1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri na Sudan zavutana ujenzi wa bwawa mto Nile

Sylvia Mwehozi
12 Januari 2018

Mgogoro wa kidiplomasia baina ya Misri na Sudan umeingia katika ugomvi wa muda mrefu juu ya ujenzi wa bwawa unaofanywa na Ethiopia katika mto Nile, ambao Cairo inaona kama kitisho. 

https://p.dw.com/p/2qlQp
Malakal in Südsudan
Picha: Reuters

Siku ya Alhamis, Sudan ilionya rasmi juu ya vitisho katika mpaka wake wa mashariki kutoka kwa vikosi vya Misri na Eritrea, mnamo ambapo Misri pia imejiingiza katika mgogoro wa pembe tatu wa eneo linalozozaniwa na Cairo na Khartoum.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Sudan kwa ghafla ilimuita nyumbani balozi wake wa Misri, ikiwa ni sura mpya katika mapambano yaliyoanza msimu uliopita wa majira ya joto ikiwa ni pamoja na kujiondoa katika biashara na ambayo yameshamiri katika wiki za hivi karibuni.

Mzozo huo wa kidiplomasia unafanya vigumu sana kushughulika na tatizo lingine linaloweza kuripuka katika uhusiano. Ufadhili wa Sudan kwa Ethiopia kwenye ujenzi wa bwawa linalogharimu bilioni 5 kwenye mto Nile, unaweza kuzuia usambazaji muhimu wa maji. Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi ameliita bwawa hilo kuwa ni suala la kufa na kupona.

Mahasimu wote wa kikanda karibu na bahari ya Shamu wanaingiliana, anasema Kelsey Lilley mkurugenzi katika kituo cha Afrika, kwenye baraza la Atlantiki, akiongeza kwamba "bwawa lenyewe ni ghadhabu kubwa katika nchi zote tatu". Na wakati nchi zote tatu zikikuna vichwa juu ya bwawa hilo kwa miaka kadhaa, mzozo baina ya Misri na Sudan unazidi kuongezeka kwa haraka.

Äthiopien Grand Renaissance Staudamm al-Sisi al-Bashir Desalegn
Marais wa Ethiopia Abdel-Fattah al-Sisi, wa Sudan Omar al-Bashir , na waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam DesalegnPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Mgogoro mkubwa umechangia kudhoofika kwa mazungumzo baina ya Misri, Sudan na Ethiopia juu ya namna gani ya kusimamia athari za bwawa, hata wakati muda unazidi kusonga. Bwawa hilo limekamilika kwa asilimia 60 na Ethiopia inaweza kuanza kujaza hifadhi haraka msimu huu wa majira ya joto, na kuacha muda mfupi wa kupata ufumbuzi bora.

Bwawa hilo katika mto Nile, kwenye vilima yya Ethiopia limekuwa ni ndoto tangu mwaka 1960. Lakini ilikuwa tu ni 2011, wakati Misri ilipokabiliwa na vuguvugu la mapinduzi ya uarabuni na vurugu za ndani, na ndipo Ethiopia ilipofanya uamuzi wa kuanza ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme wa maji barani Afrika.

Tangu wakati huo, Misri imeshikwa na hofu ya uwezekano wa athari. Bwawa hilo ambalo ni mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwenye mto Nile litaiwezesha Ethiopia kufikia malengo yake ya kuzalisha umeme wa ziada.

Itategemea ni kwa haraka kiasi gani Ethiopia itaweza kulijaza bwawa hilo, lakini usambazaji wa maji kwenda Misri unaweza kuzuiliwa, kitisho muhimu kwa nchi ambayo ni tegemezi kwa kilimo ambacho tayari kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

Ethiopia pia inaweza kuamua kulijaza bwawa hilo taratibu kwa kipindi cha miaka 15, suala ambalo litapunguza athari ya usambazaji maji licha ya kwamba itachelewesha faida ya bwawa hilo. Lakini Ethiopia ambayo imekumbwa na maandamano ya mwaka mzima ya kuipinga serikali yaliyoanza agosti 2016, na kusababishwa kutangazwa kwa hali ya hatari kwa miezi 10, bila shaka haiwezi kusubiri kipindi chote hicho anasema, Lilley.

Ägypten Kairo Nil-Fluss
Boti ya wavuvi ikielea katika maji yaliyochafuliwa ya mto Nile Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Ammar

Bwawa hilo lilisababisha majadiliano juu ya hatua za kijeshi mwaka 2013, ambapo rais Mohamed Morsi alitishia kwamba ikiwa usambazaji maji utaingiliwa, umwagaji damu ulikuwa ni njia mbadala. Mapema wiki hii, alitangaza mpango wa Misri wa ujenzi wa mtambo wa kuchuja maji ya bahari ili kupata maji safi, Sisi ameapa kulinda maslahi ya Misri katika maji ya mto Nile.

Nchi hizo zilionekana kumaliza tofauti zao mwaka 2015 kwa kufikia makubaliano ya namna gani ya kusimamia mradi lakini tangu wakati huo zimeshindwa kukubaliana hata namna ya kukabiliana na athari za bwawa hilo. Na sasa mapambano yanayoongezeka baina ya Misri na Sudan yanatishia kudhoofisha ushirikiano. Vyombo vya habari vya Ethiopia viliripoti mapema mwezi huu kwamba Misri inafikiria kuiweka kando Sudan katika mazungumzo juu ya bwawa hilo licha ya kwamba Misri yenyewe imekanusha ripoti hizo.

Jukumu la Sudan ni muhimu sana kwasababu iko katikati mwa Misri na Ethiopia kijografia na kisiasa. Misri na Sudan kwa muda mrefu zimegawana maji ya mto Nile kati yake, kulingana na makubaliano ya mkataba wa mwaka 1959 ambao hauijumuishi Ethiopia. Kwa kutumia maji kidogo ya mto huo zaidi ya ilivyokubalika, kwa miaka kadhaa Sudan imekuwa ikiruhusu maji zaidi kwenda Misri, ambayo imetumia maji zaidi kuliko inavyotakiwa.

Lakini katika miaka ya karibuni, Sudan imefikiria kuongeza matumizi yake ya maji ikilenga kuboresha sekta yake ya kilimo. Kwasababu ina matumaini ya kutumia bwawa hilo kwa kilimo cha umwagiliaji, Sudan imejisogeza karibu na Ethiopia na kuunga mkono mradi huo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Saumu Yusuf