1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya Ligi kuu Bundesliga Jumamosi

Mohammed AbdulRahman26 Oktoba 2007

Bayern bado inaongoza na lakini mambo ni magumu kwa mabingwa watetezi Stuttgart.

https://p.dw.com/p/C7nA
Mshambuliaji wa Bayern Munich Miroslav Klose anayeongoza katika ufungaji wa mabao mengi pamoja na Luca Toni.
Mshambuliaji wa Bayern Munich Miroslav Klose anayeongoza katika ufungaji wa mabao mengi pamoja na Luca Toni.Picha: AP

Werder Bremen inayokamata nafasi ya pili nyuma ya Bayern Munich, inasafirii kuelekea Gelsenkirchen kumenyana na Schalke 04, wakiwa na kazi ya kuziba kidogo mwanya wa tafauti ya pointi 6 na Bayern.

Bremen ilifanikiwa kuchupa hadi nafasi ya pili katika ligi hiyo mwishoni mwa juma lililopita , ikionekana kuwa katika hali nzuri baada ya kushinda michezo sita kati ya 10 iliopita ikiwa ni pamoja na matokeo yakusisimua jumatano katika mashindano ya kombe la vilabu bingwa vya ulaya ilipoibwaga Lazio ya Italia 2-1.

Schalke wako nafasi ya tano na leo wataingia uwanjani nyumbani wakiwa na azma ya kubadili sura ya matokeo ya kulazawa na Chelsea ya Uingereza katika kombe la vilabu bingwa 2-0 hapo Jumatano ,wakati mlinda mlango Manuel Neuer ikikabiliwa na shinikizo kutokana na kile kinachoangaliwa na mashabiki kuwa ni makosa yalioizamisha mjini London.

Katika mechi mbili zilizopita za Bundesliga,Schalke ilitandikwa na Karlsruhe 2-0 na ikaambulia sare ya 1-1 na Hansa Rostock, ambazo zitaumana hii leo. Mshambuliaji hatari wa Schalke na timu ya taifa ya Ujerumani Kevin Kuranyi hata hivyo huenda akalazimika kuwa nje ya chaki leo akikabiliwa na majeraha na kuna wasi wasi iwapo atakuwemo uwanjani .Kocha wa Schalke Mirko Slomka alisema anatarajia matokeo mazuri.

Mabingwa watetezi Stuttgart watatoana jasho jioni ya leo na Bayer Leverkusen. Stuttgart wataingia uwanjani wakijaribu kurudisha matumaini kwa mashabiki wao, baada ya kufungwa na Olympique Lyon ya Ufaransa katika mashindano ya vilabu bingwa vya ulaya. Kushindwa kwa Stuttgart kunaweza kukaiteremsha hadi katika kundi la timu tatu za miwsho zinazokabiliwa na hatari ya kushuka daraja , katika msimamo jumla wa ligi kuu Bundesliga. Lakini mkurugenzi wa kilabu hiyo Horst Heldt ana matumaini amambo yatakua mazuri.

Kwa upande wao miamba ya Bayern Munich yenye pointi 26,chini ya kocha wao Ottmar Hitzfeld watakua uwanjani kesho kuchuana na Borussia Dortmund na Bremen inahitaji ushindi leo dhidi ya Schalke kuwatia kiwewe Bayern ambayo inaongoza Bundesliga ikiwa haijapoteza hata mchezo mmoja na kesho inatarajiwa kuwa na nyota wao na mchezaji wa kiungo Mfaransa Franck Ribery na mlinzi Demichelis ambao wakiuguza mguu na kushindwa kuwemo katika kikosi kilichopambana Alhamisi na Red Star Belgrade ya Serbia katika kombe la UEFA ambapo Bayern ilifanikiwa kukomboa mabao mawili na hatimae kushinda 3-2. Pia nahodha na mlinda mlango Oliver Kahn ameanza mazoezi wiki hii, baada ya operesheni ya mkono.

Mechi nyengine Wolfsburg inaikaribisha Nüremberg,Bochum itakua ugenini huko Berlin kuchuana na Hertha Berlin na Cottbus inayokamata mkia katika nafasi ya 18 itaikaribisha Armenia Bielefeld katika mchezo mwengine hii leo. Ama Hamburg inacheza kesho nyumbani dhidi ya Duisburg. Hadi michuano ya leo inaanza ni Miroslav Klose na Luca Toni, wote wakiwa washambuliaji wa Bayern Munich wanaongoza kwa ufungaji mabao mengi, manane kila mmoja.