1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika ya CHAN yaendelea

Sekione Kitojo
22 Januari 2018

Michuano ya  kombe  la mataifa  ya  Afrika  la  CHAN yaendelea Morocco, wakati  wenyeji  waongoza kundi A

https://p.dw.com/p/2rJnr
Afrikanische Nationenmeisterschaft 2018 Nigeria - Ruanda
Picha: Iimago/Xinhua/S. Aissa

Mashindano  ya  kombe  la  mataifa ya  Afrika  kwa  wachezaji  wanaocheza  ligi  za  ndani yanaendelea , ambapo  wenyeji Morocco  waliambulia  sare  ya bila  kufungana  na  Sudan  na  kujiweka  kileleni  mwa  kundi A la mashindano  hayo.

Guinea , ambayo  iliachana  na  kocha  wake Kanfory Lappe Banguora  baada  ya  kuondolewa  kutoka  katika  kinyang'anyiro hicho  Jumatano  iliyopita, ilichukua  nafasi  ya  tatu  baada  ya ushindi  wa  bao 1-0 dhidi  ya  Mauritania  katika  mchezo uliochezwa  mjini  Marrakech.

kocha  wa  Morocco  Jamal Sellami alifanya  mabadiliko  ya wachezaji  10  katika  kikosi  chake  kilichopambana  na  Guinea siku  nne  zilizopita, ambapo mshambuliaji  mwenye  mabao matano Ayoub el Kaabi  akiwa  miongoni  mwa  wale waliopumzishwa.

Morocco wenyeji  wa  mashindano  hayo watapambana  na  timu ya  pili  katika  kundi  B, huenda Namibia , Jumamosi  ijayo  muda mfupi  kabla  ya  Sudan  kuoneshana  kazi  na  mshindi  wa  kundi B , ambao huenda  ni  Zambia mjini  Marrakech. Namibia  na Zambia  zimefanikiwa  kufuzu  kutoka  kundi B baada  ya  ushindi mara  mbili  kila  mmoja  na zinakutana  mjini  Casablanca  leo Jumatatu kuamua  ni  timu  gani  inashika  nafasi  ya  kwanza.

Nae kocha  mkuu  wa  timu  ya  taifa  ya  Misri  Hector Cuper anatarajiwa  kuiacha  timu  hiyo baad  ya  kombe  la  dunia mwaka  huu. Meneja wa  timu  ya  taifa  ya  Misri Eihab Laheita amesema  kocha  huyo  raia  wa  Argentina amepokea maombi kadhaa  ya  kazi, lakini amekataa  kuzitaja  timu zinazomtaka.

Tangu  alipochukua uongozi wa  timu  hiyo mwaka  2015 , Cuper aliiongoza  Misri hadi kufuzu  kucheza  katika  fainali za  kombe la  dunia  nchini  Urusi, kwa mara  ya  kwanza  tangu mwaka 1990. Mwaka  jana  aliifikisha  timu  hiyo  katika  fainali za kombe  la  mataifa  ya  Afrika AFCON baada  ya  mabingwa  hao mara  saba  kushindwa  kufuzu kucheza  katika  fainali  hizo tangu mwaka  2010. Kabla  ya  kuchukua  kazi  ya  kuifunza  Misri , Cuper mwenye umri  wa  miaka  62 alifundisha klabu  mbali mbali , hususan nchini  Italia na Uhispania.

 

Mwandishi :  Sekione  Kitojo / ape / rtre / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga