1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mikataba ya kuchimba mafuta yazusha mvutano

Kühntopp,C/P.Martin8 Novemba 2007

Utawala wa ndani wa Wakurdi,kaskazini mwa Irak umetia saini mikataba 7 pamoja na makampuni ya mafuta ya kigeni,bila ya kuidhinishwa na serikali ya mjini Baghdad.

https://p.dw.com/p/C777

Kwa maoni ya Baghdad,Wakurdi ambao hapo awali pia walitia saini mikataba 5 pamoja na makampuni ya kigeni,wamepaswa kungojea hadi bunge la Irak litakapopitisha sheria kuhusu mafuta ya taifa hilo.

Maelezo yafuatayo yameandikwa na Carsten Kühntopp na msomaji ni Prema Martin.

Ingawa serikali ya Wilaya ya Kaskazini ya Irak inayodhibitiwa na Wakurdi,ilitoa tangazo dogo tu kwenye tovuti kuhusu mikataba hiyo mipya,ni dhahiri kwamba hatua hiyo ni kuidharau serikali ya Baghdad.

Kwani hii ni mara ya pili kwa Wakurdi hao kutia saini mikataba pamoja na makampuni ya kigeni, kuchimba mafuta katika eneo hilo la kaskazini.Kwa hivyo sasa,jumla ya makampuni 20 ya kigeni yana ruhusa ya kuchimba mafuta katika wilaya hiyo ya kaskazini,nchini Irak.

Mikataba ya kwanza ilitiwa saini na Wakurdi wa Kiiraki katika mwezi wa Septemba-hatua iliyoihamakisha serikali kuu ya Irak,mjini Baghdad.Wakati huo,Waziri Mkuu Nuri al-Maliki alitoa mwito kwa Wakurdi kutotia saini mikataba yo yote,kabla ya kupitishwa sheria inayohusika na mafuta nchini humo.Na Waziri wa Mafuta wa Irak alisema,mikataba itakayotiwa saini na Wakurdi kabla ya kupitishwa sheria hiyo,haitokuwa halali.

Je,Wairaki wagawane vipi utajiri wa mafuta nchini mwao?Kwani jamii zote zinahusika katika taifa hilo jipya la Irak-kuanzia makundi ya kikabila hadi ya kidini na kati ya serikali za wilayani na serikali Kuu mjini Baghdad.

Kwa upande mwingine,Mkuu wa Taasisi ya Taaluma ya Mikakati nchini Irak,Abdel Jabr Fallah anasema, kwa vile serikali kuu na serikali za wilaya zimegawana mamlaka ya kisiasa,basi Wairaki wanapaswa pia kugawana mali ya nchi.Wakati huo huo anauliza:

O-TON FALLAH:

„Lakini mali hiyo watagawiana vipi?Je serikali za wilaya zidhibiti mali hiyo?Kama wilaya nne zina utajiri wa mafuta,lakini katika wilaya 14 hakuna mafuta.“

Duniani,Irak inachukua nafasi ya tatu katika utajiri wa mafuta na gesi.Wataalamu wanaamini, katika siku zijazo,Irak huenda ikawa mzalishaji muhimu kabisa katika sekta ya nishati.Lakini kiwanda cha mafuta cha Irak,hadi hivi sasa kipo katika hali mbaya sana kwa sababu mbali mbali.Kuanzia usimamizi mbaya wa kiuchumi wakati wa utawala wa Saddam Hussein,vikwazo vya Umoja wa Mataifa vya miaka na miaka na pia vurugu na machafuko ya hivi sasa nchini humo.

Irak inahitaji uwekezaji mkubwa kuchimba mafuta kabla ya kuweza kutajirika,lakini hizo ni pesa zinazokosekana.Hadi hivi sasa,Bunge la Irak limeshindwa kuafikiana kuhusu sheria ya mafuta.Kwa hivyo Wakurdi wamejiamulia kuchukua hatua,licha ya kuwepo uwezekano kuwa mikataba inayotiwa saini hivi sasa huenda isiwe halali.