1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MICHEZO WIKI HII

12 Februari 2010

Nani ataparamia kileleni leo:Munich au Leverkusen ?

https://p.dw.com/p/Lzy2
Assimiou Toure (stadi wa B.Leverkusen)Picha: AP

Michezo ya 20 ya Olimpik ya majira ya baridi, imefunguliwa rasmi jana usiku mjini Vancouver,Kanada na kinyan'ganyiro cha medali za dhahabu,fedha na shaba, kimeanza.Nani atampiku mwenzake leo katika Bundesliga-Ligi ya Ujerumani-Bayer Leverkusen na Bayern Munich zikiwa pointi sawa kileleni ?

Na mfalme wa dimba Pele wa Brazil na wa Ujerumani, Franz Beckenbauer, wanadai kuwa, timu za Afrika, zitatamba katika Kombe la dunia mwaka huu.

BUNDESLIGA NA PREMIER LEAGUE:

Bayer Leverkusen, ingawa inaongoza kwa magoli,iko pointi sawa na Bayern Munich,mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani.Leverkusen lakini, haikushindwa hata mara 1 tangu kuanza msimu.Mahasimu wao jioni hii,ni mabingwa VFL Wolfsburg.

Munich inacheza nyumbani na Borussia Dortmund na ikitamba wakati huu haitaziachia pointi 3 kuiponyoka. Schalke, iliopo nafasi ya 3 katika ngazi ya Ligi,inapambana kesho (Jumapili) na FC Cologne.Hertha Berlin,inayoburura mkia wa Ligi, inacheza na Mainz wakati Bochum wanaumana na Hoffenheim.Stuttgart wanacheza leo na Hamburg. Freiburg, inakutana na Frankfurt.Duru hii ilifunguliwa rasmi Ijumaa jioni kwa mpambano kati ya Borussia Moenchengladbach na Nuremberg.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Arsenal eti bado inaweza kutoroka na taji,mradi tu, inashinda mapambano yake 12 yajayo-adai mshambulizi wao kutoka Urusi, Arshavin.Arsenal iko pointi 6 kutoka Chelsea . Manchester United iko nyuma pointi 1 kutoka Chelsea.

KOMBE LA DUNIA 2010

Kombe lijalo la dunia nchini Afrika kusini, litakaloanza Juni 11 hadi finali Julai 11,mwaka huu. Kwa muujibu wa wafalme wa dimba Pele na Beckenbauer, huenda ikawa siku ya kutawazwa timu ya Afrika mabingwa wa dunia.

Pele,bingwa wa dunia 1958 nchini Sweden,1962 nchini Chile na 1970 huko Mexico,aliwahi kubashiri kwamba, Kombe la Dunia la FIFA litakwenda Afrika kabla ya 2000.Ndoto yake hiyo haikutimilia,kwani, umbali kabisa timu 2 za Afrika zimefika, ni robo-finali:Kameroun ikicheza na mzee Roger Milla, ilikaribia kuitoa nje Uingereza na kuingia nusu-finali.Halafu Senegal,ikicheza mara ya kwanza katika Kombe hilo huko Korea ya Kusini na Japan, 2002 ilizimwa na Utuiruki kuwasili nusu-finali.

Pele amenukuliwa kusema, "ni vigumu kusema nini kitatokea mwaka huu,lakini pengine, tutajionea maajabu." Aliuambia mtandao wa FIFA.Pele aliongeza kusema kwamba, timu za Afrika zimeangukia makundi magumu,lakini endapo zitafuzu kuingia duru ya pili ya kutoana,bila shaka kutazuka msangao.

Mfalme wa dimba wa Ujerumani,Franz Beckenbauer, alieiongoza Ujerumani akiwa nahodha 1974 na kocha 1990, kutwaa kombe la dunia,ameungamkono aliyosema Pele kuhusu nafasi za timu za Afrika mwaka huu .

Beckenbauer, amesema kuwa, ana yakini kuwa timu moja ya kiafrika itawasili nusu-finali.Beckenbauer, akaongeza kusema kwamba, Ghana, ambayo imeangukia kundi moja na Ujerumani, pia ni kali kama Ivory Coast wakati Afrika kusini,wanacheza nyumbani.

Kama katika kombe lililopita la dunia hapa Ujerumani, Tembo wa Ivory Coast, wameangukia kundi gumu kabisa kuliko timu yoyote ya Afrika na itabidi kutoa changamotokali kwa Brazil,Ureno na Korea ya kaskazini ili ifuzu kwa duru ya pili ya kutoana.

