1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Bor wakombolewa

18 Januari 2014

Vikosi vya serikali ya Sudan Kusini vimeukomboa tena mji muhimu wa Bor kwa kuwashinda maelfu ya wanajeshi wa waasi leo Jumamosi.(18.01.2014).

https://p.dw.com/p/1AtBz
Vikosi vya serikali ya Sudan Kusini.
Vikosi vya serikali ya Sudan Kusini.Picha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Msemaji wa jeshi la serikali Philip Aguer amewaambia waandishi wa habari vikosi vya kishujaa vya SPLA vimeingia Bor na kuwashinda zaidi ya wanajeshi 15,000 wa kiongozi wa waasi Riek Machar na kwa hiyo kutibua mipango yake ya kuishambulia Juba.

Bor ni mji mkuu wa jimbo la Jonglei na uko kama kilomita 200 kaskazini mwa mji mkuu wa Sudan Kusini Juba.Mji huo umekuwa chini ya mikono tafauti mara nne tokea kuibuka kwa mzozo huo katika taifa hilo changa kabisa duniani wiki tano zilizopita.

Ateny Wek Ateny msemaji wa Rais Salva Kiir amesema vikosi hivyo vya serikali vimepongezwa kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Sheria ya kimataifa kuheshimiwa

Pia amesema Jeshi la Ukombozi la Watu wa Sudan Kusini SPLA litazingatia utawala wa sheria ya kimataifa ikiwa ni siku moja baada ya mjumbe wa masuala ya haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa kuripoti kwamba mzozo huo umekumbwa na mauaji makubwa, mauaji ya kiholela,uharibifu mkubwa na uporaji.

Wanajeshi wa serikali katika doria mjini Juba.
Wanajeshi wa serikali katika doria mjini Juba.Picha: picture-alliance/dpa

Msemaji huyo ameongeza kusema iwapo kuna watu wataochukuliwa mateka watashikiliwa kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana wakati wa kukamilisha ziara yake ya wiki moja nchini Sudan Kusini Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Masuala ya Haki za Binaadamu Ivan Simonovic amesema mbali ya kuwepo kwa ukiukaji wa haki za binaadamu na uhalifu dhidi ya ubinaadamu pia kuna uhalifu wa kivita unaotendeka.

Askari watoto

Simonovic amesema kuna ripoti za kujumuishwa kwa wapiganaji kadhaa watoto katika kikosi cha wanamgambo kinachojulikana kama Jeshi Jeupe huko Jonglei ambalo linapambana kumuunga mkono Machar.

Mwanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini mjini Bor.
Mwanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini mjini Bor.Picha: Reuters

Mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekwama mjini Addis Ababa Ethiopia kutokana na kuwepo kwa mvutano kati ya viongozi wa serikali na waasi wanaodai kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa. Mataifa yalioko katika kanda hiyo tayari yameanza kutumbukia kwenye mzozo huo ambapo vikosi vya Uganda vimeanza kupambana bega kwa bega na vikosi vya serikali.

Machar ashutumu nchi za kanda

Waraka wa siri kutoka wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ulioonekana na shirika la habari la AFP umesema kwamba Machar amedai ndege za kivita za Uganda zilijaribu kushambulia kwa mabomu mahala alimokuwa amejificha huko Jonglei. Machar pia ameshutumu vikali pendekezo la serikali ya Sudan kutowa vikosi vyake kulinda visima vya mafuta vya iliokuwa adui yake wa zamani Sudan Kusini hasa kwa kuzingatia kwamba nchi hiyo ni mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Maendeleo ya kanda IGAD ambayo iko mbioni kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo.

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar.
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar.Picha: Al-Haj/AFP/Getty Images

Hata hivyo serikali ya Sudan Kusini imesisitiza kwamba ina matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ya amani nchini Ethioipia katika mazungumzo yanayosimamiwa na IGAD ambapo Uganda pia ni mwanachama muhimu wakati waasi wakielezea wasi wasi wao juu ya msimamo wa nchi hiyo kutopendelea upande wowote.

Umoja wa Ulaya hapo jana umesema inatowa euro milioni 1.1 kusaidia mazungumzo hayo ya IGAD kuzuwiya Sudan Kusini isitumbukie kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mkimbizi kutoka mji wa Bor na mwanawe.
Mkimbizi kutoka mji wa Bor na mwanawe.Picha: picture-alliance/AP

Watu wanaofikia 10,000 inaaminika kuwa wameuwawa hadi sasa katika mapigano kati ya vikosi vilivyo tiifu kwa Rais Kiir dhidi ya muungano wa wanajeshi walioasi na wanamgambo wa kikabila wanaoongozwa na Machar.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu 468,000 wameyakimbia makaazi yao tokea kuzuka kwa umwagaji damu uliogeuka kuwa mauaji ya kikabila kati ya watu wa kabila la Kiir la Dinka ambalo ndio kabila kubwa na kabila la Nuer la Machar.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Caro Robi