1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kwawaka moto

Saumu Ramadhani Yusuf29 Januari 2011

Ghasia kati ya maafisa wa polisi na waandamanaji zimetapakaa katika miji mbali mbali nchini Misri, ambapo hadi sasa maelfu ya waandamanaji wanaendelea kuingia mitaani, huku kiasi ya watu 100 wanaripotiwa kufariki.

https://p.dw.com/p/107A9
Waandamanaji mjini Cairo
Waandamanaji mjini CairoPicha: AP

Waandamanaji walifyetuliana risasi na vikosi vya usalama na vile vya kupambana na fujo katika eneo la makao yao makuu. Waandamanaji katika mji huo wa Sheikh Zuweid wanataka Rais Hosni Mubarak aondolewe madarakani pamoja na kutaka ajira, umiliki wa ardhi na kuachiwa huru watu wanaoshikiliwa jela.

Mamia kwa maelfu ya waandamanaji wamekusanyika katika uwanja wa Tahrir katikati ya mji wa Cairo wakimtaka rais Mubarak aondoke madarakani.

Mubarak aanza kukimbiwa na washirika

Rais Hosni Mubarak
Rais Hosni MubarakPicha: dapd

Hali ikizidi kuwa mbaya kuelekea utawala wa Rais Mubarak mpambe wa karibu wa mwanawe rais huyo na ambaye ni mmoja kati ya vigogo wanaokosolesolewa na waandamanaji amejiuzulu kutoka chama tawala.Taarifa hizo zimetangazwa na Televisheni ya taifa.

Waandamanaji waliivamia na kuichoma moto mojawapo ya ofisi zake kubwa katika eneo la Mohandiseen mjini Cairo.Baraza zima la mawaziri wa rais Mubarak limejiuzulu rasmi hii leo kufuatia ahadi ya rais aliyoitoa mapema hii leo kwamba angeivunja serikali hiyo.

Kwa mujibu wa kituo cha Al Jazeera idadi ya waliouwawa nchi nzima imefikia watu 100, 36 wakiwa wameuwawa mjini Alexandria. Kufuatia hali nchini humo mashirika ya safari yamehairisha safari za kuelekea nchini Misri hii leo wakati nchi mbali mbali zikiwatahadharisha upya raia wake kujiepusha kusafiri nchini humo.

Mataifa yazuia watu wao kutembelea Misri

Jumuiya ya Kimataifa yatiwa wasiwasi na hali ya Misri
Jumuiya ya Kimataifa yatiwa wasiwasi na hali ya MisriPicha: DW

Utawala wa Japan umewataka raia wake wote walioko nchini Misri waondoke ikiwa wanaouwezo wa kufanya hivyo au wajiepushe kuwa karibu na maandamano hayo pamoja na mikutano.

Australia pia imewataka raia wake wasisafiri Misri. Aidha nchi hiyo pia imeonya kwamba imeendelea kupokea ripoti za kutokea mashambulio ya kigaidi yanayopangwa kulenga maeneo kadhaa ya Misri ikiwemo maeneo yanayopendwa sana na watalii.

Barani Ulaya mashirika ya usafiri ya Ubelgiji yameamua kufuta safari zote za kitalii za kwenda Misri lakini mashirika hayo hayajapanga kuwaondoa watalii walioko Misri. Nchi nyingine za Ulaya ambazo zimewatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri Misri ni pamoja na Austria, Uingereza, Bulgaria, Denmark, Ufaransa na Sweden pamoja na Marekani na Israel.

Jeshi laonekana kuingilia kati

Wanajeshi wakiuzunguka uwanja wa Tahrir
Wanajeshi wakiuzunguka uwanja wa TahrirPicha: dapd

Jeshi la Misri limetoa taarifa likisema mtu yoyote atakayekiuka amri ya kutotoka nje iliyowekwa baada ya siku kadhaa za maandamano hayo ya kuipinga serikali, atajiweka hatarini.

Upande mwingine, Umoja wa Afrika umesema unawasiwasi na hali hiyo ya machafuko ya kisisasa nchini Misri. Mkuu wa kamisheni ya Umoja huo, Jean Ping, katika taarifa hiyo amesema kwamba Misri iko katika wakati mgumu na ni hali ya kufuatiliwa kwasababu inatia wasiwasi. Umoja wa Afrika unakutana katika mkutano wake wa kilele wa siku mbili kuanzia Jumapili.

Kikao hicho bila shaka kinategemewa kugubikwa na suala la wimbi la machafuko ya kisiasa barani humo kuanziaTunisia, Cote d'Ivoire hadi Misri huku Sudan nako hali ikiwa pia ni ya kuangaliwa kwa ukaribu.

Mwandishi: Saumu Ramadhani Yusuf
Mpitiaji: Mohammed Khelef