1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjane wa rais wa zamani wa Rwanda Habyarimana akamatwa mjini Paris

Oumilkher Hamidou2 Machi 2010

Eti kweli maafisa wa Ufaransa watamrejesha Kigali bibi Agathe Habyarimana?

https://p.dw.com/p/MHwI
Rais Nicolas Sarkosy alipokutana na rais Kagame mjini Kigali mwezi uliopitaPicha: AP

Mjane wa rais wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, anaetuhumiwa kuhusika na mauwaji ya halaiki ya mwaka 1994, amekamatwa hii leo nchini Ufaransa, siku chache baada ya ziara ya rais Nicolas Sarkozy nchini Rwanda.

Akikamatwa kusini mwa mji mkuu, Paris, Agathe Habyarimana alikua akisakwa kwa waranti wa kimataifa wa vyombo vya sheria vya Rwanda tangu october mwaka jana, na kuandamwa pia na ofisi ya mwanasheria mkuu wa Paris.

Kuuwawa Juvénal Habyarimana mnamo mwaka 1994 ndio chanzo, inasemekana, cha mauwaji ya halaiki yaliyogharimu maisha ya watu wasiopungua laki nane. Na mkewe anatuhumiwa kua miongoni mwa waasisi wa mauwaji hayo ya halaiki.

Akifanya ziara ya suluhu mjini Kigali, February 25 iliyopita, rais Nicolas Sarkozy alikiri kwamba Ufaransa ilifanya "makosa makubwa ya tathmini" wakati wa mauwaji ya halaiki nchini Rwanda.Lakini hakufika umbali wa kuomba radhi.

Hata hivyo,alipokua pamoja na rais Paul Kagame wa Rwanda, Nicolas Sarkozi alitoa taarifa zinazochukua sura nyengine kabisa hii leo.

"Tunataka wenye kubeba dhamana ya mauwaji ya halaiki wakamatwe na watiwe adabu" alisema, na kujiuliza tunanukuu:Kwani wapo nchini Ufaransa? Vyombo vya sheria vitafafanua."Mwisho wa kumnukuu.

Bibi Agathe Habyarimana, anaeshikiliwa katika kituo cha polisi cha Versaille, aliondoka Rwanda siku tatu baada ya shambulio la april 6 mwaka 1994 dhidi ya ndege aliyokua akisafiria mumewe,iliyodenguliwa kwa makombora ilipokua ikituwa mjini Kigali.

Alikua baadae awekwe kizuwizini akisubiri kurejeshwa Rwanda ambayo inatazamiwa kuwasilisha maombi rasmi na ushahidi wa tuhuma dhidi yake.

Korti ya rufaa ya Paris itabidi iidhinishe maombi ya kumrejesha Rwanda yatakayotekelezwa baada ya waziri mkuu kutia saini waraka maalum. Utaratibui wote huo unaweza kudumu miezi kadhaa.

Duru za mahakama zinasema, hata hivyo, uwezekano wa kumrejesha nyumbani mjane huyo wa rais wa zamani wa Rwanda, Agathe Habyarimana, si mkubwa hivyo.

Hata kama Rwanda imepiga marufuku adhabu ya kifo, masharti ya kuwashikilia watu jela yanatajwaa kua "hayalingani na vipimo vya nchi za Ulaya-hoja ambayo, kwa mujibu wa wadadisi, inaweza kuzuwia asirejeshwe nyumbani.

Utaratibu huu wa kumrejesha nyumbani bibi Agathe Habyarimana hauhusiani na mashtaka ya mashirika yanayotetea masilahi ya wahanga wa mauwaji ya halaiki yanayomutuhumu kuchangia katika mauwaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinaadam.

Pindi utaratibu wa kumrejesha nyumbani ukishindwa, vyombo vya sheria vya Ufaransa vinaweza kumuandama bibi Agatha Habyarimana kwa misingi ya sheria za kimataifa, kama yanavyopendekeza mashirika yanayopigania haki za binaadam.

Itafaa kusema hapa kwamba maombi ya ukimbizi ya bibi Agathe Habyarimana yalikataaliwa na vyombo vya sheria vya Ufaransa mwezi October mwaka jana.