Migogoro mibaya kabisa duniani
Kwa mujibu wa Heidelberg Institute for International Conflict Research (HIIK), kulikuwa na migogoro 400 duniani kote mwaka jana, 20 kati yao ikiwa vita. DW inaiangazia baadhi ya migogoro hatari zaidi kati yao.
Hakuna amani kwa karibu
Ama iwe ni kutokana na siasa kali za kidini, malighafi au uroho tu wa madaraka, sababu za migogoro zimekuwa hizo hizo kwa miaka kadhaa sasa. Hali haikuwa tafauti kwa mwaka 2013. Taasisi ya Heidelberg Institute for International Conflict Research (HIIK) imeorodhesha migogoro mingi katika "Kipimo cha Migogoro cha mwaka 2013".
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Huko Kivu, mwaka 2013 jeshi la serikali lilipigana mara kwa mara na kundi la waasi la M23. Baada ya mazungumzo ya amani na serikali, wapiganaji hao waligawika kwenye makundi mbalimbali. Mwishoni mwa mwaka 2013, serikali ya Kongo ilitangaza kuwa imewashinda waasi hao. M23 wamesema kuanzia sasa watakuwa chama cha kisiasa.
Mali
Nchini Mali, wapiganaji wa Kiislamu walijaribu kuchukua madaraka. Mwaka 2012, sehemu kubwa ya kaskazini iliangukia mikononi mwao. Ufaransa ikaingilia kijeshi kwa mashambulizi ya angani na ardhini kuwarudisha nyuma wapiganaji hao wa Kiislamu. Sasa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wana jukumu la kutunza usalama, lakini mashambulizi na mabomu ya kujitoa muhanga yanaendelea.
Nigeria
Kundi la Boko Haram linataka kuanzishwa kwa utawala wa Kiislamu nchini Nigeria. Ili kufikia lengo hilo, kundi hilo linaendelea kuwashambuliwa Wakritsto na Waislamu wenye msimamo wa wastani. Pichani, jamaa wa wahanga wa Kikristo wakichimba kaburi baada ya mashambulizi. Nigeria ni eneo la vita vyengine pia: wakulima wa Kikristo wanapigana na wachungaji wa Kiislamu juu ya ardhi ya malisho.
Sudan
Kwa miaka 10 sasa, makabila mbalimbali yamekuwa yakipigana kwenye jimbo la Darfur dhidi ya vikosi vya serikali ya Sudan na washirika wao. Kwenye mgogoro huu, maji na ardhi ya malisho iko hatarini. Maelfu ya watu wameshakufa kwenye mapigano na mamilioni wamelazimika kukimbia makaazi yao.
Afghanistan
Mapigano yanaendelea nchini Afghanistan baada ya wanajeshi wa NATO kukabidhi udhibiti wa usalama kwa vikosi vya huko. Taliban na makundi mengine ya wanamgambo wanaendelea kupigana na mamlaka za nchi hiyo wakitumia mashambulizi ya kujitoa muhanga na kuvizia. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya raia 2,500 waliuawa mwaka 2013.
Mexico
Biashara ya madawa ya kulevya, kusafirisha wanaadamu, ulanguzi na magendo. Hivi ndivyo makundi ya kihalifu ya Mexico yanavyopata fedha. Ili kulinda mtiririko wao wa fedha, makundi hayo hupigana yenyewe kwa yenyewe na pia na serikali karibuni kila wiki. Matokeo yake, mwaka jana pekee kiasi cha watu 17,000 waliuawa nchini Mexico, kwa mujibu wa takwimu za serikali.
Syria
Katika mwaka wa nne wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, machafuko ndiyo yanayotawala. Nchi hiyo imegawika baina ya vikosi vya Rais Bashar al-Assad, makundi yenye msimamo wa wastani, Waislamu wenye siasa kali, wahuni na wahalifu. Zaidi ya watu 100,000 wameshapoteza maisha yao, kiasi cha milioni tisa wameshakimbia majumba yao. Mgogoro huo unatishia kusambaa hadi nchi jirani.
Ufilipino
Kwa miaka 40 sasa, watu wa Moro wamekuwa wakipigania uhuru wao kusini mwa Ufilipino. Baada ya kipindi cha utulivu kidogo, mgogoro huo ukaanza tena mwaka 2013, huku kundi la waasi la MNLF likitangaza uhuru wa visiwa vilivyo kusini mwa nchi hiyo. Wapiganaji waliojaribu kuuchukuwa mji wa Zamboanga walirejeshwa nyuma na wanajeshi. Zaidi ya watu 120,00 walilazimika kukimbia mapigano hayo.
Somalia
Mapigano kati ya wanamgambo wa al-Shabaab na vikosi vya serikali nchini Somalia yamekuwa yakiendelea kwa mwaka wa nane sasa. Kwa msaada wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, serikali imeweza kuwang'oa madarakani al-Shabaab, lakini bado wanadhibiti sehemu kubwa ya kusini mwa nchi hiyo. Al-Shabaab walihusika na mashambulizi kadhaa ya mabomu kwenye mji mkuu Mogadishu mwaka 2013.
Sudan ya Kusini
Miaka mitatu baada ya kuundwa kwake, Sudan ya Kusini imeendelea kuwa nchi iliyotawaliwa na migogoro ambako vita viwili vinapiganwa. Wapiganaji watiifu kwa makamu wa rais wanapigana na vikosi vya rais, ambao pia wanapigana kwenye uwanja mwengine wa mapambano. Katika nchi jirani ya Sudan, wanajeshi wa Sudan ya Kusini wanasaidia juhudi za kujitenga kwa majimbo mawili yenye utajiri wa mafuta.