1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yaitia mashaka Marekani

27 Desemba 2013

Marekani imepaza sauti yake dhidi ya hatua ya serikali ya Misri kulitangaza kundi la Udugu wa Kiislamu, huku ikilaani mashambulizi yaliyotokea hivi karibuni dhidi ya makao makuu ya polisi pamoja na basi.

https://p.dw.com/p/1AhLx
Waandamanaji wanaomuunga mkono Rais Mohamed Mursi nchini Misri.
Waandamanaji wanaomuunga mkono Rais Mohamed Mursi nchini Misri.Picha: picture-alliance/dpa

Rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Mursi, yuko kizuizini. Waziri Mkuu wake, Hashim Qandil, amekamatwa wiki hii, na kimsingi viongozi wote wa kundi la Udugu wa Kiislamu ama wameshakamatwa, wameuawa, au wanasakwa. Wote wakishukiwa kwa mauaji, uhaini na ugaidi.

Kwa hivyo, tangazo la hapo Alkhamis kwamba kuanzia sasa Udugu wa Kiislamu ni magaidi na watashughulikiwa kama magaidi, halina tafauti na wala halibadilishi chochote katika namna ambavyo serikali ya mpito imekuwa ikiwashughulikia wapinzani wake tangu kuondoshwa madarakani kwa Mursi.

“Hapana shaka, tangazo hili linahalalisha tu matumizi ya nguvu zisizo mipaka dhidi ya Udugu wa Kiislamu, na hivyo kikubwa tutarajie kuongezwa kwa hatua hizo ambako nako hakuwezi kuisaidia Misri kwenda kwenye jamii ya kidemokrasia na kiraia.” Anasema Günter Meyer wa Taasisi ya Masomo ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Mainz.

Marekani yafadhaishwa

Hapo jana (tarehe 26 Disemba), Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alielezea wasiwasi wake juu ya hatua hizo za Misri kuliandama kundi la Udugu wa Kiislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.Picha: picture-alliance/dpa

Akizungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Misri, Nabil Fahmi, Kerry alilaani mashambulizi dhidi ya makao makuu ya polisi mjini Mansoura siku ya Jumanne na ya jana dhidi ya basi mjini Cairo, lakini pia akakosoa hatua za serikali dhidi ya Udugu wa Kiislamu, kukamatwa na kuwekwa kizuizini ovyo ovyo kwa wale wanaotofautiana na serikali.

Mawaziri hao wawili walikubaliana juu ya ulazima wa kuwepo kwa amani na utulivu nchini Misri, lakini Kerry alisema kuna haja kubwa zaidi ya maendeleo hayo ya kisiasa kupatikana kwa njia za kisiasa na pia kuheshimiwa kwa haki za binaadamu.

Marekani ni mchangiaji mkubwa wa bajeti ya kijeshi ya Misri, lakini tangu jeshi kumpindua Rais Mohamed Mursi mwezi Julai mwaka huu, mahusiano kati ya pande hizo mbili yamekuwa ya mashaka.

Uamuzi watokana na mashambulizi ya Mansoura

Kwa mujibu wa serikali, uamuzi huu wa kulitangaza kundi la Udugu wa Kiislamu kuwa la kigaidi unatokana na mashambulizi ya bomu ya Mansoura siku ya Jumanne, ambapo watu 16 waliuawa na wengine wapatao 100 kujeruhiwa, wengi wao maafisa wa usalama.

Jengo lililoshambuliwa na magaidi mjini Mansoura, Misri.
Jengo lililoshambuliwa na magaidi mjini Mansoura, Misri.Picha: Reuters

Mashambulizi hayo yalilaaniwa vikali na Udugu wa Kiislamu waliyoyaita kuwa ni ishara ya kuikwamisha nchi, lakini kundi la Ansar al-Bait Maqdis, ambalo serikali inasema lina mafungamano na Udugu wa Kiislamu, lilitangaza kuhusika, kwa kile lilichosema ni kulipiza kisasi “damu ya Waislamu”.

Tangu Mursi aondoshwe madarakani mwanzoni mwa mwezi Julai, maelfu ya watu wameshauawa, kujeruhiwa na kukamatwa katika jitihada za serikali na jeshi kupambana na upinzani dhidi yao.

Kwa upande mwengine, mashambulizi dhidi ya vyombo vya usalama yameongezeka na sasa kuvuuka mpaka wa jimbo la Sinai yalikoanzia na kusambaa kwenye maeneo mengine ya nchi, ukiwemo mji mkuu Cairo.

Mashambulizi dhidi ya basi katika kiunga cha Nasr hapo jana, yalijeruhi watu watano na hivi leo mwanafunzi mmoja ameuawa alipokuwa kwenye maandamano ya kumuunga mkono Mursi kwenye eneo hilo hilo.

Afisa wa ngazi za juu wa Chama cha Uhuru na Haki, tawi la kisiasa la Udugu wa Kiislamu, Ibrahim El-Sayed, alisema hapo jana kwamba licha ya mauaji na kukamatwa kwa watu wao, “maandamano yataendelea” na akauita uamuzi huo wa kuwatangaza kuwa maadui kuwa usio na maana yoyote kwao.

Mwandishi: Diana Hodali/Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba