1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milipuko yarindima katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

2 Juni 2011

Nchini Libya, mashambulizi ya ndege za kivita za jumuiya ya kujihami ya NATO yameendelea kuitikisa Tripoli. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa zatuhumu serikali na waasi kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/11Swz
Moshi umetanda TripoliPicha: picture alliance/dpa

Mfululizo wa milipuko sita ilitokea kwa dakika kadhaa katika mji mkuu wa Libya, Tripoli ambao umekabiliwa na mashambulizi kama hayo kutoka kwa NATO kwa wiki kadhaa sasa.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ufaransa AFP, ndege za kivita za jumuiya hiyo zilifanya mashambulizi mengine Jumatatu na Jumanne katika mji huo wa Tripoli huko kwenye vitongoji vya Tajura na Al-Jafra upande wa kusini.

Frankreich Luftwaffe Kampfjet Dassault Rafale über Libyen
Ndege ya Kivita ya Kifaransa katika anga ya Libya.Picha: AP

Jana msemaji wa serikali ya Libya Mussa Ibrahim alisema mashambulizi ya anga ya NATO yameuwa raia 718 na kuwajeruhi wengine zaidi ya elfu 4, tangu kuanza kwa operesheni hiyo Machi 19 mpaka Mei 26.

Hata hivyo kwa upande wake jumuiya ya NATO imepuuza matamshi hayo kwa kusema hakuna uthibitisho.

Naye waziri wa mafuta wa Libya Shukri Ghanem, vile vile amekuwa miongoni mwa wafuasi wa Gaddafi wa hivi karibuni kumuasi kiongozi huyo. Shukri ambaye kwa hivi sasa yupo nchini Italia, amejiuzulu wadhfa wake wa uwaziri.

Amenukuliwa akisema kwamba ameondoka nchini Libya ili ajiunge na vuguvugu la kisiasa kupigania demokrasia ya nchi hiyo dhidi ya ukandamizaji wa bosi wake.

Katika tukio lingine huko Benghazi, mlipuko mkubwa umetokea katika gari moja iliyokuwa imeegeshwa katika eneo la hoteli moja ingawa hakukuwa na madhara yaliyoripotiwa.

Tume maalumu ya uchunguzi iliyoundwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva nchini Uswisi, imeushtumu utawala wa Gaddafi kwa kufanya mashambulizi dhidi ya raia. Tume hiyo imesema utawala huo haukufanya tu uhalifu dhidi ya binadamu, bali pia uhalifu wa kivita.

Ingawa tume ya uchunguzi iliyoundwa na baraza hilo haikugundua visa vya uhalifu kwa upande wa waasi, tume hiyo imesema waasi pia walifanya vitendo ambavyo ni uhalifu wa kivita.

Tume hiyo imefikia uamuzi kwamba jeshi la Libya limefanya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.

Wajumbe 47 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa walianza kufanya uchunguzi huo Februari mwaka huu baada ya utawala wa Gaddafi kuruhusu jeshi kufanya mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Mwandishi: Sudi Mnette//AFP

Mhariri:Josephat Charo