1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala kuhusu katiba mpya Uturuki

Sekione Kitojo
9 Januari 2017

Bunge la Uturuki leo limeanza kujadili mswada wa katiba mpya yenye utata wenye lengo la kupanua madaraka ya rais ya rais Erdogan, ambao unatarajiwa kufanyiwa kura ya maoni ifikapo mwezi wa Machi.

https://p.dw.com/p/2VX4B
Türkei Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Ozer

Katiba  hiyo  mpya , ambayo  itakuwa  badala  ya  sheria  mama iliyotungwa  baada  ya  mapinduzi  ya  kijeshi  nchini  Uturuki  mwaka 1980, inataka  kuweka  kwa  mara  ya  kwanza  mfumo  wa  kirais kwa  ajili  ya  kuliongoza  taifa  hilo  la  kisasa  lililoundwa  kutokana na  mabaki  ya  himaya  ya  Ottoman.

Wakosoaji  wamedai  kwamba  hatua  hiyo  ni  sehemu  ya  uporaji wa  madaraka  unaofanywa  na  Rais Recep Tayyip Erdogan -- waziri  mkuu  wa  Uturuki kuanzia  mwaka  2003  hadi  2014  na  baadaye  rais , na  kuiingiza nchi  hiyo  katika  utawala  wa  mtu  mmoja  baada  ya  jaribio lililoshindwa  la  mapinduzi  Julai  mwaka  jana.

Türkei | Polizei blockiert Straße um Proteste vor dem Parlament gegen die Verfassungsänderung zu verhindern
Polisi wa kuzuwia ghasia wakiwazuwia waandamanaji kufika katika jengo la bungePicha: Reuters/U. Bektas

Lakini Erdogan  na  chama  chake  tawala  cha  Justice  and Development AKP wanasema  mfumo  wa   kirais  utaiweka  Uturuki katika  njia  moja  na  mataifa  mengine  kama  Ufaransa  na Marekani  na   unahitajika  kwa  ajili  ya  serikali  yenye  ufanisi.

Mjadala  huo  kuhusiana  na  katiba  hiyo  mpya  yenye sura 18 ulianza  baada ya mswada  huo  kukubaliwa  na  tume  ya  bunge. Uwasilishaji  wa  mswada  huo  mara  mbili  unatarajiwa  kukamilika mnamo  siku  13  hadi  15.

Waandamanaji

Kundi  dogo  la  waandamanaji  lilijitokeza  nje  ya  jengo  la  bunge mjini  Ankara  kabla  ya  mjadala  wenyewe , lakini  polisi  walivunja maandamano  hayo  wakitumia   maji  ya  pilipili  dhidi  ya waandamanaji.

Türkei | Polizei blockiert Straße um Proteste vor dem Parlament gegen die Verfassungsänderung zu verhindern
Waandamanaji wakijaribu kupita vizuwizi vya polisi wa kuzuwia ghasiaPicha: Reuters/U. Bektas

Mmoja  kati  ya  waandamanaji  alilalamika  baada  ya  polisi kulitawanya  kundi  lao kwa  mabomu  ya  kutoa  machozi.

"Uturuki  imevamiwa. wale  wanaohusika  na  miripuko, mapambano, silaha  ni  wale walioko  madarakani hii  leo. Kwa  nini  kunakuwa  na ulinzi  kiasi  hiki, kuna  vita  vinavyoendelea  hapa? Nataka  kupita vizuwizi  na  kwenda  mbele  ya  bunge  lakini  polisi  hawataki kuniruhusu, wamejazana  hapa. Kitu  gani  kinatokea  katika  nchi hii? Je  kuna  vita  vya  wenyewe  kwa  wenyewe?"

Chama  cha  AKP  kinahitaji  zaidi  ya  kura  330 , tatu  ya  tano  ya wingi  kwa  ajili  ya  mswada  huo  kuweza  kufikishwa  katika  kura ya  maoni ili  kuidhinishwa  na  wapiga  kura.

Türkei verlängert Ausnahmezustand - Yildirim
Waziri mkuu Binali Yildirim akiwahutubia wabunge katika bunge la Uturuki Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Katiba  hiyo  mpya  inapingwa  na  chama  kikuu  cha  upinzani , chama  cha  Republican Peoples Party CHP, ambacho  naibu mwenyekiti  wake  Bulent Zezcan  alisema  itapeleka  madaraka ikulu , yaliyochukuliwa  kutoka  Sultan  wa  enzi  za  Ottoman  karne moja  iliyopita.

Wakati  huo  huo  rais Erdogan  amesema  leo kwamba  anaamini mjadala  kuhusu  Uturuki  na  Marekani  utashika  kasi  baada  ya rais  mteule  Donald  Trump  kuingia  madarakani  na  kwamba amjadiliano  hayo  yatafikia  muafaka  katika  masuala  ya  kikanda. Uhusiano  kati  ya  Marekani  na  Uturuki , washirika  muhimu  katika mapambano  ya NATO  dhidi  ya  kundi  la  Dola  la  Kiislamu  nchini Syria  na  Iraq wameporomoka  kwa  kiasi  kikubwa  tangu  jaribio lililoshindwa  la  mapinduzi  ya  kijeshi  Julai  mwaka  jana.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe

Mahariri: Yusuf  , Saumu