1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miriam Makeba ameiaga dunia

Hamidou, Oumilkher10 Novemba 2008

Mama Afrika,amefariki akiwa katika harakati za kuhimiza upendo na amani

https://p.dw.com/p/FqjA
Miriam Makeba katika tamasha moja mwaka 2005Picha: AP



Mama Afrika,Sauti ya Afrika ,Miriam Makeba,ameiaga dunia akiwa na umri wa miaka 76,baada ya kumaliza tamasha dhidi ya Mafia nchini Italy.


Ugonjwa wa moyo ndio sababu ya kuiaga dunia bibi huyo mwenye sauti ajabu kabisa .Akijivunia umaarufu na kugeuka wajih wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na mtengano Apartheid,Miriam Makeba,aliyezaliwa Johannesburg  March nne mwaka 1932 na ambae nyimbo yake Pata Pata imejipatia umaarufu katika kila pembe ya dunia,kila wakati alikua akishadidia umuhimu wa watu kupendana,kuishi kwa amani na kuvumiliana.


Unaweza kusema amefariki akiwa jukwaani,usiku wa jana kuamkia leo,baada ya kuimba,katika tamasha dhidi ya uhalifu na dhidi ya ubaguzi.


Tamasha hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya watu elfu moja,katika mtaa wa Caserte,kusini mwa Italy, iliwaleta pamoja wasanii wengine pia,ili kumuunga mkono muandishi vitabu wa kitaliana Roberto Saviano,aliyeandika kitabu "Gomorra",kufichua visa vya uhalifu vya Mafia.


 Ni katika mtaa huo huo wa karibu na Neapolis ambako wahamiaji sita wa kiafrika na mtaliana mmoja waliuliwa na watu wasiojulikana mwezi September mwaka huu.


"Alikua wa mwisho kupanda jukwaani,na baadae akapigwa na kizungu zungu" amesema hayo mpiga picha mmoja  mbele ya maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP.


Kwa mujibu wa shirika la habari la Italy,ANSA,Miriam Makeba amefariki dunia baada ya kupelekwa katika hospitali ya Pineta Grande.


Miriam Makeba,ambae jina lake la kuzaliwa ni Uzenzile,alishuhudia kuingia madarakani waafrikanda nchini Afrika kusini mnamo mwaka 1947.Aliipa kisogo nchi yake akiwa na umri wa miaka 27,ili kujiendeleza kimuziki ,bila ya kujua kwamba atajikuta akipigwa marufuku kurejea nchini kutokana na msimamo wake dhidi ya Apartheid.


Alipitisha miaka 31 uhamishoni,barani ulaya,na Marekani hadi pale Nelson Mandela alipomsihi akubali kurejea nyumbani mnamo mwaka 1990.


Mama Afrika,Miriam Makeba atakumbukwa daima....