1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjumbe wa U. Mataifa kukutana na Kiongozi wa Kijeshi wa Myanmar Jumanne

Tuma Provian Dandi1 Oktoba 2007

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bwana Ibrahim Gambari aliyetumwa nchini Myanmar kushughulikia mzozo wa kisiasa unaoikabili serikali ya kijeshi ya nchi hiyo, ameambiwa kukutana na mkuu wa kijeshi Thna Shwe hapo kesho

https://p.dw.com/p/CH7O
Maandamano dhidi ya serikali ya Myanmar mjini Berlin, Ujerumani
Maandamano dhidi ya serikali ya Myanmar mjini Berlin, UjerumaniPicha: AP

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bwana Ibrahim Gambari atalazimika kusubiri hadi hapo kesho atakapokutana na kiongozi mkuu wa serikali ya kijeshi ya Myanmar Bwana Than Shwe.

Badala ya kukutana na kiongozi mkuu wa nchi hiyo kama ilivyokuwa imepangwa, Bwana Gambari amepelekwa katika mji wa Naypyidaw kulikokuwa na warsha nyingine za kisiasa.

Tangu alipowasili nchini Myanmar siku mbili zilizopita, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Bwana Ibrahim Gambari amekuwa na mazungumzo na kiongozi wa kambi ya upinzani Bi Aung San Suu Kyi, na maofisa wa Serikali ya kijeshi ya nchi hiyo.

Baadhi ya watu aliokutana nao ni Kaimu Waziri Mkuu Bwana Khin Aung Nyint na Waziri wa Habari Bwana Kway San.

Uongozi wa kijeshi wa Myanmar haukuwa tayari kueleza sababu ya kumpeleka Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kwenye mkutano uliohusu ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Asia, badala ya kumpeleka kwa Kiongozi mkuu wa utawala wa Kijeshi Than Shwe.

Serikali hiyo ya Kijeshi inayosemekana kutokuwa wazi kwa wananchi wake imekuwa ikikumbwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Jumuiya ya kimataifa, ikiwemo vikwazo kadhaa vilivyopitishwa na Umoja wa Mataifa.

Licha ya kusababisha vifo vya watu 13 na mamia ya majeruhi, maandamano yaliyoanzishwa na watawa wa kibudha kwa amani, yanaelezwa kuwa makubwa ambayo hajawahi kutokea katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Lengo la maandamano hayo linaelezwa kwamba ni kupinga utawala wa kijeshi kwa kuwa hauzitangii haki za binadamu na demokrasia.

Askari wa kijeshi wakiwa na silaha nzito wameendelea kuonekana kwenye mitaa mbalimbali zikiwemo nyumba za kuabudia, na taarifa zinaelezwa kwamba wamefanikiwa kutuliza maandamano hayo yaliyodumu kwa kipindi cha siku nne mfululizo.

Mashirika yanayojihusisha na haki za binadamu bado yanaendelea kufuatilia kwa karibu ili kufahamu ni idadi ya watu wangapi waliokamatwa kutokana na maandamano hayo.

Hata hivyo takwimu za awali zilizotolewa na Shirika moja la Thailand linalojihusisha na msaada kwa wafungwa, limesema kwamba karibu watu elfu 1 na mia 5 tayari wamekamatwa na kuwekwa ndani tangu wiki iliyopita.

Shirika hili ambalo kwa kifupi linaitwa AAPP limefafanua kwamba waratibu wengi wa maandamano hayo wamekamatwa, wakiwemo mabudha elfu 1, wanafunzi wapatao 400 pamoja na wanaharakati wengine.

Kutokana na ulinzi mkali wa vikosi vya serikali, baadhi ya maduka ya shule zimefunguliwa na kuanza masomo ikiwemo kuruhusu mabasi ya abiria ili kuwawezesha watu kwenda kwenye shughuli zao za kila siku.

Wakati ujumbe wa Umoja wa Mataifa ukiwa nchini Myanmar, pia Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Mitoji Yabunaka yuko nchini humo kwa ajili ya kufuatilia kifo cha mwandisi wa habari wa Japan Kenji Nagai aliyeuawa na majeshi ya Myanmar.