1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mitihani kwa Hollande wa Ufaransa

7 Mei 2012

Ufaransa imeamua, lakini katika ngazi ya Ulaya si mengi yatabadilika. Msoshalisti Francois Holland ametangaza kwamba anataka kufanya tena mashauriano juu ya mkataba wa Ulaya wa kuunusru uchumi.

https://p.dw.com/p/14rO6
Mshindi wa urais wa Ufaransa, Francois Hollande
Mshindi wa urais wa Ufaransa, Francois HollandePicha: Reuters

Kila mmoja katika Umoja wa Ulaya anataka uchumi upande. Kwa hivyo jambo hilo mtu anaweza kuliandika upya na kulitangaza ili liwe na msisimko kwa vyombo vya habari. Kikundi cha washauri wa rais mpya wa Ufaransa na wale wa serikali ya Ujerumani tayari vimeshakubaliana katika suala hilo. Hollande hataanza kipindi chake cha urais kwa kuwa na mabishano na Ujerumani. Kwa mtizamo wa siku nyingi zijazo, ushirikiano mzuri baina ya Ufaransa na Ujerumani ni jambo muhimu kwa Umoja wa Ulaya, bila ya kujali mitizamo ya kinadharia ya wale wanaotawala. Yawezekana kwamba baada ya miezi hivi Merkel na Holland wakauimarisha urafiki wao. Hiyo haitakuwa ndoa ya kimapenzi, lakini ni jambo muhimu katika ukweli halisi wa kisiasa. Kansela wa Ujerumani aliye na siasa za kihafidhina, bila ya shaka, atapatana na Francois Hollande, kwa vile tabia ya ukimya ya Hollande iko karibu zaidi na ile ya kansela , ukilinganisha na machachari ya Nicolas Sarkozy. Ufaransa na Ujerumani zitabakia kuwa ni injini ya Umoja wa Ulaya, japokuwa uhusiano huo hivi sasa mwanzoni una kigugumizi.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na aliyekuwa rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na aliyekuwa rais wa Ufaransa, Nicolas SarkozyPicha: picture-alliance/dpa

Hali pia haijawa vingine baina ya Merkel na Sarkozy. Hata Sarkozy katika miaka yake ya mwanzo madarakani mara kadha alibishana na Kansela. Alitaka kuachana kushirikiana sana na Ujerumani, na kuona bora ashirikiane kwa karibu zaidi na Uhispania. Alikuja na fikra ya kuwa na eneo la Bahari ya Mediterranean kushindana na Umoja wa Ulaya. Mpango huo ulishindwa. Ni katika majira ya mapukutiko ya mwaka 2010 ndipo urafiki wa kisiasa baina ya Angela Merkel na Francois Sarkozy ulipozaliwa, kama suluhisho la kupambana na mzozo wa madeni na wa sarafu ya Euro. Ilikuwa ni jambo la dharura katika siasa ya kuunusuru mfumo wa fedha wa Ulaya. Licha ya msimamo wa Bibi Merkel kubadilika mara kadha, lakini wakuu hao wawili kila wakati walionesha msimamo wa pamoja. Katika kampeni yake ya uchaguzi, Sarkozy aliitaja Ujerumani kama nchi ya kupigiwa mfano.

Rais msoshalisti Francois Hollande pia anayaona yako mazuri kutoka Ujerumani, lakini anakumbusha juu ya masuala ya misaada ya kijamii, na sio tu kushughulikia kusawazisha bajeti na kupunguza madeni ya serikali, kama vile seriklai ya mseto ya Wa-Conservative na waliberali inavojaribu kufanya mjini Berlin. Ukweli wa kiuchumi, hata hivyo, utamlazimisha Hollande mnamo wiki chache zijazo pia huko Ufaransa kuamrisha mkwiji ukazwe. Pindi yeye ataregeza katika ile ahadi alioitoa ya kupunguza madeni ya serikali, basi masoko ya fedha hayataistahamilia Ufaransa. Riba kwa ajili y a dhamana za mikopo ya Ufaransa zinaweza kupanda, na uaminifu wa Ufaransa kuweza kukopeshwa utapungua. Francois Hollande hatakuwa na nafasi kubwa ya kutimiza ahadi alizotoa katika kampeni ya uchaguzi. Nakisi ya bajeti mwaka 2011 ilikuwa asilimia tano. Si marekebisho ya mfumo wa pensheni wala kupunguza matumizi katika sekta ya serikali yatakayozuwia jambo hilo. Fedha kwa ajili ya kuupiga jeki uchumi au kupunguza kodi ya mauzo hazitakuweko; pia kodi itakayotozwa matajiri haitaleta fedha nyingi. Ukosefu wa ajira nchini Ufaransa ni mkubwa, na wapiga kura watampima Francois Hollande kama ataweza kupunguza idadi ya watu wasiokuwa na kazi. Hollande anaitaka Benki Kuu ya Ulaya ilio huru ijifugamanishe zaidi na suala la kukuwa uchumi, jambo ambalo kwa sasa linapingwa na serikali ya Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais mpya wa Ufaransa, Francois Hollande
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais mpya wa Ufaransa, Francois HollandePicha: picture-alliance/dpa

Na ikiwa Ugiriki baada ya uchaguzi wa jana haitokuwa na serikali madhubuti na kutumbukia katika mvurugano, basi nchi hiyo itabidi mwishowe huenda labda ikatoka katika eneo la sarafu ya Euro. Lakini Umoja wa sarafu ya Ulaya unaweza kustahamilia jambo hilo; lakini ikiwa Ufaransa itaingia zaidi katika mzozo wa madeni, basi sarafu ya Euro itakuwa ndio mwisho wake.

Ujerumani hivi sasa ndio nchi kubwa ya mwisho katika eneo la sarafu ya Euro ambayo kutokana na mzozo wa madeni haijawa na mabadiliko ya serikali. Mwaka 2013 Kansela Angela Merkel itabidi akabiliane na wapiga kura watakaomtaka ajielezee juu ya siasa yake ya kuunusuru uchumi wa Ulaya. Hana hakika kama nako Ujerumani hakutatokea mabadiliko ya serikali. Hata hivyo, tarakimu za kukuwa uchumi hapa Ujerumani ni bora kuliko sehemu nyingine za Ulaya, lakini jambo hilo linaweza kubadilika kwa haraka. Mzozo wa madeni bado kabisa haujesha.

Mwandishi: Riegert, Bernd/ Othman, Miraji/ZR

Mhariri. Mohammed Khelef