1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yalipa kisasi dhidi ya Ghana

Sekione Kitojo
14 Novemba 2016

Misri jana Jumapili (13.11.2016)ilifanikiwa kupata ushindi muhimu dhidi ya Ghana wakati timu hiyo ikiwania kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/2SgSn
Fussball WM-Qualifikation Ägypten gegen Ghana
Mlinda mlango wa Misri Essam el-Hadary akishangiria ushindiPicha: Getty Images/AFP/M. El-Shahed

Katika  bara  la  Afrika , Misri  ililipa  kisasi  kipigo  cha kudhalilisha   katika  mchezo  wa  kombe  la  dunia  dhidi ya  ghana  miaka  mitatu  iliyopita  kwa  kuishinda   timu hiyo  Black Stars  kwa  mabao  2-0  jana  Jumapili   ambapo mashabiki  85,000  walishuhudia  pambano  hilo  mjini Alexandria.

Ghana  ilishinda  kwa  mabao 6-1  katika  mchezo  wa mkondo  wa  kwanza  wa  wa  kombe  la  dunia  mwaka 2014  na  ushindi  huo  uliendeleza  maumivu  ya  Misri , ambayo  haikushiriki  katika  fainali  za  kombe  la  dunia tangu  mwaka  1990.

Ghana  ambayo  inawania  kufuzu  kucheza  katika  fainali za  kombe  la  dunia  kwa  mara  ya  nne  mfululizo , ilitawala  kipindi  cha  pili bila  ya  kuweza  kupata  njia  ya kumfikia   mlinda  mlango  mwenye  umri  wa  miaka  43 Essam El Hadary.

Fussball WM-Qualifikation Ägypten gegen Ghana
Wachezaji wa Ghana wakipambana na Misri mjini AlexandriaPicha: Getty Images/AFP/M. El-Shahed

Katika  michezo  mingine Guinea  iliangukia  pua  pale ilipolazwa  kwa  mabao  2-1  dhidi  ya  Jamhuri  ya Kidemokrasi  ya  Congo  jana  Jumapili  na  Tunisia  iliibuka kidedea  dhidi  ya  Algeria  kwa  ushindi  wa  bao 1-0.

Kocha  wa  timu  ya  taifa  ya  Afrika  kusini Ephraim Mashaba  amesitishwa  kazi  na  chama  cha  kandanda nchini  humo  baada  ya  kuhusika  katika  mvutano  na maafisa  kufuatia  ushindi  wa  timu  hiyo  katika  kombe  la dunia  dhidi  ya  Senegal  mwishoni  mwa  juma.

Präsident der Südafrikanische Fussballverband Danny Jordaan
Rais wa shirikisho la soka nchini Afrika kusini Danny JordaanPicha: picture alliance/AP Images/E. Risch

Mashaba  atakosa  kuwapo  katika  benchi  la  ufundi  la timu  hiyo  Bafana Bafana  kesho  Jumanne  dhidi  ya Msumbiji  na  anakabiliwa  na  kikao  cha  nidhamu kuhusiana  na  madai  ya  tabia  ya  kiburi  dhidi  ya  rais wa  shirikisho  la  kandanda  nchini  Afrika  kusini  SAFA Danny Jordaan  na  wageni  wake,  ambao  walikwenda kuipongeza  timu  katika  vyumba  vya  kuvalia  baada  ya ushindi  wa  mabao 2-1  siku  ya  Jumamosi  dhidi  ya Senegal  mjini  Polokwane.

 

Mwandishi:  Sekione  Kitojo

Mhariri: Yusuf  Samu