1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wa Ramadi wadhibitiwa na Dola la Kiislamu

18 Mei 2015

Kundi la Dola la Kiislamu limetangaza limeudhibiti kikamilifu mji wa Ramadi wakati wanajeshi wa Iraq wakiripotiwa kuukimbia mji huo mkuu wa mkoa wa Anbar. Marekani inasita kuthibitisha kutekwa kwa mji huo.

https://p.dw.com/p/1FRAo
Irak IS erobert Ramadi
Picha: Reuters/Stringer

Wanajeshi wa Iraq walionekana wakiukimbia mji wa Ramadi wakiziacha silaha zao na magari yasiyoweza kutobolewa na risasi, katika kile kinachoonekana kuwa pigo kubwa la kushindwa vita dhidi ya Dola la Kiislamu licha ya ongezeko la mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Maiti zilionekana zimezagaa katika barabara za mji huo, baadhi zikiwa zimechomwa moto, huku maafisa wakiripoti kwamba wanamgambo wa kundi hilo walifanya mauaji ya kiholela ya wanajeshi wa Iraq na raia.

"Mji wa Ramadi umeanguka. Mji umedhibitiwa kabisa na jeshi linakimbia," alisema Muhannad Haimour, msemaji wa gavana wa mkoa wa Anbar.

"Tunakaribisha kundi lolote wakiwemo waasi wa kishia, waje watusaidie kuukomboa mji wetu kutoka mikononi mwa wanamgambo. Kilichotokea leo ni hasara kubwa iliyosababishwa na jeshi kushindwa kujipanga vizuri," alisema Naeem al Gououd, kiongozi wa ukoo wa madhehebu ya Sunni wakati alipozungumza na shirika la habari la Associated Press.

Irak IS erobert Ramadi
Mwanamume wa Kisunni akimsukuma mama mlemavu nje ya BaghdadPicha: Reuters/Stringer

Gavana wa mkoa wa Anbar, Suhaib al Rawi, alisema anadhani harakati ya kijeshi inayofanywa na jeshi la Marekani ni hatua nzuri ya kuelekea kulishinda kundi la Dola la Kiislamu. "Operesheni yoyote ya maana inayofanywa na vikosi vya muungano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu itakuwa na matokeo mazuri. Kundi hili halitishii tu usalama wa Iraq na Syria bali pia usalama wa ulimwengu mzima. Tunahitaji operesheni za namna hii, zinazotoa ishara kwamba muungano wa kimataifa umejizatiti kuyashinda makundi ya kigaidi yanayotishia sio tu mkoa wa Anbar, Iraq na Syria bali dunia nzima."

Wakaazi wakimbia Ramadi

Mamia ya wakazi wa Ramadi waliukimbia mji huo siku ya Jumamosi wakihofia mashambulizi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu lakini wakanyimwa ruhusa ya kuingia Baghdad na mikoa mingine na wanajeshi wa Iraq kwa sababu za kiusalama. Wakazi hao sasa wamekwama karibu na daraja la Bzibiz, kiasi kilometa 65 kutoka mji mkuu Baghdad na hawaruhusiwi kuvuka mto wa Euphrates kuelekea mji huo.

Um Mohammed, ambaye ni miongoni mwa wakaazi waliokwama, alisema hali ilikuwa ngumu Ramadi. "Vurugu, machafuko na hofu vimeenea katika barabara za Ramadi. Makombora na mabomu yalianguka kiholela kwa nyumba. Kuna ripoti mpya kwamba familia nyingi zimeuwawa. Wanawake walionekana wakikimbia mabarabarani."

Irak Anbar Provinz Flüchtlinge IS-Opfer
Wakimbizi wa Iraq mkoani AnbarPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Kadim

Huku akikaribia kushindwa, waziri mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, aliamuru wanajeshi wasiondoke maeneo yao katika maeneo yote ya mkoa wa Anbar, akihofia wapiganaji wanaweza kuliteka eneo zima la jangwa lilishohudia mapigano makali baada ya uvamizi wa Iraq mnamo mwaka 2003 ulioongozwa na Marekani ambao ulimuangusha kiongozi wa zamani wa Iraq, hayati Saddam Hussein.

Marekani yafuatilia matukio ya Ramadi

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema inaendelea kufuatilia ripoti za mapigano yanayoendelea mjini humo, huku ikikiri wanamgambo wa kundi hilo wanaonekana kuwa na nguvu zaidi katika makabiliano yanayoendelea. Msemaji wa wizara hiyo Maureen Schumann amesema ni mapema mno kutoa kauli kuthibitisha kinachoendelea Ramadi kwa sasa, lakini hata kama mji huo utaanguka mikononi mwa Dola la Kiislamu, muungano unaoongozwa na Marekani utawasaidia wanajeshi wa Iraq kuukomboa.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alisema bado ana imani na vita dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu. Akiwa katika ziara nchini Korea Kusini, Kerry amesisitiza vita dhidi ya kundi hilo vitakuwa vigumu na virefu katika mkoa wa Anbar, ambako wanajeshi wa Iraq hawajakuwa imara.

Makundi ya waasi wa Kishia yamekusanyika mjini Ramadi mapema leo kuvisaidia vikosi vya Iraq kujaribu kuukomboa mji wa Ramadi.

Mwandishi:Josephat Charo/AP/AFP

Mhariri:Daniel Gakuba