Ghana, ikiwa kundi moja na Ujerumani ,Serbia na Australia pia ina kibarua wakati simba wa nyika kameroun watatoana jasho na Holland,Denmark na japan kabla kunguruma kucheza duru ya pili.

Mzee Roger Milla ,aliekosha nyoyo za mashabiki wa dimba ulimwenguni na Afrika 1990 huko Itali,amesema kwamba, kuamua tu kuchezwa Kombe la Dunia barani Afrika mwaka hu, ni ushindi pekee.Akasema ,

"Kila ninapokwenda zurich,ninamshukuru rais wa FIFA Sepp Blatter kwa kulileta Kombe la dunia barani Afrika."-alisema Rogger milla.

Wenyeji Bafana Bafana, wanakumbana na Mexico watakapofungua dimba Juni 11 .Stadi wa Mexico, Hugo Sanchez anatarajia mchezo wa kukumbukwa. Alisema amefurahishwa sana na Afrika.Stadi huyo wa zamani wa real Madrid akasema na ninamnukulu,

"Kuwa afrika Kusini inaandaa Kombe la Dunia 2010 sio tu jambo zuri kwa mpira,bali pia kwa bara zima la Afrika."

Algeria na Nigeria, ni timu nyengine mbili zilizofuzu kwa Kombe la dunia Juni mwaka huu .Algeria, ina miadi na Uingereza,Marekani na Slovenia katika Kundi C wakati Super Eagles-Nigeria,inakumbana na Ugiriki,Korea ya kusini na Argentina , chini ya kocha wao Diego Armando Maradona.Maradona alikuwa Afrika kusini hivi karibuni ambako alipokewa kwa shangwe na shamra shamra na mashabiki wa dimba.

Afrik nzima kwahivyo, inasubiri firimbi kulia Juni 11 ili kuandika historia ya dimba.Na ikiwa ndoto za Pele na Beckenbauer,zitatimilia, ulimwengu utajua kuwa simba na tembo wa Afrika wametamba katika pori lao la dimba-Afrika.

MICHEZO YA OLIMPIK VANCOUVER:

Michezo ya XX ya Olimpik ya majira ya baridi ilifunguliwa rasmi jana usiku mjini Vancouver,Kanada,ikiwa ya pili kufanyika nchini humo tangu ile ya Calgari. Kinyan'ganyiro cha medali za dhahabu,fedha na shaba nacho kimeanza leo huku wanariadha wa nchi za kaskazini mwa dunia wakitia fora zaidi kuliko wale wa Kusini mwa sayari yetu.

Zaidi ya miaka 6 tangu pale mji huu wa Vancouver, kushinda kuandaa michezo hii hapo Julai,2003,mwenge wa Olimpik, uliwasili vancouver siku 1 kabla ya ufunguzi rasmi na ukapokewa na wenyeji kwa shangwe na shamra shamra .Mvua ikinyesha na zaidi ikitabiriwa ni hali ambayo ilisababisha sherehe za jana za ufunguzi kuandaliwa ukumbini badala ya hadharani.

Kwa ufunguzi wa jana , michezo hii ya 2o itaendelea kwa wiki mbili na wenyeji Kanada wanatumai watanyakua idadi kubwa ya medali .Medali na ya kwanza kwa Kanada ikitazamiwa leo ambapo 6 zinaaniwa.

Kabla kufunguliwa michezo hii ya majira ya baridi,yalifanyika Vancouver maandamano -ukumbusho kuwa , sio kila mmoja ameikaribisha michezo hiyo .Wanadai kwamba dala bilioni 6 zilizotumika kuandaa michezo hii, zingetumiwa bora kuwaondoshea shida masikini.

Kabla ya kuanza rasmi michezo hii, ilikumbwa na mkasa wa kwanza wa madhambi ya (doping) ukimhusu mwanariadha wa kirusi wa mchezo wa hoki ya barafuni-Ice hockey, Svetlana Terenteva .Hatahivyo, Svetlana amekaripiwa tu,lakini hakutimuliwa nje ya Olimpik.

Mwanariadha wa Ghana, amekuwa akijiandaa muda mrefu huku ulaya kwa michezo hii na hata baadhi kutoka Kenya , maarufu katika michezo ya Olimpik ya majira ya joto. Iwapo Waafrika wanaweza kufua dafu katika michezo hii ya Olimpik ya majira ya baridi, tusubiri kuona.

Mwandishi:Ramadhan Ali /DPAE/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman