1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Cape Town wakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji

Sylvia Mwehozi
18 Januari 2018

Mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini umetangaza hatua mpya za kubana matumizi ya maji ili kukabiliana na ukame.

https://p.dw.com/p/2r73Q
Südafrika Wassermangel |
Picha: Getty Images/AFP/R. Bosch

Meya wa jiji la Cape Town Patricia de Lille,  amesema mwezi ujao watalazimika kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 40, na kuruhusu lita 50 kwa mtu mmoja kwa siku, wakati jiji hilo likikabiliana na hali mbaya zaidi ya ukame kuwahi kuukumba katika karne hii.

Meya de Lile ameonya kwamba kama mvua hazitanyesha na jitihada za kupunguza matumizi ya maji hazitafanikiwa, basi usambazaji maji ya kawaida utafungwa.

Badala yake wakazi wa Cape Town watalazimika kupanga foleni kwenye vituo vya mabomba ya maji kwa mgao wa maji ambapo kila mtu ataruhusiwa kupata lita 25 za maji kwa siku. 

Meya de Lile amesema wamefikia hatua hiyo baada ya kuwaeleza wananchi kutumia maji vizuri lakini hali bado majibu yamekuwa siyo ya kuridhisha,  na sasa watachukua hatua ya kuwalazimisha.

Jiji hilo ambalo huvutia mamilioni ya watalii kila mwaka, limeimarisha udhibiti mkubwa wa taka ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku umwagaji wa maji kwenye mabwawa ya manispaa na kuwapeleka mahakamani wamiliki wa nyumba wanaofuja maji.

Mwandishi. Sylvia Mwehozi/afpe.

Mhariri: Daniel Gakuba