1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya kombe la Afrika kuanza Libreville

Sekione Kitojo
14 Januari 2017

Kombe la mataifa ya Afrika, maarufu kama Afcon, linaanza rasmi kuwaniwa na  timu 16 za bara hilo,leo Jumamosi(14.01.2017) ambapo wenyeji wa mashindano Gabon wanafungua dimba kwa kupambana na Guinea Bissau.

https://p.dw.com/p/2VncO
Gabun Stade d'Oyem Eröffnung Präsident Ondimba
Rais Omar Bongo akifungua moja ya viwanja vitakavyofanyiwa michezo ya kombe la Afrika nchini GabonPicha: Getty Images/AFP/S. Jordan

Wenyeji  wa  mashindano Gabon  wanapaswa  kujiweka  imara kiakili  wakati  watakapopambana  na  wapinzani  hao  ambao hawafahamiki  sana  katika  soka  la  Afrika  Guinea  Bissau  wakati wanawania  kuanza  vizuri  kampeni  yao  wakati fainali  za  kombe hilo  zitakapofunguliwa  rasmi  kwa  michezo  miwili leo Jumamosi(14.01.2017).

"Kuna  mbinyo  mkubwa  lakini  ni  vizuri  kwamba  tunacheza nyumbani. Tuna mkandamizo  mkubwa  wa  mawazo  na  majukumu," mlinzi  wa  Gabon Bruno Ecuele Manga  alisema  katika  mkesha  wa mchezo  wao  leo.

Gabun Libreville Stadion Stade de L'Amitie
Uwanja wa Stade de L'Amitie mjini Libreville utakaotumika katika mchezo wa ufunguzi na fainali ya kombe la Afrika 2017.Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

Kombe  la  mataifa  ya  Afrika  linaelekea  kuzowea  kufanyika  nchini Gabon , likirejea  katika  taifa  hilo  ambalo  lilikuwa  koloni  la zamani  la  Ufaransa   katika  pwani  ya  magharibi  ya  Afrika  kwa mara  ya  pili  katika  mashindano  manne  yaliyopita. Gabon  ilifanya kazi  nzuri  kuwa  wenyeji  wenza  pamoja  na  Guinea  ya  Ikweta mwaka  2012  na   mwaka  huu  inafanya  kazi  hiyo  peke  yake baada  ya  Libya  inayokumbwa  na  vita  kuamua  kujitoa  kuwa mwenyeji  wa  mashindano  hayo.

Wapinzani  hao  wa  Gabon  Guinea  Bissau  wanawania kuendeleza mafanikio  yao  waliyoyapata  katika  michezo  ya mchujo. Guinea  Bissau  ni  moja  kati  ya  nchi  masikini  sana barani  Afrika   na  matayarisho  yao  wamekumbwa  na  matatizo  ya fedha, ikiwa  ni  pamoja  na  mgomo  wa  wachezaji  wiki  iliyopita.

Fußball Qualilfikation African Cup of Nation 2017 Pierre Aubameyang
Pierre-Emerick Aubameyang tegemeo la Gabon Picha: Getty Images/AFP

Matumaini ya robo fainali

Burkina  Faso  na  Cameroon  zinapambana  katika  mchezo  wa  pili wa  kundi  A  katika  uwanja  unaoweza  kuingiza  mashabiki 40,000 wa  Stade de I'Amitie, mjini  Libreville, timu  zote  zikiwa  na matumaini  ya  kushinda  na  kujiweka  katika  nafasi  nzuri  ya kutinga  katika  nusu  fainali.

"Iwapo tutashinda  mchezo  huu tayari  tutakuwa  na  asilimia  50  ya kuingia  katika  robo  fainali,"  amesema  kocha  wa  Cameroon Hugo Broos. Michezo  ya  leo  Jumamosi  inazindua  wiki  tatu  za  heka heka  za  mapambano  ya  kuwania  kombe  la  mataifa  ya  Afrika kuamua  nani atakuwa  bingwa  mpya  wa  bara  la  Afrika  katika fainali  itakayofanyika  mjini  Libreville  hapo  Februari  5.

Ghana  imewahi  kukaribia  kupata  mafanikio  baada  ya  kuonesha mchezo  mzuri   katika  fainali  tano  za  kombe  hilo  la  Afrika  lakini imeshindwa  kulinyakua  kila  mara,  hali  inayotoa changamoto kubwa  na  pia  motisha  kwa  kikosi  hicho  cha  Black Stars  wakati wakiwania  tena  kulinyakua  kombe  hilo  mara  hii.

Afrika 2015 Africa Cup of Nations (Andre Ayew)
Nahodha wa Ghana Andre Ayew akilia baada ya kushindwa katika fainali dhidi ya Cote d'Ivoire 2015Picha: picture-alliance/dpa/G. Barker

Tembo wa  Cote d'Ivoire

Kikosi  kipya  cha Tembo  wa  Cote d'Ivoire  kinajitayarisha  kutetea ubingwa  wao  wa  kombe  la  Afrika , wakichochewa  na  matokeo mazuri  na  kiwango  cha  juu  cha  timu  yao  kutoka  kwa  mchezaji mpya  Wilfried Zaha.

Mshambuliaji  huyo  wa  timu  ya  Crystal Palace  anamatumaini  ya kuweka  alama  yake  katika  mashindano  hayo  ambayo yanajumuisha  wachezaji  kadhaa  wanaocheza  soka  katika mataifa  ya  Ulaya  kama  Riyad Mahhrez  wa  Algeria , Pierre -Emerick Aubameyang  wa  Gabon  na  Sadio  Mane  wa  Senegal.

Elfenbeinküste Fußball Nationalmannschaft
Mabingwa watetezi Tembo wa Cote d'IvoirePicha: I. Sanogo/AFP/Getty Images

Zaha  ni mchezaji  muhimu  aliyeongezwa   katika  kikosi  hicho  kwa kuwa  nyota  wengi  wa  zamani  kama  ndugu wawili  Toure , Kolo na  yaya  wamejiuzulu  na  mshambuliaji  nyota  wa  pembeni Gervinho  ni  majeruhi.

Zaha  aliyezaliwa  mjini  Abidjan  ameshawishiwa  kushiriki  katika kombe  la  mataifa  ya  Afrika  na  uwezekano  wa  mafanikio  katika kombe  hilo  na  kombe  la  dunia baada  ya  kushiriki  katika michezo  miwili  ya  kirafiki  katika  timu  ya  nchi  anakoishi  hivi sasa  England.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Zainab Aziz