1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kwaendelea kutokota

27 Januari 2011

Tayari watu sita wameshauawa hadi sasa nchini Misri na polisi inawashikilia watu 1,000, kufuatia maandamano makubwa yanayoendelea kufanyika waandamanaji wakishinikiza kuondoka madarakani utawala wa Rais Hosni Mubarak.

https://p.dw.com/p/105og
Maandamano yapamba moto Misri
Maandamano yapamba moto MisriPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, polisi nchini Misri wanaonekana kuzidiwa nguvu na wimbi kubwa la waandamanaji linalozidi kumiminika mitaani, ambalo inasemekana limetiwa moyo na yale yanayoitwa 'Mapinduzi ya Asumini', yaliyofanikiwa kumng'oa Rais Zine Al-Abidine Ben Ali wa Tunisia, kiasi ya wiki mbili zilizopita.

Waandamanaji hao sasa hawaheshimu tena amri ya polisi, na vuguvugu la vijana, lijuilikanalo kama Aprili 6, limeapa kwamba linaingia tena mitaani leo (Alhamis, 27 Januari 2011) nzima, na limeitisha maandamano makubwa zaidi baada ya sala ya Ijumaa hapo kesho. Wanasema lengo lao ni lile lile la ndugu zao wa Tunisia. Kuung'oa utawala wa kidkteta.

"Tunachotaka ni kimoja tu, tuondokane na Mubarak, tuondokane na utawala wa yeye na mwanawe."

Wamisri wakaidi amri ya serikali

Waandamanaji wakikabiliana na polisi mjini Cairo
Waandamanaji wakikabiliana na polisi mjini CairoPicha: dapd

Jana, serikali ya Misri ilitangaza kuyapiga marufuku maandamano haya, ingawa ilikuwa imeyaruhusu yalipoanza hapo Januari 25. Lakini wakiwa wamevunjika moyo kabisa na utawala wa miongo mitatu, wanaoamini umewakandamiza vya kutosha, waandamanaji wamekaidi amri hiyo ya serikali na wameendelea kujazana kwa maelfu katika mitaa ya miji ya Cairo, Suez na Alexandria kudai kumalizika kwa utawala wa Mubarak.

"Televisheni ya taifa inazungumzia mageuzi. Sisi hatutaki mageuzi. Tunataka kuupindua kabisa utawala huu."

Katika saa za usiku hapo jana, polisi walipambana na waandamanaji katika mitaa ya Cairo, huku polisi wakitumia mabomu ya machozi na risasi za mipira na waandamaji wakitumia mawe. Hiyo ilikuwa ni baada ya waandamaji hao kukiuka vizuizi vilivyowekwa kuelekea kwenye jengo la wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

Vurugu katika miji mikubwa

Vurugu kubwa zaendelea huku majeruhi wakiongezeka
Vurugu kubwa zaendelea huku majeruhi wakiongezekaPicha: AP

Huko katika mji wa bandari wa Suez, waandamanaji walitumia fashifashi kuyatia moto majengo ya serikali na kuyavamia na baadaye kuyakalia kamao makuu ya chama tawala cha National Democratic Party katika eneo hilo.

Matabibu wanasema waandamanaji 55 na polisi 15 walijeruhiwa katika makabiliano haya, huku polisi ikisema inawashikilia makumi ya watu katika mji mwengine wa Alexandria.

Marafiki waanza kumuacha mkono Mubarak?

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: AP

Na katika kile kinachoonekana kuchelea aibu iliyoikuta Ufaransa kwa kuchelewa kwake kuitambua nguvu ya umma wa Tunisia, na kuendelea kumuunga mkono Ben Ali hadi karibuni na mwisho wa utawala wake, tayari marafiki wakubwa wa Rais Hosni Mubarak, nchi za Marekani na Uingereza, wameshamtaka mshirika wao huyo, kuitikia kile wanachokiita "matakwa ya haki ya kutoka kwa umma" wa Misri, ingawa hawakusema ikiwa matakwa hayo ni yale ya kuondoka Mubarak na safu yake madarakani.

Hapo jana jioni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hilary Clinton, aliitaka serikali ya Misri kufanya mabadiliko makubwa.

"Tunatarajia kuwa serikali ya Misri itatumia fursa hi kufanya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumii na kijamii ambayo yataakisi maslahi ya Wamisri. Tutaendelea kushirikiana na jumuiya za kiraia, serikali na watu wa nchi hii tukufu." Alisema Bi Clinton.

Waziri Mkuu Ahmed Nazif aliwataka waandamanaji kutulia na kwamba serikali yake inaahidi kulinda uhuru wa watu kutoa maoni kwa njia za halali. Maandamano haya ni makubwa zaidi kuwahi kufanyika nchini Misri tangu yale ya mwaka 1977, yaliyochochewa na kupanda kwa bei ya mkate, miaka minne kabla ya Mubarak kuingia madarakani.

Katika maandamano hawa yanayoendelea sasa, waandamanaji wanadai kuchoshwa na ukadandamizaji unaofanywa na na vikosi vya usalama dhidi yao, miongo mingi ya hali ya hatari iliyotangazwa na Mubarak, mishahara midogo na bei kubwa za vyakula.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa bunge wa Novemba 2011, ambao wengi wanauchukulia kuwa chama tawala kiliiba kura kuruhusu wagombea wake kushinda kwa kiwango cha juu, hali nchini Misri haijarudi tena kuwa shwari hadi sasa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman