1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji wateketezwa jimbo la Darfur

P.Martin8 Oktoba 2007

Serikali ya Sudan inazidi kushinikizwa baada ya Umoja wa Mataifa hii leo kutuma ujumbe wake wa pili katika mji wa Haskanita,uliotiwa moto katika jimbo la Darfur.

https://p.dw.com/p/C7iN

Msemaji wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Sudan,Khartoum leo amethibitisha kuwa mji mzima umeteketezwa isipokuwa msikiti na shule moja.

Tume ya mwanzo ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika,iliyotembelea mji wa Haskanita siku ya Jumamosi,imethibitisha kuwa mji huo unaodhibitiwa na serikali ya Khartoum,umechomwa moto na wakaazi wake wameuhama mji.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa,zaidi ya wakaazi 7,000 wa Haskanita wameukimbia mji huo na sasa kunahitajiwa operesheni kubwa ya msaada kuwapatia wakaazi hao chakula,maji na mahala pa kuishi.

Inasemekana kuwa shambulizi hilo linalipiza kisasi shambulizi lililofanywa Septemba 29 dhidi ya vikosi vya amani vya Umoja wa Afrika.Wanajeshi 7 wa Nigeria na 3 kutoka Mali,Senegal na Botswana waliuawa katika shambulizi hilo.

Kwa mujibu wa msemaji wa kundi la waasi wa Darfur SLA,watu wasiopungua 100 wameuawa katika mji wa Haskanita.Suleiman Jamous,ameilaumu serikali ya Sudan kwa uteketezaji wa mji huo.Lakini waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Lam Akol amekanusha tuhuma hizo.

Kwa upande mwingine,taarifa iliyotolewa na maafisa wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumapili haikusema nani alieutia moto mji wa Haskanita, lakini imeeleza kuwa majeshi ya serikali ya Sudan yaliudhibiti mji huo baada ya kituo cha vikosi vya Umoja wa Afrika kushambuliwa juma moja lililopita.

Hapo awali,mji wa Haskanita ulikuwa ukidhibitiwa na waasi wanaodhaniwa kuwa ndio walihusika na shambulizi la Septemba 29 dhidi ya vikosi vya Umoja wa Afrika.Hilo ni shambulizi baya kabisa kupata kutokea tangu ujumbe wa Umoja wa Afrika kupelekwa Darfur mwaka 2004.Umoja huo ungali ukifanya uchunguzi wa shambulizi hilo na serikali ya Sudan imeombwa kulilinda eneo hilo.Kwa hivyo hakuna wasimamizi wa kimataifa katika eneo linaloshuhudia mapambano kati ya jeshi la serikali na waasi.

Mgogoro wa Darfur,magharibi mwa Sudan unaokaribia kutimiza miaka mitano,umepoteza maisha ya zaidi ya watu 200,000 na wengine wapatao milioni 2.5 wamelazimika kuondoka makwao.