nigeria, inataka kufuta madhambi hayo.Inaelewa lakini kwamba njia ya kwenda Afrika Kusini 2010 inapitia Tunisia.Kwa jicho hili, nisingependa kuagua matokeo ya changamoto hii.Jambo moja ni dhahiri:Utakuwa mbele ya mashabikiw a nyumbani mpambano wa kufa-kupona kwa Super eagles.

Kenya Harambee Stars, hawana tena matarajio ya kwenda Afrika kusini,lakini hawatopenda kuvunjiwa heshima na Msumbiji mjini Maputo.Katika kundi C Algeria inajaribu kukwepa risasi za Chipolopolo-Zambia nyumbani.

Katika Kundi D:Black Stars-(nyota nyeusi) - Ghana inakusudia kunawiri tena katika mawingu ya Accra jioni hii wakichuana na Sudan.Benin inacheza na mali katika kundi hili. Simba wa nyika -Kamerun wako Gabon wakati mabingwa wa Afrika Misri, wamewasili mjini Kigali,Ruanda.Tembo wa Ivory Coast wanatamba nyumbani wakijaribu kuwakanyaga Burkina Faso.Malawi imeikaribisha Guinea.

Shirikisho linaloongoza Ligi Ujeruman- DFL litazingatia kulichukulia hatua ya kisheria, shirikisho la dimba la dunia-FIFA, ikiwa FIFA itashikilia kuwa klabu za Ujerumani ziwaruhusu wachezaji wao kwenda Misri, kwa Kombe lijalo la dunia la chipukizi chini ya umri wa miaka 20.Kombe hilo litaanza kuaniwa hapo Septemba 25 na kuendelea hadi Oktoba 14 wakati ambao Bundesliga imeuma.

Katika mahojiano rais wa FIFA Sepp Blatter, wiki hii aliomba pwepo umoja na mshikamano kwa njia ya kuwa klabu hizo zinawaruhusu wachezaji wao kushiriki katika Kombe hilo la dunia na akaarifu atalipeleka swali hilo mbele ya Halmashauri Kuu-tendaji ya FIFA.Halmashauri hiyo inatazamiwa kukutana mjini Rio de Janeiro,Brazi,l Septemba 29-30.

Katika taarifa nyengine, rais wa shirikisho la kabumbu la ujerumani Theo zwanziger alizima uvumi kuwa kocha wa zamani wa Timu ya taifa ya ujerumani katika Kombe la dunia, Jürgen Klinsmann atarejea katika timu ya Taifa. Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti hapo awali, kwamba yamkini kwa Klinsmann alieiongoza ujerumani pamoja na kocha wa sasa katika Kombe lililopita la dunia akarejea kama mshauri wa kocha Loew wakati wa finali ya Kombe la dunia nchini Afrika Kusini 2010.Ingawa alisema zwanziger anamthamini Klinsmann na mawazo yake,lakini hadhani kuwa kocha wa sasa wa taifa anahitaji mshauri.

Hapo kabla meneja wa timu ya taifa Oliver Bierhoff alithibitisha katika gazeti la BILD kuwa shirikisho la dimba la Ujerumani -DFB-lina mawasiliano mazuri na Klinsmann alietimuliwa na bayern munich hapo April mwaka huu kama kocha.

Chelsea,imethibitisha wiki hii kuwa itakata rufaa kupinga marufuku iliopigwa na FIFA ya kutoajiri mchezaji yeyote mpya hadi 2011 kwa madhambi ya kumshawishi chipukizi wa Ufaransa -Kakuta kuachana na klabu yake ya RC Lens ili kuichezea Chelsea.

Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 alijiunga na Chelsea ya Ufaransa miaka 2 iliopita na hii ikapelekea Lens kupeleka mashtaka kwa FIFA. FIFA ikaamua kuwa Chelsea iliwasiliana na Kakuta kwa njia isiofaa.Mbali na marufuku ya kuajiri wachezaji wapya kwa kipindi hadi 2011, Chelsea inapaswa kulipa RC Lens faini ya Euro 130.000.

Muandishi:Ramadhan Ali/AFPE

Uhariri: Othman,Miraji