1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkasa wa Rüttgers ni pigo kwa Merkel

23 Februari 2010

Mwanachama mwandamizi wa CDU katika mkoa wa Ujerumani wa North Rhine Westphalia,amejiuzulu baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa wafadhili walitozwa fedha ili kuweza kuonana na Waziri Mkuu wa mkoa huo Jürgen Rüttgers.

https://p.dw.com/p/M9S1
ARCHIV - Der nordrhein-westfaelische Ministerpraesident Juergen Ruettgers spricht am 6. September 2009 waehrend der Auftaktveranstaltung der CDU fuer die Bundestagswahl zu ihren Parteimitgliedern Zwischen Ministerpraesidenten der CDU und dem Berliner Koalitionspartner FDP bahnt sich ein neuer Streit ueber die ab 2011 geplanten weiteren Steuersenkungen an. Im Gespraech mit der Nachrichtenagentur DAPD aeusserten sich die Regierungschefs Roland Koch, Juergen Ruettgers und Christian Wulff zurueckhaltend zu deren Umfang und warnten vor einer fruehzeitigen Festlegung auf bestimmte Summen. (AP Photo/Roberto Pfeil, Archiv) ** zu APD0145 ** --- FILE - North Rhine-Westfalia's state governor Juergen Ruettgers talks to Christian Democratic party members during the official start of their election campaign for upcoming German federal elections at the end of the month in Duesseldorf, Germany, Sept. 6, 2009. (AP Photo/Roberto Pfeil)
Waziri Mkuu wa Mkoa wa North Rhine Westphalia, Jürgen Rüttgers.Picha: AP

Kashfa hiyo ni pigo kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwani katika mwezi wa Mei, chama chake cha CDU kitagombea uchaguzi kwenye mkoa wa North Rhine Westphalia. Huo utakuwa mtihani wa kwanza kwa CDU tangu Merkel alipounda serikali ya muungano pamoja na chama cha kiliberali cha FDP Oktoba iliyopita. Katibu Mkuu wa chama cha CDU katika mkoa wa North Rhine Westphalia, Hendrik Wüst amesema, yeye anajiuzulu kwa sababu hataki kuhatarisha uwezekano wa Jürgen Rüttgers kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Mei ijayo.

Kwani mwishoni mwa juma lililopita, vyombo vya habari nchini Ujerumani viliripoti kuwa chama chake cha CDU kilidai fedha kwa wafadhili ili kuweza kukutana na waziri mkuu wa jimbo hilo Juergen Rüttgers. Wüst alipozungumza na waandishi wa habari hakueleza kwa urefu sababu za kujiuzulu kwake lakini alisema, " Mtu hufikia wakati ambapo hujiuliza ikiwa bado anaweza kukisaidia chama chake katika kampeni za uchaguzi. Anaposhindwa kujibu "ndio" moja kwa moja, basi ni bora kumuachia kazi hiyo mtu mwengine." Rüttgers amesema kuwa yeye hakujua cho chote kuhusu malipo hayo, lakini aliongezea kuwa chama chake kilituma barua zinazoweza kutafsiriwa kama ni kudai fedha ili kupata fursa ya kukukutana nae. Gazeti la Süddeutsche Zeitung likieleza maoni yake juu ya ripoti za kashfa hiyo limesema, "chama kinachomtembeza waziri mkuu wake kama bidhaa, husaliti mali yake muhimu yaani uaminifu." Kwa upande mwingine, gazeti la Financial Times la Ujerumani katika toleo la hii leo limesema," hali ya mambo ni mbaya ikiwa wajasiriamali wanaweza kujinunulia wakati wa kuonana na wanasiasa kwa matumaini ya kukidhiwa mahitaji yao." Kujiuzulu kwa katibu mkuu Wüst kumetafsiriwa kama ni jitahada ya kutaka kumkinga Rüttgers lakini kwa sasa hakuna ishara kuwa lengo hilo limefanikiwa. Mwenyekiti wa chama cha SPD, Sigmar Gabriel alipozungumza na gazeti la Rheinische Post alisema," kama Rüttgers angekuwa na hata chembe ya uungwana basi angewajibika na angejiuzulu." Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa huenda ikawa vigumu kwa chama cha CDU kubakia madarakani pamoja na FDP katika serikali ya mkoa wa North Rhine Westphalia baada ya uchaguzi wa Mei 9. Ikiwa CDU kitapoteza mshirika wake FDP katika uchaguzi ujao, basi hilo litakuwa pigo kwa Kansela Merkel na pia vyama vya CDU na FDP vitapungukiwa na wingi wake katika baraza linalowakilisha serikali za mikoa-Bundesrat.

Mwandishi: Martin,P/DPA/RTRE

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed