1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri yazitaka nchi za Ulaya na Marekani kuzuia mali za Mubarak

15 Februari 2011

Misri imeziomba nchi za Ulaya na Marekani kuzizuia akiba za benki za aliekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak. Nchi kadhaa ikiwemo Ujerumani zimethibitisha zimelizipokea ombi hilo na zimeahidi kufanya uchunguzi.

https://p.dw.com/p/10HHQ
Rais wa zamani wa Misri, Hosni MubarakPicha: AP

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la Ujerumani DPA, Misri imetoa ombi kwa nchi za Umoja wa Ulaya la kuzizuia akiba za benki za aliekuwa rais nchi hiyo Hosni Mubarak.Shirika hilo limezinukulu duru za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya. Mawaziri wa Umoja huo leo watakutana kulijadili ombi hilo la Misri.

Ombi hilo limetolewa kwa Uingereza,Ujerumani na Ufaransa la kuzizuia fedha za viongozi wa ngazi za juu wa utawala wa Mubarak.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema nchi yake italizangatia ombi hilo na kwamba itachukua hatua madhubuti na za haraka endapo patapatikana ushahidi juu ya wizi wa fedha za serikali ya Misri.

Akizungumza bungeni waziri Hague alisema kuwa serikali ya Uingereza imepokea ombi kutoka kwa serikali ya Misri la kuzikamata mali za viongozi kadhaa waliokuwamo katika utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Aussenministertreffen in London Guido Westerwelle William Hague
Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle (Kulia), na William Hague wa UingerezaPicha: AP

Waziri Hague aliliarifu bunge kuwa Uingereza tayari imeshakua hatua kama hiyo kuhusiana na Tunisia baada ya rais wa nchi hiyo Zine El Abidine Ben Ali kupinduliwa na watu wake. Amehakikisha kwamba Uingereza itashirikiana na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya na washirika wake wa kimataifa katika kulitekeleza ombi la Misri.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya leo watakutana mjini Brussels kulijadili ombi la Misri, Na waziri Mkuu wa Luxemburg Jean-Claude Juncker amezitaka nchi za Umoja wa Ulaya ziige hatua iliyochukuliwa na Uswisi ya kuzizuia mali za Mubarak.

Ujerumani pia imesema kuwa imelipokea ombi la Misri la kuzitia kufuri akiba za benki za viongozi wa serikali na wabunge wa Misri waliokuwamo katika utawala wa Mubarak.

Lakini Uingereza ndiyo hasa ipo chini ya shinikizo la kuchukua hatua dhidi ya mali za Mubarak na familia yake kutokana namadai kwamba Mubarak na watu wake wameficha mamilioni ya fedha nchini Uingereza.

Mwandishi:Schauf Ralf
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri:Aboubakary Liongo