1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mitchell akutana na Netanyahu kwa mazungumzo ya mashariki ya kati.

Sekione Kitojo12 Oktoba 2009

Mjumbe wa Marekani katika mashariki ya kati George Mitchell amekutana na waziri mkuu wa Israel pamoja na rais wa Palestina Mahmoud Abbas katika juhudi za kufufua mazungumzo ya amani.

https://p.dw.com/p/K4kz
Mjumbe maalum wa Marekani George Mitchell, kushoto na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: AP

Mjumbe wa Marekani katika mashariki ya kati George Mitchell amekutana na waziri mkuu wa Israel tena jana Jumapili baada ya kwenda Misr kwa muda ikiwa ni sehemu ya jukumu lake kubwa la kuzirejesha Israel na Palestina katika meza ya majadiliano. Lakini hadi sasa hakuna dalili ya kupatikana njia ya kuwaleta pamoja viongozi wa pande hizo mbili.

Seneta huyo wa zamani wa Marekani alikutana kwa muda wa saa moja mjini Jerusalem na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, maafisa wamesema , baada ya mkutano mwingine tofauti siku ya Ijumaa na waziri mkuu huyo mpenda mabavu pamoja na rais wa Palestina Mahmoud Abbas. Ofisi ya Netanyahu imeeleza mwishoni mwa mkutano huo, ambao ulihudhuriwa pia na waziri wa ulinzi Ehud Barak , kwamba wasaidizi wawili waandamizi wa waziri mkuu watasafiri kwenda Marekani wiki hii kwa ajili ya mazungumzo zaidi.

Mitchell , ambaye hakuzungumza baada ya mkutano huo , hapo kabla aliwaambia waandishi habari mjini Cairo kuwa , mtu yeyote ambaye anaamini kuhusu amani anapaswa kuchukua jukumu kuchukua hatua kufikia lengo hilo.

Mitchell alifanya mazungumzo na mkuu wa kitengo cha ujasusi cha Misr Omar Suleiman siku ya Jumamosi pamoja na waziri wa mambo ya kigeni Ahmed Abul Gheit jana Jumapili kabla ya kurejea mjini Jerusalem kwa mazungumzo na Netanyahu kama sehemu ya ziara yake katika eneo hilo.

Rais wa Marekani Barack Obama , ambaye amepata tuzo ya amani ya Nobel , amesema kuwa waziri wa mambo ya kigeni Hillary Clinton ataripiti ifikapo katikati ya mwezi huu kuhusu juhudi za Mitchell za kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina yaliyositishwa tangu mwezi Desemba mwaka jana.

Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amedai kuwa Israel ifuate hatua za kuleta amani katika kile kinachoitwa road map na kusitisha shughuli zote za ujenzi wa makaazi ya Wayahudi katika ardhi ya Wapalestina. Akipinga mbinyo kutoka Marekani, Netanyahu ameahidi kuendelea na baadhi ya ujenzi wa makaazi katika eneo la ukingo wa magharibi na Jerusalem ya mashariki eneo linalokaliwa na Waarabu.

Mahmoud Abbas West Bank city Ramallah
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas,wakati akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni mjini Ramallah.Picha: AP

Wakati huo huo rais Mahmoud Abbas amekishambulia kikundi cha Hamas jana Jumapili kwa kuchelewesha hatua ya mapatano kati ya Wapalestina ambayo yalikuwa yatiwe saini mjini Cairo mwezi huu na kumaliza mivutano ya ndani.

Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni , amekishutumu chama cha Hamas , ambacho kinadhibiti eneo la Gaza kwa kutumia ripoti ya umoja wa mataifa inayozungumzia mashambulio ya Israel dhidi ya ukanda wa Gaza kuwa kama kisingizio cha kutoweza kutia saini makubaliano hayo.

Mwandishi Sekione Kitojo/RTRE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman