1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kivumbi cha soka Euro 2008 kuanza kesho

Liongo, Aboubakary Jumaa6 Juni 2008

Kipyenga cha michuano ya fainali za kombe la Ulaya kinapulizwa kesho huko Geneva na Basel Uswis kwa mapambano mawili ambapo wenyeji Uswis wataingiliana na Jamhuri ya Czech huku Ureno ikipepetana na Uturuki.

https://p.dw.com/p/EEtX
Nyasi za mojawapo ya viwanja vitakavyochezwa fainali za Euro 2008 zikiwa tayari kuhimili mikimiki ya madaluga 22 ya wachezajiPicha: AP

Fainali hizi za Ulaya zinaandaliwa kwa pamoja kati ya Uswis na Austria.


Hii ni mara ya kwanza kwa Uturuki kuibuka tena katika mashindano makubwa toka iliposhiriki fainali za dunia mwaka 2002 huko Korea Kusini na Japan, ambapo iliondoshwa katika nusufainali na Brazil.


Brazil kwa wakati huo ilikuwa ikifundishwa na Felipe Scolari ambaye kwa sasa ndiye kocha wa Ureno.


Timu hizo ziko katika kundi A.


Ujerumani itaanza kampeni zake Jumapili kwa kupambana na Poland katika mji wa Klagenfut huko Austria.Siku hiyo pia wenyeji wenza Austria watapambana na Croatia.


Ujerumani ambayo imewahi kushinda mara tatu ubingwa huo, safari hii ni miongoni mwa nchi ambazo zinapigiwa upatu kuibuka mabingwa.


Washabiki wengi wanaipa nafasi Ujerumani pamoja na kwamba haijawahi kushinda michuano ya fainali hizo katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.


Timu hiyo ikiwa na majogoo kama nahodha Michael Ballack, winga mwenye mbio Odonkwa, washambuliaji, wenye uchu wa kutia mabao, Lucas Podoski, Mario Gomes, Miroslav Klose na Bastian Schweinsteiger, inajiwinda kuondoa jinamizi hilo.


Hata hivyo kiungo wa timu ya Poland Mariusz Lewandowski anaamini kuwa wataifunga Ujerumani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 75.


Amesema kuwa Ujerumani haina kandanda la kiufundi kama Ureno ingawaje ina soka lenye kutumia nguvu.


Poland katika mbio za kuwania kufuzu kwa fainali hizi, ilimaliza ya kwanza mbele ya Ureno kwa pointi nne zaidi.


Lewandowski amesema kuwa anategemea ushindani mkali kutoka kwa Ballack na wenziye hiyoJumapili, na kuongeza kuwa atahakikisha Ballack hapati mwanya wa kusambaza mipira kwa wenziye.


Tayari homa ya michuano hiyo miongoni mwa washabiki hapa Ulaya imefikia katika kiwango cha juu.


Kwa hapa Ujerumani maduka yamekuwa yakifurika washabiki ambao wananunua jezi, kofia na vitu vingine vyenye kuashiria timu ya Ujerumani.


Wamiliki wa migahawa na sehemu nyingizeno za vinywaji wamekuwa wakizidisha idadi ya vinywaji, kufuatia sheria ya kuzuia kunywa nje ifikapo saa nne usiku kuondolewa kwa muda.


Hiyo ni kuwapa nafasi washabiki kuwa huru kupiga kelele pale wanapoguswa na dimba hususani Ujerumani inapofanya vitu vyake.


Kwa upande mwengine  Mkuu wa Shirikisho la Soka la Ujerumani, ametetea uamuzi wa shirikisho hilo, kutumia mamilioni ya fedha kuweka kambi katika hoteli ya kifahari nchini Uswis huku kituo chake kikiwa ni Austria.


Ujerumani itakuwa ikienda kucheza mechi zake Austria na kurudi Uswis katika hoteli hiyo ambayo gharama zake kwa timu nzima ni kiasi cha Euro millioni 1.6 ambazo ni sawa na takriban dola millioni mbili unusu.


Iwapo Ujerumani itashinda kombe hilo shirikisho hilo limesema kuwa kila mchazaji atapewa Euro  laki mbili unusu.


Kambi ya timu hiyo imewekewa meza ya mchezo wa pool pamoja na mpira wa meza ili kuzifanya akili za wachezaji ziwe katika hali nzuri.