1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kwafukutana, majenerali, wandamanaji wauawa

Admin.WagnerD28 Novemba 2014

Watu wapatao wanne wameuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mji mkuu wa Misri, Cairo, wakati maelfu ya watu walipojitokeza kuandamana kuipinga serikali ya rais wa nchi hiyo Abdel Fatah al-Sisi.

https://p.dw.com/p/1Dwhk
Symbolbild Arabischer Frühling Ägypten
Picha: AFP/Getty Images/M. Abed

Waandamanaji hao waliuwawa baada ya maafisa wa usalama kufyetua risasi katika wilaya ya Matrya mashariki mwa mji wa Cairo. Maandamano ya kundi la Salafi Front yalifanyika katika maeneo ya Nile Delta na yalifanyika sambamba na maandamano ya kila Ijumaa ambayo yamekuwa yakifanywa na wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislamu kilichopigwa marufuku tangu kuondolewa madarakani aliyekuwa rais wa Misri, Mohammed Mosri.

Rais wa sasa wa Misri Abdul-Fatah al-Sisi.
Rais wa sasa wa Misri Abdul-Fatah al-Sisi.Picha: picture-alliance/dpa

Majenerali wa kijeshi wauawa

Maafisa wawili wa ngazi ya juu wa jeshi la Misri waliuwawa mapema Ijumaa huku maafisa wa usalama wakiwatia mbaroni waislamu zaidi ya 100 kabla kufanyika maandamano ya kuipinga serikali. Maafisa hao waliuwawa katika matukio tofauti ya mashambulizi ya risasi yaliyofanywa na watu wasiojulikana mjini Cairo ambapo pia wanajeshi wawili walijeruhiwa.

Duru za usalama zinasema Brigedia wa jeshi alipigwa risasi katika kitongoji cha Gesr al-Suez mjini Cairo wakati washambuliaji walipofyetua risasi katika eneo la kuegesha magari kabla kutoroka.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndandi ya Misri Hani Abdel-Latif alisema mabomu saba yalitenguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Mwito uliotolewa na Waislamu wa makundi ya Salafi kuitisha maandamano ya nchi nzima kuiangusha serikali na kuilinda dini yao ni jaribio la kwanza katika miezi kadhaa kufanya maandamano makubwa huku kukiwa na ukandamizaji mkubwa tangu jeshi lilipomuondoa madarakani rais Morsi mwaka uliopita.

Polisi waliojihami kwa silaha wakiweka ulinzi mkali kufuatia wito wa maandamano ya kuipinga serikali.
Polisi waliojihami kwa silaha wakiweka ulinzi mkali kufuatia wito wa maandamano ya kuipinga serikali.Picha: Reuters/A. Waguih

Ulinzi waimarishwa maeneo nyeti

Maafisa wa vikosi vya usalama, ambao awali waliapa kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji, walifanya operesheni kubwa tangu alfajiri. Magari yasiyoweza kutobolewa na risasi yalikuwa yanapiga doria katika maeneo yote ya mji wa Cairo huku vizuwizi vikitumiwa kuzifunga barabara zinazoelekea makao makuu ya idara ya usalama, ikulu ya rais na wizara ya ulinzi.

Vituo vya televisheni vilionyesha moja kwa moja vidio ya waziri mkuu wa Misri Ibrahim Mahlab akiongoza kikao maalumu cha baraza la mawaziri kufuatilia matukio yanayoendelea. Usalama uliimarishwa nchini kote huku kukiwa na hofu ya kutokea machafuko.

Wakati maandamano yaliyofanywa na wafuasi wa Morsi hayakuzingatia misingi ya dini, na badala yake kujikita zaidi katika kupinga mapinduzi dhidi ya kiongozi wao na kupigania demokrasia irejee Misri, miito ya maandamano ya Ijumaa yalijumuisha wazi wazi kauli za kidini. Kundi la Salafi lililoyaandaa maandamano hayo lilionya juu ya vita dhidi ya Uislamu na kuwahimiza waandamanaji wainue Qur'ani kwa mikono yao. Kauli mbiu ya maandamano ya Ijumaa ni "Mapinduzi ya Vijana wa Kiislamu".

Rais wa Misri aliepinduliwa Mohamad Mursi akiwa kizimbani.
Rais wa Misri aliepinduliwa Mohamad Mursi akiwa kizimbani.Picha: STR/AFP/Getty Images

Kundi la Salafi Front lilichapisha maelekezo katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, likiorodhesha majina ya misikiti itakayotumiwa kama maeneo ya kukusanyika na kuwataka wafuasi kupiga kelele kusema Mungu ni Mkubwa mara tu sala itakapomalizika.

Kundi la Udugu wa Kiislamu la rais wa zamani Mohammed Morsi limeuunga mkono mwito huo lakini likawaonya wafuasiw ake dhidi ya kuburuzwa na kuingizwa katika makabiliano yanayoweza kuibua machafuko.

Mwandishi: Josephat Charo/APE
Mhariri: Iddi Ssessanga