1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yatamba mbele ya Kameroun (4:2)

23 Januari 2008

Mabingwa Misri walipeleka salamu kali kwa mahasimu wengine katika Kombe la afrika baada ya kuwazaba Kameroun 4:2.

https://p.dw.com/p/CwPP

Mabingwa watetezi Misri jana walitoa onyo kali kwa wale wote wanaojitapa kwamba watarudi Cairo bila ya kombe.Kwa kuwazaba simba wa nyika-Kamerun mabao 4:2, Misri jana imetoa salamu zake kwa Ghana ,Ivory Coast na Moprocco kwamba, hawakusudii kuondoka Accra bila ya kombe waliokuja nalo.

Chipolopolo-Zambia nayo ilifyatua risasi 3 kali kuihilikisha Sudan,mabingwa wa Afrika mashariki na kati .

Leo ni zamu ya Simba wsa Terange-Senegal na Tai wa Carthage-Tunisia kuingia uwanjani mwanzoni mwa changamoto za kundi C kabla Bafana Bafana kupimana nguvu na jirani zao Angola.

Magoli yanaendelea kumiminika wavuni katika kombe hili la 26 la Afrika nchini Ghana kwa kutiwa jana kimiyani mabao 9 na mengi zaidi yanatazamiwa leo pale Senegal ikitimiza miadi yake na Tunisia na Angola ikipanga kuwafumania chipukizi Bafana Bafana. Jumla ya magoli 20 yameingia kapüuni hadi sasa kutoka kombe hili la Afrika.

Misri,mabingwa watetezi waliwachezesha simba wa nyika jana kindumbwe-ndumbwe na kuwazaba mabao 4-2 ya Samuel Eto-o-jogoo lao pekee lililowika.

Mshambulizi wa Hamburg katika Bundesliga-Mohamed Zidan alilifumania lango la simba wa nyika mara 2 akimuuigiza mwenzake Hosni Rabou alietikiswa pia wavu mara 2.Hata samuel Eto’o alipiga hodi mara 2 katika lango la Misri na kukaribishwa ndani.

Licha ya ushindi huo wazi, Misri inashikilia kwamba mlango wa kundi hili C kuingilia duru ijayo ungali bado wazi kwa kila mmoja bado kupita.Kocha wa Misri , Hassan Shehata ,alisema ushindi wa jana ni wa kuridhisha kabisa dhidi ya mabingwa mara 4 wa Afrika-Kamerun,lakini timu yake bado haikukata tiketi ya duru ijayo ya robo-finali.Misri imebidi kucheza jana bila ya mastadi wake wengi miongoni mwao nahodha wao Ahmed Hassan na mshambulizi Abou Terrika.

Kocha wa simba wa nyika,mjerumani Otto Pfister aliungama kwamba,Misri waliwaibisha simba wa nyika.Kwani, asema hasa kipindi cha kwanza,Misri ilitamba kweli.

Katika mpambano wapili jana,chipolopolo-zambia kwenye mpambano wao wa kwanza wa kombe la Afrika tangu 1994 waliwatandika mamba wa mto Nile-Sudan risasi 3 licha ya vishindo vikubwa vya mamba hao mwishoe,walikata roho.Ilikua risasi ya kwanza ya James Chamanga iliowazika mamba wa mto nile-mabingwa Afrika masdhariki na kati.Mabao 2 mengine-moja kutoka kwa Jacob Mulenga na la jengine la Felix Katongo,yalitosha kuwazika mamba na kupeleka buriani mto Nile.

Wakati leo ni zamu ya Senela kuonana na Tunisia na Afrika kusini na Angola, simba wa nyika Kameroun wanakutana na chipolopolo-Zambia na mabingwa Misri na Sudan huko Kumasi,jumamosi hii ijayo.