1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa China Sudan

28 Februari 2008

Mjumbe maalumu wa China nchini Sudan amemaliza jana ziara yake ya 4 nchini Sudan na amesema hakuna tena pingamizi ya kuwekwa vikosi vya kimataifa.

https://p.dw.com/p/DF1T

Mjumbe maalumu wa Jamhuri ya watu wa China aliemaliza ziara yake nchini Sudan hivi punde,amesema hali ya mambo mkoani Dafur -magharibi mwa Sudan itatengenea.Kuwekwa huko vikosi vya kuhifadhi amani vya kimataifa kimsingi, hakuna pingamizi . Kambi ya magharibi lakini, inabidi kuchangia zaidi katika suluhisho la kisiasa.

Mjumbe maalumu wa China kwa Sudan, amekamilisha ziara yake ya 4 nchini Sudan na kwa jicho la Beijing hakuna kipingamizi tena cha kuwekwa mkoani Dafur kwa vikosi vya kuhifadhi amani vya kimataifa .Mjumbe wa China Liu Guijin akaitaka jamii ya kimataifa kuimarisha juhudi zake ili kufanya hali mkoani Dafur kutengenea.

Miongoni mwa juhudi hizo ni kuwashinikiza waasi ili warejee nao katika meza ya mazungumzo pamoja na serikali ya Khartoum.Isitoshe, mjumbe wa China amehimiza mchango wa nchi za kiafrika ambazo zapaswa kushika usukani katika kikosi cha mchanganyiko wa askari wa UM na wa Umoja wa Afrika (AU). Liu akasema,

"Hadi sasa , hakuna hata moja kati ya nchi kubwa za kiafrika iliotekeleza ahadi yake kupeleka Sudan vikosi vyake.Pengine, nchi hizo za kiafrika zina matatizo ya kiufundi,pengine hazina silaha za kutosha.Lakini, jamii ya kimataifa imeyatambua mno matatizo hayo na itazisaidia nchi hizo kutimiza ahadi zao."

Mjumbe huyo wa China Liu Gujin alieleza ziara yake ya siku 3 nchini Sudan iliofanikiwa.Liu alipongeza kazi ya wanajeshi 140 wa kichina waliopo Dafur kuhifadhi amani.

Liu akasisitiza kwamba hakuna kipingamizi tena kinachozuwia kuwekwa Dafur vikosi vya kimataifa.Katika jumla ya askari 26,000 waliopangwa kupelekwa Dafur, ni mia kadhaa tu waliowasili huko hadi sasa.

Mjumbe huyu wa China hatahivyo,amepongeza juhudi za serikali ya Sudan na akasisitiza juu ya usuhuba mkubwa baina ya Beijing na Khartoum. Siku za nyuma China ,ikitumia tena na tena kura yake ya turufu kuzima vikwazo vikali vilivyolengwa dhidi ya serikali ya Sudan katika Baraza la Usalama la UM .

Liu akasema nchi yake China, kimsingi inapinga aina yoyote ile ya vikwazo dhidi ya mshirika wake Sudan.

Akawaambia maripota jana mjini Khartoum:

"Tutaendelea kuishawishi serikali ya Sudan ishirikiane, lakini wakati huo huo, Jamii ya kimataifa inabidi na hasa marafiki zetu katika baraza la Usalama la UM ,kutekeleza sehemu ya jukumu lao.Hatuwezi tu kuzungumzia swali la kuwekwa kwa vikosi,i utaratibu wa kisiasa pia una uzito wake ."

Mjumbe wa China akaongeza kusema kwamba, bila ya suluhisho la kisiasa kutazuka mapigano mapya nchini Sudan mara tu vikosi vya kimataifa vimeondoka nchini.Akavitaka vikundi vya waasi kukaa katika meza ya mazungumzo na akazishauri nchi za magharibi kuvishinikiza zaidi vikundi vya waasi vilipo uhamishoni nje ya nchi kuridhia mazungumzo.

Mmoja kati ya viongozi mashuhuri wa vikundi vya waasi aliopo Paris, Ufaransa anapinga moja kwa moja mazungumzo.

Wiki hii imetimu miaka 5 tangu mgogoro wa dafur kuripuka ambamo si chini ya watu robo-milioni wamepoteza maisha.