1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala juu ya msaada kwa Ugiriki Bungeni Ujerumani

4 Mei 2010

Obama :hatarini kupoteza hadhi yake ya kutetea mazingira ?

https://p.dw.com/p/NE2Q
Merkel asaka kitita cha kuisaidia Ugiriki ?Picha: AP

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo yamechambua mada mbali mbali tangu za ndani kama kuundwa motokaa zinazotumia umeme badala ya mafuta, lakini pia mada za nje, kama sheria inayotazamiwa kupitishwa bungeni ijumaa hii ya msaada wa fedha wa Ujerumani kuiokoa Ugiriki.

Hatua ya Rais Barack Obama ya kulitupia lawama Shirika la mafuta la BP kwa uchafuzi wa mazingira katika pwani ya Marekani ni mada nyengine. Gazeti la Saarbrücker Zeitung laandika:

"Kwamba sheria hiyo juu ya msaada wa dharura wa Ujerumani kwa Ugiriki ijumaa hii itapita, hakuna shaka yoyote. Kwani mwishoe, kwa jicho la kuonesha dhamana barani Ulaya, hakuna chama bungeni kinachoweza kukwepa kutoyapitisha mapendekezo ya msaada huo isipokuwa vyama vya mrengo wa shoto ambavyo vyabainika haviwezi kuachana na jaribio jengine la kujipigia debe kwa wananchi. Azma hapa ni kuimarisha sarafu ya Euro na Umoja wa Sarafu ya Ulaya, kwa jumla. Kwa bahati njema raia wengi wametambua hayo hivi sasa, hata ikiwa kutoa msaada wa mabilioni kadhaa wanakubali shingo upande."

Ama gazeti la Nordwest-Zeitung kutoka Oldenburg limeandika kwamba katika hali ya sasa ya kuyumbayumba kwa Euro, mara nyingi watu wanakumbuka enzi za D-Mark. Hapo inafanywa kana kwamba kurejea kutumika kwa sarafu hiyo ya Ujerumani ndio dawa pekee mujarab kwa maradhi ya sasa .Gazeti la ongeza:

"Kusema kweli hatua kama hiyo yaweza kuwa ni ya kujikomboa chini ya masharti fulani la sihivyo yaweza kuwa kujimbia binafsi kaburi. D-Mark hapo ingejikuta imepanda thamani mbele ya Euro au sarafu nyengine. Baadhi ya mabingwa wanasema kwa kiwango cha hadi 30%. Lakini bidhaa inazosafirisha nje Ujerumani zitapungua mno na viwanda vyake vitajikuta vinazorota. Hapo Ujerumani itajikuta kwenye mashaka makubwa zaidi yatakayoufanya msukosuko wa leo ni mchezo wa kitoto."

Gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung linadai kwamba Kanzela Merkel na serikali yake ya muungano wa vyama vya CDU/CSU na chama cha kiliberali cha FDP kwa msaada huo wa fedha inaoazimia kutoa kwa Ugiriki inakiuka kanuni za Umoja wa Ulaya na pengine hata na katiba ya fedha ya Ujerumani. Kisa hiki bila ya shaka kitafikishwa mahkama Kuu ya katiba mjini Karlsruhe. Ladai gazeti na linaongeza:

"........Hata Wagiriki binafsi waweza wakalitia munda jaribio la kuiwaokoa na kwa kufanya hivyo wakauporomoa pia chini Umoja wa Sarafu wa Ulaya. Na hicho kitakua kilele cha upumbavu."

Likitugeuzia mada, gazeti la Fuldaer Zeitung linachambua ajali ya kuvuja mafuta ya petroli katika kisima kimoja nje ya pwani ya Marekani. Gazeti limeandika:

"Rais Obama, amebainisha wazi wazi, dhahiri-shahiri, kuwa kampuni la mafuta la BP ,ndio dhamana wa ajali iliotokea. Amesema hivyo pengine kuwafunga mdomo waliomkosoa kwamba, hakuchukua hatua haraka kuukabili msiba huo.Yamkini pia, kuna kitu kilichobadilika mno kimsingi, katika uhusiano kati ya serikali ya Marekani na kampuni hilo la mafuta ambalo , shughuli zake zaonekana sasa zimepitwa na wakati."

Ama Nordbayerischer Kurier, laandika kwamba ni Obama mwenyewe alieidhinisha kuchimbwa mafuta katika pwani nyeti ya Alaska. Alikuwa na shabaha kuwaridhisha wabunge wapingao ulinzi wa mazingira katika bunge la Marekani ili waunge mkono mapatano ya hifadhi ya mazingira ya ulimwengu. Sasa lakini,laandika gazeti:

"Anapaswa Obama kujiuliza: jinsi gani atampunga shetani huyo. Heba ya Obama kama mtunzaji mazingira , inatishia kuzama katika tundu la kuchimba mafuta linalovuja baharini."

Mwishowe, gazeti la Schweriner Volkszeitung, linauchambua uamizi wa kocha wa Taifa wa Ujerumani wa kutomchagua mshambulizi wa timu ya Schalke, alietia mabao mengi msimu huu, Kevin Kuranyi, kwa Kombe lijalo la dunia, Afrika Kusini:

"Kocha Löw amefichua siri hadharani na yabainika hakumsamehe Kuranyi kwa madhambi alioyafanya .Amempiga kumbo nje ya Kombe la dunia. Amedai mkasa wa Oktoba 2008 alipokorofishana na Kuranyi,hatahivyo, haukuwa sababu ya uamzi wake, bali ni mkakati wa mchezo alioupanga. Kocha Löw, amepanga mkakati wa mshambulizi 1 tu usoni na kwa mkakati huo, anahisi mshambulizi wa sasa wa Bayern Munich, Miroslav Klose, ndie anaefaa.Wengine wenye turufu ya kuchaguliwa, ni Gomez, Kiessling na jogoo chipukizi, Müller."

Mwandishi: Ramadhan Ali /DPA

Uhariri: Miraji Othman